Dodoma.Suala la mvua za kutengeneza kutoka nchi ya Thailand maarufu kwa jina la ‘Mvua za Lowassa’ liliwagonganisha mawaziri wawili wa Serikali bungeni jana.
Ubishi mkali ulizuka baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Terezya Huvisa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waliokuwa wakivutana juu ya ukweli kuhusu teknolojia hiyo.
Wakati Waziri Huvisa akisema kwamba hakuna utaalamu wa aina hiyo, Lukuvi alisimamia kumpinga na kusisitiza kuwa jambo hilo lipo.
Suala la mvua hizo lililetwa nchini na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa mwaka 2007, baada ya kufanya ziara Thailand ambako alivutiwa na utaalamu wa kutengeneza mvua na kuahidi kuuleta nchini.
Kutokana na mvutano wa mawaziri hao, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alipewa dakika moja na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama kutoa ufafanuzi ambapo aliunga mkono hoja ya Lukuvi.
Malumbano hayo yalisababishwa na swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo ambaye alihoji mpango wa kutengeneza mvua ulipoishia kwa kuwa Serikali imekuwa kimya.
“Sasa ni miaka takriban sita au saba tangu Serikali ilipokuja na mpango wa kutengeneza mvua ambao iliuchukua kutoka nchi za wenzetu, mpango huo umefikia wapi?” aliuliza.
Akijibu swali hilo, Waziri Huvisa alisema: “Mimi ni Rais wa Mazingira wa Afrika, nasema hakuna kitu kama hicho, si Marekani wala Malaysia ambao wanaweza kutengeneza mvua, hayo ni mabadiliko ya tabianchi tu.”
Waziri Lukuvi alionyesha kutokuridhishwa majibu hayo, ndipo aliposimama kutoa ufafanuzi na kusema Lowassa alikwenda Thailand ambako kuna utaalamu huo na kusisitiza kwamba upo na bado unaendelea kutumika hata Ujerumani wanakotumia mitambo ya kijeshi kusambaratisha mawingu.
Alisema kilichokwamisha mpango huo nchini ni ufinyu wa bajeti ya Serikali.
Baada ya majibu hayo, Lowassa alisimama akitaka kutetea wazo lake. Hata hivyo, kabla ya kumruhusu, Mhagama alimwomba akae chini kwanza ili atoe maelekezo.
“Mheshimiwa Lowassa, yeye siyo waziri na hivyo hastahili kutoa majibu ya Serikali, lakini kwa kutumia kanuni zetu bungeni kuhusu kutengeneza utaratibu mzuri wa kuongoza Bunge, naomba Lowassa usimame sasa walau kwa dakika moja au mbili utoe ufafanuzi,” alisema Mhagama.
Aliposimama Lowassa alizungumza kwa ufupi; “Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kukazia tu kuwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Lukuvi ndilo jibu sahihi.”
Majibu hayo yalisababisha Bunge kulipuka kwa shangwe.
Mara baada ya majibu ya Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza naye alisimama akitaka kutoa maelezo. Hata hivyo, Mhagama alisema inatosha na kuwaagiza mawaziri hao kukutana kuliangalia jambo hilo badala ya kuwa na majibu kinzani.
Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alitaka kujua ni kwa nini Serikali isirasimishe utaalamu wa kuleta mvua kutoka kwa waganga wa jadi walioko Mikoa ya Katavi na Rukwa ili maeneo yanayokabiliwa na ukame yapate mvua?
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipinga mpango huo na kusema hakuna kitu kama hicho isipokuwa wapo watu wenye utaalamu wa kuangalia mawingu yanayoendana na mvua.
Alisema watu wote wanaosema kuwa wanaweza kutengeneza mvua kwa imani za kishirikina ni waongo na hivyo hawapaswi kuaminiwa.
Alisema siyo wakati mwafaka kwa Serikali kushinikizwa kurasimisha utaalamu huo wa kuleta mvua kwa kuwa hakuna tafiti zozote zilizofanyika na kuthibitisha kuwapo kwake.
No comments:
Post a Comment