Mratibu wa maonyesho hayo, Ally Nchahaga (wa kwanza kulia) akizungumza na wanahabari.
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, atakuwa mgeni maalum katika kuzindua tamasha la maonyesho magari nchini lijulikanalo kama Automotive Festival (Autofest) linalotarajiwa kuonyesha magari mapya na ya kisasa katika viwanja vya Biafra, Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 28 hadi 30 mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mratibu wa Maonyesho hayo, Ally Nchahaga, amesema tamasha hilo litakuwa na matoleo mapya ya kila aina ya magari kama vile magari ya abiria, ya biashara, bodi za magari, mashine zinazohusiana na magari sambamba na pikipiki za kisasa na burudani mbalimbali za kusisimua zitakazofanywa katika kuyaendesha magari na kurukisha pikipiki juu kwa mbwembwe na kadhalika.
“Tukio hili linahusisha moja ya maonyesho muhimu na yenye mvuto katika ulimwengu wa vyombo vya moto na lengo letu ni kuendelea kuleta aina mbalimbali ya bidhaa za vyombo vya moto na huduma kwenye ‘Autofest’ ili wadau wapate kujifunza na kufurahia na kukidhi tamaa yao kwani magari yatakayokuwepo yanatumia teknolojia mpya na si ya zamani,” alisema Nchahaga.
Aidha alitaja viingilio katika tamasha hilo kuwa ni 10,000/= kwa sehemu ya kawaida, 5,000/= kwa watoto, 40,000/= ni kwa tiketi za VIP na 100,000/= kwa tiketi za musimu.
Kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Kuendesha tunaelekea wiki ya usalama barabarani, ni muhimu madereva kutoa fursa kwa madereva wenzao hata kama una haki”.
No comments:
Post a Comment