Tuesday, May 19

LICHA YA JANGA LA CORONA, HUDUMA ZA CHANJO NA UFUATILIAJI WA MAGONJWA YANAYOZUILIKA KWA CHANJO ZAENDELEA KWA UANGALIFU MKUBWA TANGA

Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.


Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.



***********************************

Na Mwandishi Maalum –Pangani,Tanga.

LICHA ya janga la Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya Mapafu (COVID19), Watoa huduma za chanjo na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo hizo Wilayani Pangani Mkoani Tanga zinaendelea kama kawaida huku wahudumu wakichukua tahadhari kubwa kwa kuzingatia muongozo wa kujikinga na janga hilo.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Tanga, Seif Shaib wakati wa ziara maalum ya usimamizi elekezi na uhamasishaji wa muongozo wa kujikinga na COVID 19 kwa watoa huduma hizo iliyofanywa na Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi.

Mratibu huyo wa Chanjo mkoa, Seif Shaib alisema chanjo zipo na huduma vituoni zinaendelea kwa kuzingatia muongozo.

Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi ameweza kushuhudia uwepo wa chanjo hizo kwenye vituo sambamba na watoa huduma wakifuata miongozo ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu kwa kuacha nafasi, uwapo wa maji safi na tiririka ya kunawa mikono na uvaaji barakoa.

“Watoa huduma za chanjo na wafuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto wanatakiwa waendelee kulingana na ratiba za chanjo zao lakini kwa kuzingitia muongozo wa kujikinga dhidi ya COVID 19.” Alisema Richard Magodi

Akielezea upande wa chanjo ya kukinga ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi (HPV) inayotolewa kwa wasichana wa umri wa miaka 14 ipo na inatolewa kwa walengwa hao.

“Chanjo hii ya HPV bado ipo lakini tunacho sisitiza kwa watoto ambao ratiba zao zinafikia hivi sasa wanaweza kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kamati za afya za kituo na Uongozi wa vijiji ama mtaa wahusishwe kuhamasisha wananchi kuwapeleka watoto wa kike wenye miaka 14 kupatiwa chanjo hiyo.” Alisema Magodi.

Sambamba na hilo, watoa huduma hao wametakiwa kufuatiliaji pia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hususani ugonjwa wa Surua, Polio na Pepopunda kwa watoto kwa kipindi hiki cha COVID19.

“Tuongeze jitihada za chanjo. Kwani tusipofanya hivyo watu wengi wanaweza kufariki na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

“Mfano tukiangalia takwimu za mwaka jana nchini Congo (DRC), ugonjwa wa Ebola uliua watu wachache kuliko Surua hii ni kutokana na kuipa kipaumbele Ebola na kuacha magonjwa yanayozuilika kwa chanjo nchini humo..Hivyo sisi Tanzania tunaendelea na huduma kwa kufuata muongo na tahadhari kubwa ikiwemo kuhimiza suala hilo la chanjo.” Alisema Magodi.

Aidha aliwataka watoa huduma hao kuzingatia matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki ngazi ya kituo (Tanzania Immunizations Registry -TImR) ili kuwa na takwimu sahihi na zitakazosaidia kufanya maamuzi bora kwa wakati kwenye ngazi ya kituo hadi ngazi ya Taifa.

“Katika vituo ambavyo tumetembelea Watumishi wameendelea kutumia mfumo huu kwa kuchanja na kuomba dawa, vifaa vya chanjo na kupata taarifa mbalimbali wanazozihitaji kwa wakati kupitia Vishishwambi (tablets) na wamefundishwa namna ya kutumia mfumo huo ambao umekuwa ukisaidia sana” alisema.

Awali Magodi aliweza kutembelea vituo vya chanjo hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, kituo cha chanjo Zahanati ya Bushiri, kituo chanjo Zahanati ya Madanga na kituo cha Chanjo Zahanati ya Kimang’a.

Nae Muuguzi mkunga wa Kituo cha Chanjo Zahanati ya Madanga alisema tokea uwepo wa COVID 19, wamechukua hatua mbalimbali na kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Madanga.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kimang’a, Dkt. Mohammed Kombo alisema wameweza kuchukua hatua dhidi ya COVID19 ikiwemo kutoa elimu kwa wanakijiji.

“Tumechukua tahadhari ya COVID19 ikiwemo pia kutoa elimu kwa wanakijiji. Lakini wanakijiji nao wameweka utaratibu mgeni akija kijijini hapa lazima ajitenge kwa maangalizio na kuchukuliwa taarifa zake mpaka tunapojiridhisha” alisema Dkt kombo.

Ziara ya usimamizi elekezi inaendelea tena katika Wilaya mbalimbali za mkoa huo wa Tanga kwa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na wadau wake.

No comments:

Post a Comment