Sunday, January 7

SOPHIA SIMBA AWATAKA WANAWAKE KUJITOKEZA KUGOMBEA KWENYE UCHAGUZI

Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuiya ya wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) Sophia Simba amewataka wanawake kuandaa kushika nyadhifa mbalimbali kwa kujitokeza kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.


Sophia Simba amesema hayo leo alipokuwa akihutubia Kongamano la Wanawake wa UWT lenye lengo la kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yametimiza miaka 60.

" katika kuyaenzi Mapinduzi Matukufu kama wanawake ambao tulishiriki moja kwa moja ni wakati Wetu sasa nasi kuchukua nafasi za Uongozi katika Majimbo, Kata na Mitaa" amesema Sophia Simba.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda amemshukuru Mama Sophia Simba kwa kukubali mwaliko huo na kuweza kuvuka mpaka visiwani humo kwa ajilinya kutoa neno kwa wanawake ambao ni Nguzo ya Chama cha Mapinduzi.

Mama Chatanda aliendelea kushukuru kwa kusema UWT imara ya leo ni matokeo mazuri ya Malezi yake mazuri kwa wanawake akiwa Mwenyekiti.

"Nakumbuka nilitoka kwenye mikono yake na kunipa Baraka za kwenda kugombea jimbo la Korogwe na Hatimae nikafanikiwa kuwagaragaza wanaume hivyo alinitia moyo na kuniambia kuwa naweza " Amesema Mama Chatanda.

Aliongeza kuwa na hata alivyosikia nimechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa UWT Taifa aliiinuka na kunisemea vyema kila mahala kwa kutamka kuwa huu ni wakati sahii wa Maria kushika hii nafasi.

Kwa Upande wake Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa na Mwenyekiti wa Zanzibar Mama Zainabu Shomari aliendelea kwa kuwashukuru wajumbe na Watoa mada kwa kuweza kufika katika kongamano


 Mwenyekiti Mstaafu wa UWT Taifa, Sophia Simba akizungumza  na wanawake wa Jumuiya Visiwani Zanzibar katika Kongamano Maalum la kuhadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
 

Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania UWT Taifa Mary Chatanda,  akizungumza na wanawake wa Jumuiya ya wanawake wa Visiwani Zanzibar katika kongamano la kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
 

Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Bi Zainabu Shamari  akitoa neno kwa wajumbe.
 

 Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo akizungumza na wanawake wa Jumuiya hiyo wa Visiwani Zanzibar katika Kongamano Maalum la kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
 

 Naibu katibu Mkuu  UWT Taifa Bara, akizungumza na wajumbe

Thursday, September 9

COVID 19 ILIVYOSABABISHA MAJANGA KWA WANAFUNZI SIMANJIRO

 LIKIZO isiyo ya lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi kwenye Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kwa sababu ya ugonjwa COVID 19 ilisababisha wasichana 50 wasiendelee na masomo yao kutokana na kufungwa shule kwa takribani miezi mitatu mwaka jana.


Inaelezwa kuwa wanafunzi hao walishindwa kurudi masomoni kutokana na kuolewa au kupata ujauzito kutokana na baadhi ya wazee wa jamii ya kifugaji kutumia fursa hiyo ya likizo na kuwaoza mabinti hao.

Wanafunzi 50 wa shule ya msingi Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliacha shule kwa kuolewa wakiwa wadogo au kupata ujauzito kutokana na kuwa majumbani mwao kipindi cha likizo ya takribani miezi mitatu ya Covid 19.

Ofisa elimu wa shule za msingi Wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema likizo hiyo iliyotokana na Covid 19 ilisababisha wanafunzi hao kuacha masomo yao na hawakurudi shuleni baada ya shule kufunguliwa.
 
Tairo amesema shule zilifungwa kutokana na Covid 19 Machi 17 mwaka 2020 na kufunguliwa Juni 29 mwaka 2020 na wakabaini baadhi ya wanafunzi hawakurudi masomoni.

Mmoja kati ya viongozi wa kimila wa (Laigwanani) Yohana Ole Tiamongoi amesema, viongozi wa kimila wa eneo hilo wamekuwa wakikubaliana kwenye vikao vyao kila mara kuwa suala la watoto wa jamii ya kifugaji kupatiwa elimu liwe ni kipaumbele.  

“Jamii yetu imekuwa na mwamko wa kuwapatia elimu watoto wote wakifugaji wakiume na wakike japokuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wenzetu wanamtazamo hasi kwa mtoto wa kike kuwa bado ni wakuolewa na siyo kupata elimu,” amesema Ole Tiamongoi.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Arusha Mashariki, Usharika wa Purana, Enock Paulo amesema hivi sasa jamii ya kifugaji imebadilika kwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.

Mchungaji Paulo amesema jamii ya kifugaji inawasomesha watoto wakiume na watoto wakike wasidhani ni wakuolewa pekee kama walivyokuwa wana dhana potofu miaka iliyopita.

Amesema watoto wa kike wana msaada mkubwa kwa jamii ya kifugaji na anapaswa kuolewa akifikisha umri wa miaka 18  kwa asilimia kubwa wengi wameelimika kwenye suala la kusomesha watoto wao.

“Jamii ina kazi kubwa kuwapeleka shule watoto wao hasa wa kike kwani wanakuwa na uwezo mkubwa wa kusababisha mabadiliko kwenye familia na hata taifa kwa ujumla,” amesema mchungaji Paulo.

Amesema hivi sasa jamii ya kifugaji imekuwa na mwamko mkubwa wa kusomesha watoto wao ili kuhakikisha wanakuwa na chachu ya maendeleo kwa miaka inayokuja.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni anasema kwenye kijiji chake hakukuwa na mwanafunzi hata mmoja ambaye aliacha masomo kipindi cha likizo ya Covid 19 mwaka jana kwani wazazi na walezi, walishaelezwa kuwa wanafunzi wanapaswa kupatiwa elimu na siyo kuozeshwa wakiwa wadogo.

"Kwa kweli jamii ya kifugaji ya kimasai kwa upande wa Naisinyai imebadilika kwenye mtazamo wa kusomesha watoto hasa wakike kwani tunaona faida kubwa ya elimu hivi sasa" amesema Makeseni.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera, hivi karibuni alikutana na wakuu wa idara ya elimu na kuwaagiza kuandaa na kuweka mpango mkakati wa kupunguza na kukabiliana na tatizo la utoro na mimba za utotoni kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Dkt Serera amesema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakikatisha masomo yao kutokana na kupata ujauzito na wengi kushindwa kuhudhuria masomo baada ya kubebeshwa mimba bado wakiwa wanasoma.

"Wakuu wa idara za elimu mnapaswa kuweka mpango mkakati ambao utatekelezeka ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na  sekondari," amesema Dkt Serera.

Ametoa rai kwa wataalamu hao wa idara ya elimu, kuwashirikisha wazawa waliopata fursa ya kupata elimu, kushawishi  wazazi na walezi wa eneo hilo, kuwapeleka watoto wao shule.

Pia, amewaagiza wahahakikishe wanafunzi wanahudhuria masomo kwa vipindi vyote vya muhula wa masomo na kuimarisha mfumo wa elimu kwa watu wazima (MEMKWA).

SERIKALI YATENGA TRILIONI 2.03 KUZIKWAMUA KAYA ZOTE MASKINI NCHINI

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa neno la utangulizi wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akitoa neno la utangulizi wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Baadhi ya Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)  wakimsilikiza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TASAF iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakisikiliza mada kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyowasilishwa kwao na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga (hayupo pichani).



Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

SERIKALI imetenga kiasi cha shilingi trilioni 2.03 kwa ajili ya kuzikwamua kaya zote maskini nchini kutoka katika lindi la umaskini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kilichoanza 2020 mpaka 2023.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa semina ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.

Mhe. Mchengerwa amesema, kwa kuwa Serikali imetenga fedha za kutosha kuzifikia kaya zote maskini, amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kufanya ufuatiliaji ili kaya zote maskini zinazostahili kupata ruzuku zinanufaika.

“Kama kuna kaya yoyote maskini imesahaulika, nawaomba mtupatie taarifa ili watendaji wetu wazifikie na kukamilisha taratibu za kuwawezesha kupata ruzuku na kuongeza kuwa, katika utekelezaji wa awamu hii, Serikali itahakikisha kila Mtanzania anayestahili kunufaika na mpango huu, anapata ruzuku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema licha ya TASAF kuziwezesha kaya maskini kiuchumi, pia imewawezesha watoto wa kike wanaotoka kwenye kaya hizo maskini kupata elimu kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) ameipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa azma yake ya kutenga fedha za kutosha kuziwezesha kaya zote maskini nchini. Mhe. Polepole amesema, azma ya Mhe. Samia ya kutenga fedha hizo inaonesha nia ya dhati ya Serikali yake na Watendaji wake ya kuzikwamua kaya zote maskini.

Akiwasilisha mada kwa kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, idadi ya kaya za walengwa katika utekelezaji wa Mpango wa TASAF, Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu inatarajiwa kufikia milioni moja laki nne na nusu, hivyo wanufaika kwenye  kaya hizo watakuwa zaidi ya watu milioni 10.

Bw. Mwamanga amesema, ofisi yake imetekeleza zoezi la utambuzi wa kaya maskini kwa kushirikisha jamii na viongozi katika maeneo husika ili kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa awamu iliyopita. Katika kuhakikisha hakuna udanganyifu wakati wa zoezi la uandikishaji wa kaya maskini, Watendaji wanaohusika na zoezi hilo wamesainishwa kiapo cha kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu.

KESI YA MBOWE KUENDELEA KUUNGURUMA KESHO

 


KESI ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu itaendelea kusilizwa  kesho Septemba 10, 2021 mbele ya Jaji Mustapha Siyani baada ya kupangiwa Jaji huyo mpya kufuatia kujitoa kwa Jaji Elinazer  Luvanda aliyekuwa akiisikiliza mwanzo.

Leo Septemba 9,2021 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Magdalena Ntanda kesi amesema, kesi itaanza kuanzia saa 3 asubuhi na kwamba muda kamili utategemea magereza watawapeleka washitakiwa hao saa ngapi.

Awali, kesi hiyo ilipaswa kuanza kwa kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi lakini upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala ulipinga hatua hiyo kwa kuwasilisha mapingamizi yenye hoja nne kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba hati ya mashitaka ni batili na kuomba mahakama iwaondolee washitakiwa mashtaka hayo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga hoja hizo ukidai mahakama hiyo inayo mamlaka na hati ya mashtaka iko sahihi.

Kutokana na hali hiyo Jaji Elinazer Luvanda alitupilia mbali mapingamizi yote lakini kesi hiyo haikuweza kuendelea baada ya Mbowe kudai hana imani na jaji huyo katika kutenda haki na kumuomba ajitoe.

Katika Maelezo ya Mbowe ya kwa niniJaji ajitoe Katika  shauri Hilo  ametoa madai Mbalimbali ikiwa Ni Pamoja na  kutupilia Mbali kila Mapingamizi yanayowasilishwa na Upande wa Utetezi.

 Pia  amedai Kuwa  Mapingamizi yanayowasilishwa na upande wa Utetezi  hayazingatiwi na kwamba hata vifungu vya sheria wanavyotumia kama mfano kwenye kutetea mapingamizi yao havizingatiwi wakati wa kutoa  uamuzi  wake  jambo ambalo anadaia ni ukiukwaji wa haki za Msingi.

Mbowe alidai "Mheshimiwa Jaji naomba kunukuu taarifa....Jaji Elinaza Luvanda ni Mserikali na Tiss, yupo Mahakama ya Mafisadi kimkakati, anaelekezwa kumfunga Mbowe huku msajili akishughulika na Chadema, Rais atamuachia baada ya muda kila pingamizi atalitupilia mbali, haijalishi uhalali wake.'' mwisho wa kunukuu..." 

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni   Halfan  Hassan, Adamu  Kasekwa, Mohamed Abdillahi Ling'wenya ambao wanakabiliwa na mashitaka sita katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.

Mbowe anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili fedha kwa ajili vitendo vya kigaidi.

Inadaiwa washitakiwa kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Mei Mosi, 2020 na Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, walitenda kosa hilo.

Washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa walikula njama za kulipua vituo mbalimbali vya mafuta na katika mikutano isiyokuwa ya kisiasa na kusababisha hofu kwa wananchi kwa lengo la kuutishia umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mashitaka ya pili yanayomkabili  Mbowe inadaiwa katika tarehe hizo, katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, Mbowe aliwafadhili Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya, huku akiwa na lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo ya mafuta na mikusanyiko ya wananchi.

Wahamiaji Haramu 12 Waishiwa Nguvu,Njaa Yawakomoa,Wakamatwa Baada Ya Mtafutano Na Polisi

 Na Amiri Kilagalila,Njombe

 Wahamiaji haramu 12 kutoka Ethiopia waliovikimbia vikosi vya Ulinzi na usalama vya jeshi la polisi na uhamiaji  August 8 katika msako uliofanyika katika eneo la machungio la kijiji cha Uhambule wamekamatwa baada ya kushinda muda mrefu na njaa na kisha kuishiwa nguvu za kuendelea kukimbia katika mapori ya wilaya ya Wanging'ombe

 Hapo jana vikosi vya Ulinzi na usalama kutoka jeshi la polisi na uhamiaji baada ya kuskia Kuna hali isiyo ya kawaida katika eneo hilo vilifanya msako mkali katika Kijiji kinatajwa kutumika Sana Kama kituo Cha wahamiaji haramu Cha Uhambule kilichopo wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe  na Kisha kufanikiwa kuwashika wahamiaji 26 huku wengine wakifanikiwa kumbilia porini ambapo Leo wamekamatwa Tena.

 Kamanda kikosi cha uhamiaji kamishna msaidizi mwandamizi John Yindi baada ya kuwakamata watu hao amewapongeza wananchi wa eneo Hilo ambao wamekubali kutoa taarifa ya uwepo wa watu hao aambao walikuwa wakituma watu kuwasaidia kupata chakula mafichoni waliko.

 “Swala la ulinzi na usalama ni la kila mtanzania kwa hiyo tunaomba muendelee kutoa taarifa kwa viongozi weny wa vijiji mnavyoona watu kama hawa”alisema kamanda Yindi

 Nae Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issa ambaye alilazimika kuingia porini kuwasaka watu hao amesema Jana wamekamata 26 huku 15 wakifanikiwa kuwakimbia ambao Leo 12 wameshikwa ,hivyo wananchi waendelee kupinga uwepo wa watu hao Kijijini kwao kwakuwa hawajui na magaidi au vipi.

 “Hili eneo watu wameona ni sehemu ya kujificha sasa hivi watu wanaogopa hata kuingia kwenye majani kule,jana wamekamatwa 26 na wengine watano jumla wamekuwa 31 kwa hiyo wako wengi hawa hata ukiwapa basi hawatoshi bado watatu kwa kuwa tumewapata 12,kuna watu wameleta huku na kwa hali kama hii hatuwezi kujua kama ni wema”alisema Kamanda Issa

 Awali afisa Mtendaji wa Kijiji Cha Uhambule Yasinta Lupumbwe amesema wamewatia nguvuni watu hao na Kisha kuwaweka katika ofisi ya kata kwakuwa walianza kusimamishwa watu njiani na kuomba wanunuliwe chakula.

 “Saa nne asubuhi alinipa taarifa katibu wa uhambule kwamba porini kule kuna wahamiaji amekutana nao wakawa wanamuomba awanunulie chakula,tukaongea nao tukajua ni wale wale miongoni ambao walichukuliwa tarehe nane.Wananchi hawa wa kijiji cha uhambule wakaandaa uji na chakula wamekula”alisema Yasinta Lupumbwe

MARUFUKU MACHINGA KUFANYA BIASHARA KWENYE NJIA ZA WATEMBEA KWA MIGUU - RC MAKALLA

  - Asema agizo hilo ni kwa Wafanyabiashara Mkoa mzima.

 

- Amtaka DC Ilala na Uongozi wa Machinga kuweka utaratibu mzuri kuwapanga Machinga Kariakoo.


- Awapo mbinu ya kufunga baadhi ya Mitaa Kariakoo kwaajili ya kufanya Biashara.










-  Wamachinga wakiri kuingilia maeneo ya watembea kwa miguu na kuahidi kuhama

- Aeleza dhamira yake ya kuboresha mandhari ya Dar es salaam


MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam  Amos Makalla amepiga marufuku ufanyaji wa biashara kwenye maeneo hifadhi ya barabara zote za Mkoa huo baada ya utaratibu huo kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na ongezeko la ajali.

RC Makalla ametoa maelekezo hayo alipotembelea Soko la Kariakoo na kujionea kero ya ufanyaji biashara holela kwenye maeneo ya watembea kwa miguu.

Kutokana na hilo RC Makalla amewaelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kufanya kikao na Wafanyabiashara hao Jumatatu ya Septemba 13 na kuainisha maeneo ya kuwapeleka wote waliovamia hifadhi ya barabara.

Aidha RC Makalla amewaelekeza kuangalia utaratibu mzuri wa kufunga na kufungua baadhi ya mitaa Kariakoo kwaajili ya kufanya biashara Kutokana na ufinyu wa maeneo ili Waweze kupata riziki.

Hata hivyo RC Makalla amesema kwa tathimini aliyofanya amebaini hali ya ufanyaji biashara holela Dar es salaam ipo kwa kiwango kikubwa na kuwanyima watembea miguu haki zao za msingi.

Pamoja na hayo RC Makalla ameelekeza Manispaa zote za Mkoa huo kuweka vibao vya kuzuia biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu.

TANZANIA MWENYEJI WA ONESHO LA UTALII LA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

 KATIKA jitihada za kuvutia na kukuza uwekezaji katika sekta  ya Utalii Mawaziri wa Jumuiya  ya Afrika  Mashariki wanaoshughulikia Masuala ya wanyamapori  na utalii wamepitisha mkakati wa kutangaza utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Akiongea leo na wandishi wa habari Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema onyesho hilo litakuwa linafanyika kwa mzunguko katika nchi wanachama kila mwaka.

Amesema  kwa kutambua utalii ni sekta mtambuka onesha  hilo ni fursa muhimu ya kuhamasisha uhifadhi wa maliasili na malikale pamoja na kuchochea ukuaji wa utalii hususani utalii wa mikutano na matukio (MICE TOURISM) ambao ni zao jipya la utalii la kimkakati la kufanikisha kuongeza idadi ya watalii  katika ukanda wa Afrika Mashariki.

"Napenda kuwajulisha kuwa Tanzania ndio  itakuwa mwenyeji wa kwanza wa onesho hili  la utalii wa jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kauli mbiu ya onesha  hilo inasema " Utangazaji utalii stahimilivu  kwa maendeleo  jumuishi ya kijamii na uchumi, ".

Onesho la EARTE litafanyika jijini Arusha  Oktoba 2021 ambapo litajumuisha  siku tatu za maonesho  na siku tano za ziara maalum ya kutembelea vivutio vya utalii pamoja na fursa za utalii wa ndani kwa Tanzania bara na Zanzibar," Amesema Naibu Waziri Masanja.

Akizungumzia jinsi ugonjwa wa Corona ulivyoathiri sekta ya utalii ambapo kabla ya ugonjwa idadi ya watalii walifika Milioni 1.5  lakini baada ya kuzuka kwa ugonjwa  huo idadi ya watalii ilipungua na kufikia 620,000 huku makusanyo na mapato yakishuka.

" Kwa  sasa hali inaenda vizuri  baada Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan kuleta chanjo ya ugonjwa wa Corona ambapo namba ya watalii kuingia nchini inapanda," amesema Naibu Waziri Masanja.

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma.

Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma leo alipokua akitangaza juu ya kuanza kwa onesho la utalii kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tuesday, May 19

LICHA YA JANGA LA CORONA, HUDUMA ZA CHANJO NA UFUATILIAJI WA MAGONJWA YANAYOZUILIKA KWA CHANJO ZAENDELEA KWA UANGALIFU MKUBWA TANGA

Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.


Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.



***********************************

Na Mwandishi Maalum –Pangani,Tanga.

LICHA ya janga la Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya Mapafu (COVID19), Watoa huduma za chanjo na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo hizo Wilayani Pangani Mkoani Tanga zinaendelea kama kawaida huku wahudumu wakichukua tahadhari kubwa kwa kuzingatia muongozo wa kujikinga na janga hilo.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Tanga, Seif Shaib wakati wa ziara maalum ya usimamizi elekezi na uhamasishaji wa muongozo wa kujikinga na COVID 19 kwa watoa huduma hizo iliyofanywa na Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi.

Mratibu huyo wa Chanjo mkoa, Seif Shaib alisema chanjo zipo na huduma vituoni zinaendelea kwa kuzingatia muongozo.

Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi ameweza kushuhudia uwepo wa chanjo hizo kwenye vituo sambamba na watoa huduma wakifuata miongozo ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu kwa kuacha nafasi, uwapo wa maji safi na tiririka ya kunawa mikono na uvaaji barakoa.

“Watoa huduma za chanjo na wafuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto wanatakiwa waendelee kulingana na ratiba za chanjo zao lakini kwa kuzingitia muongozo wa kujikinga dhidi ya COVID 19.” Alisema Richard Magodi

Akielezea upande wa chanjo ya kukinga ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi (HPV) inayotolewa kwa wasichana wa umri wa miaka 14 ipo na inatolewa kwa walengwa hao.

“Chanjo hii ya HPV bado ipo lakini tunacho sisitiza kwa watoto ambao ratiba zao zinafikia hivi sasa wanaweza kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kamati za afya za kituo na Uongozi wa vijiji ama mtaa wahusishwe kuhamasisha wananchi kuwapeleka watoto wa kike wenye miaka 14 kupatiwa chanjo hiyo.” Alisema Magodi.

Sambamba na hilo, watoa huduma hao wametakiwa kufuatiliaji pia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hususani ugonjwa wa Surua, Polio na Pepopunda kwa watoto kwa kipindi hiki cha COVID19.

“Tuongeze jitihada za chanjo. Kwani tusipofanya hivyo watu wengi wanaweza kufariki na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

“Mfano tukiangalia takwimu za mwaka jana nchini Congo (DRC), ugonjwa wa Ebola uliua watu wachache kuliko Surua hii ni kutokana na kuipa kipaumbele Ebola na kuacha magonjwa yanayozuilika kwa chanjo nchini humo..Hivyo sisi Tanzania tunaendelea na huduma kwa kufuata muongo na tahadhari kubwa ikiwemo kuhimiza suala hilo la chanjo.” Alisema Magodi.

Aidha aliwataka watoa huduma hao kuzingatia matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki ngazi ya kituo (Tanzania Immunizations Registry -TImR) ili kuwa na takwimu sahihi na zitakazosaidia kufanya maamuzi bora kwa wakati kwenye ngazi ya kituo hadi ngazi ya Taifa.

“Katika vituo ambavyo tumetembelea Watumishi wameendelea kutumia mfumo huu kwa kuchanja na kuomba dawa, vifaa vya chanjo na kupata taarifa mbalimbali wanazozihitaji kwa wakati kupitia Vishishwambi (tablets) na wamefundishwa namna ya kutumia mfumo huo ambao umekuwa ukisaidia sana” alisema.

Awali Magodi aliweza kutembelea vituo vya chanjo hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, kituo cha chanjo Zahanati ya Bushiri, kituo chanjo Zahanati ya Madanga na kituo cha Chanjo Zahanati ya Kimang’a.

Nae Muuguzi mkunga wa Kituo cha Chanjo Zahanati ya Madanga alisema tokea uwepo wa COVID 19, wamechukua hatua mbalimbali na kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Madanga.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kimang’a, Dkt. Mohammed Kombo alisema wameweza kuchukua hatua dhidi ya COVID19 ikiwemo kutoa elimu kwa wanakijiji.

“Tumechukua tahadhari ya COVID19 ikiwemo pia kutoa elimu kwa wanakijiji. Lakini wanakijiji nao wameweka utaratibu mgeni akija kijijini hapa lazima ajitenge kwa maangalizio na kuchukuliwa taarifa zake mpaka tunapojiridhisha” alisema Dkt kombo.

Ziara ya usimamizi elekezi inaendelea tena katika Wilaya mbalimbali za mkoa huo wa Tanga kwa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na wadau wake.

UZALISHAJI WA VAZI KINGA (PPE) MUHIMBILI WAONGEZEKA KWA 400% HUKU MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA (TMDA) IKIRIDHIA NA KULITAMBUA


Mafundi wa kitengo cha Ushonaji MNH wakiendelea na ushonaji wa vazi la PPE 
Vazi la PPE likiwa tayari kupelekwa kwa wateja .
Mafundi wa Kitengo cha Ushonaji MNH wakiwa katika maandalizi ya awali ya ushonaji wa vazi la PPE
Muonekano wa vazi la PPE linaloshonwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
*******************************
  Dar es Salaam, Jumanne Mei 19, 2020.
  Uzalishaji wa vazi kinga linalovaliwa na watoa huduma ili kuhudumia wagonjwa walioambukizwa Covid 19 umeongezeka kutoka mavazi 120 hadi kufikia 600 kwa siku sawa na ongezeko la 400% katika kipindi cha mwezi mmoja tangu lilipozinduliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili Aprili 17, 2020.
 
 Mpaka sasa Hospitali imezalisha PPE 10,553 kati ya hizo 5,000 zimesambazwa MSD na nyingine katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya, Taasisi zisizo za kiserikali, Hospitali binafsi, makampuni, Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini. Tunaendelea kupokea mahitaji mbalimbali kwani sasa uwezo wa kuzalisha tunao. Bei ya PPE moja ni TZS. 50,000.
 
 Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilitambua vazi hili kupitia barua yenye Kumb. Na. BC.248/383/01/13 ya tarehe 23 Aprili, 2020 hivyo kuiruhusu Hospitali kuendelea kushona na kufanya usambazaji kote nchini.
 
 “Tunapenda kukufahamisha kuwa Mamlaka imepitia na kuridhia ombi lako la utambuzi wa nguo za kujikinga na maambukizi (coverall, shoe cover na apron) zinazotengenezwa na Muhimbili Tailoring Unit kwa kutumia malighafi ya nylon” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
 
 Kwa hiyo utengenezaji na usambazaji wa vifaa hivi unazingatia matumizi na uhifadhi unaofuata kanuni za udhibiti wa vifaa tiba nchini, The Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (Control of Medical Devices) Regulation, 2015 kama ambavyo tulivyoelekezwa na TMDA.  Pia vazi hili linafanyiwa utasishaji kabla ya kwenda kwa mtumiaji.

KORTI YAMUHUKUMU RAIA WA SOMALIA KWENDA JELA MIAKA MITATU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu raia wa Somalia, Jama Jes (50), kulipa faini ya Sh. Milioni moja ama kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini bila kuwa na kibali.

Hukumu hiyo imetolewa jana Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya mshtakiwa huyo kukiri shtaka lake na hivyo kutiwa hatiani.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Simba amesema amezingatia maombi ya mshtakiwa kuwa anategemewa na familia na hivyo, mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh. Milioni moja au kwenda jela miaka mitatu.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo , Wakili wa Serikali, Ngwijo Godfrey akisaidiana na  Sitta Shija, aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi mshtakiwa huyo ili fundisho kwa wengine.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuingia nchini bila kuwa na kibali katika kesi ya jinai namba 76/2020.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 12, 2020 mtaa wa Ohio wilaya ya Ilala, ambapo alikutwa hati ya kusafiria ilisha muda wake na hivyo kuishi nchini bila kuwa na kibali  huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.