Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, CP Simon Sirro, akilionyesha gari hilo lililokuwa limeibwa kwa wanahabari (hawapo pichani).
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, CP Simon Sirro, amesema watu hao walimteka raia wa China mwanamke aitwaye Liu Hong (48) ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa Le Grande Cassino waliyemteka Oktoba 23 mwaka huu ambapo polisi walimkuta akiwa ndani ya chumba cha Hotel ya Palm Beach iliyoko Upanga jijini Dar es Salaam na walimkamata pia mtu aliyekuwa amekodi chumba hicho.
…Akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).
Alifafanua kuwa Oktoba 24 majira ya saa kumi na moja jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha polisi kilifanikiwa kumtia nguvuni raia mmoja wa China akiwa ndani ya chumba cha hoteli hiyo baada ya kuvunja mlango.
Madawa ya kulevya aina ya mirungi yaliyokamatwa na jeshi la polisi kwenye operesheni hiyo.
Sirro alisema baada ya kufungua chumba hicho walimkuta raia aliyetekwa akiwa hajitambui na akiwa na majereha usoni, pia palikutwa vipande vya taulo vyenye damu vilivyotumika kumfungia mikono ambapo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Ameeleza kuwa sababu kubwa ya utekaji nyara huo ilikuwa kumtaka majeruhi huyo atoe YEN 100,000 ambazo ni sawa na dola za Marekani 19,000.
…Sirro akionyesha mitambo ya kutengenezea pombe aina ya gongo iliyokamatwa wakati wa operesheni.
Katika hatua nyingine Sirro amesema kuwa wamefanikiwa kukamata wezi wa magari na kupatikana kwa gari la ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mkoa wa Morogoro, Capt. Innocent Philipo Dallu ambaye alikuwa ameegesha gari lake maeneo ya Mbezi Juu akitokea kanisani kwa ajili ya kuingia kwenye duka la vifaa vya ofisini na mashuleni ambapo gari hilo liliporwa.
…Akionyesha baadhi ya funguo bandia zilizokamatwa katika oparesheni hiyo.
Amesema jeshi lake limefanikiwa kulikamata gari hilo aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 400 DEH huko Kiwangwa, Bagamoyo mkoani Pwani likiwa na watu wawili ambao ni Ezekiel David (25) na Geofrey Nkwabi (52) na upelelezi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.