Friday, June 16

MREMA: RAIS MAGUFULI AWEKA HISTORIA MAPAMBANO YA UCHUMI


Mwanasiasa mkongwe nchini Augustine Lyatonga Mrema amesema Rais John Pombe Magufuli ameweka historia ya mapambano ya uchumi nchini kutokana na namna ambavyo analishughulikia suala la madini.

Bwana Mrema amesema kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton kusafiri usiku kucha kuja kuonana na Rais Magufuli na kukubali kuilipa Tanzania fedha zote ilizokoseshwa na Kampuni Acacia ni kielelezo kuwa sio tu kuwa ujumbe wake umefika lakini zaidi inadhihirisha kuwa madai yake dhidi ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini ni ya msingi.

“Ni kiongozi gani barani Afrika aliyethubutu kuishutumu kampuni ya nje kama alivyofanya Rais Magufuli halafu viongozi wake wakasafiri kuonana na kiongozi huyo kutaka suluhu kama alivyofanya Mwenyekiti huyo wa Barrick kwa Tanzania?”alihoji Bwana Mrema.

Mwanasiasa huyo aliungana na wito wa Rais Magufuli wa kuwataka baadhi ya watu wanaowahusisha viongozi wastaafu na taarifa za Tume za Rais za kuchunguza Makinikia.

“Si vizuri na kwamba si sheria kwa mtu yeyote kuwatukana au kuwashambulia marais wastaafu kama ilivyo kwa Rais aliye maradakani na sheria inatoa dhabu kali kwa wanaofanya hivyo” alieleza bwana Mrema.

Alibainisha kuwa kuwahusisha na taarifa hizo wakati hazijawataja kunaweza kusababisha kuigawa nchi na kuhatarisha mshikamano wa Taifa katika kipindi hiki ambacho watanzania wanapaswa kuwa kitu kimoja kumuunga mkono Rais wao na Serikali kwa hatua mbalimbali anazozichukua kuimarish uchumi.

“Tumekubali kikatiba Marais wetu waliopo madarakani na wastaafu walindwe kwa kuwa ndio ni msingi wa utulivu, amani na mshikamano wetu hivyo hatuna budi kuwaheshimu kwa kutekeleza hilo tulilokubaliana” alieleza Mrema.

Mwansiasa huyo alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge kumdhihaki Rais na kutozipa uzito jitihada zake za kutetea maslahi ya nchi na kuhoji mbona wananchi wa nchi nyingine kama Uingereza na Japan hawawabezi watawala wao akimaanisha Malkia na Mfalme.

“Baadhi ya wabunge wanaacha ajenda ya msingi ya kupambana na unyonyaji unaofanywa na makapuni ya madini badala yake wanaanzisha kampeni dhidi ya Rais”alieleza Bwana Mrema na kusema kuwa vitendo hivyo ni vya kichochezi, usaliti na ni vya kizandiki kwa Taifa.

Bwana Mrema alifafanua kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge kusema eti “Rais kama angekuwa makini” asingechukua hatua alizochukua za kuzuia mchanga na kuunda Tume ni kitendo cha kumdhallisha Rais ambaye alichaguliwa baada ya kuwashinda wagombea wengine alioshindana nao katika mbio za uchaguzi wa nafasi hiyo.

“Huyo Rais ‘makini’ ni yupi zaidi ya yule aliyewashinda wengine wote. Rais amekuja na mpango anautekeleza, tumuunge mkono…sisi ndio tuliomchagua” Alisisitiza bwana Mrema

Anabainisha kuwa haiwezekani mtu mkubwa na mashuhuri kama Profesa John Thornton atoke Canada kuja kuonana na Rais wetu tena akiwa na Balozi wa nchi yake iwe ni jambo la kupuuzwa.

Bwana Mrema alisema wako waliotaka Rais ataifishe mali za makampuni zinazotuhutumiwa kuiibia Tanzania lakini Rais Magufuli ametambua kuwa huu si wakati tena wa kutaifisha mali bali ni wa kutumia sheria zilizopo kupata haki na ndivyo anachofanya.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha TLP alilikumbusha Jeshi la Polisi wajibu wake wa kumlinda Rais dhidi ya kejeli za baadhi ya watu wakiwemo wabunge na kulitaka jeshi hilo kutofanya ajizi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo dhidi ya Rais na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Sheria ziko wazi kuhusu jambo hilo. Hata mimi mwenyewe niliwahi kushitakiwa mahakamani kwa kesi kama hiyo lakini nikashinda kwa kuwa waendesha mashitaka walishindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa nilifanya kosa hilo” alifafanua Mrema na kujinasibu kuwa akiwa mtu safi aliyelelewa vyema na Taifa lake kamwe hathubutu kumtusi au kumdhihaki kiongozi wa nchi yake.

Tangu Rais Magufuli aunde Tume za Kuchukunguza Mchanga wa madini kumwekuwepo na baadhi ya watu wanaopinga hatua hiyo kwa madai kuwa inaweza kuitia Tanzania katika mgogoro wa kisheria na kampuni ya Acacia.

Hata hivyo, baada ya ripoti ya Kamati ya Pili ya Uchunguzi kuwasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli hivi karibuni ambayo ilizidi kuonesha namna Kampuni hiyo ilivyoikosesha Serikali trilioni za shilingi, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton alikuja nchini kwa mashauriano na Rais.

Katika mazungumzo hayo muafaka ulifikiwa kuwa iundwe Tume ya mashauriano kati ya kampuni hiyo na Serikali huku kiongozi huyo wa Barrick akiahidi kurejeha fedha zote ambazo itabainika kuwa kampuni ya Acacia ilipaswa kuilipa Tanzania.

KAIMU KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI AWAASA WANACHAMA WA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA(SADC) KUPAMBANA NA MATENDO YA UHALIFU



Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amewaomba washiriki wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuhakikisha wanapambana kupunguza vitendo vya ujangili, biashara ya magendo, biashara ya binadamu, uhamiaji haramu kwani vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi zilizopo katika jumuiya hiyo, hivyo kupelekea kurudi nyuma kwa shughuli za maendeleo na uchumi.

Balozi Simba aliyasema hayo alipozungumza katika Mkutano huo uliojadili masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo, uliohusu masuala ya uhamiaji, ukimbizi, mbuga na wanyamapori katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya ya SADC, leo jijini Dar es Salaam.

“Hatuwezi kuendelea kiuchumi katika nchi zetu za wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, kama matendo ya ujangili,biashara ya binadamu, masuala ya wakimbizi, uhamiaji haramu hayajatafutiwa ufumbuzi, kwani haya yatazorotesha shughuli za kiuchumi ikiwepo utalii, hivyo ni bora tukayafanyia kazi maeneo hayo,” alisema Balozi Simba.

Akizungumza wakati wa uchangiaji mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jorge Cardoso, alisema uhalifu katika mipaka ya nchi wanachama ikiwemo uwindaji haramu wa pembe za ndovu, uhamiaji haramu,biashara ya binadamu na madawa ya kulevya lazima vidhibitiwe kwani vikiachwa mbeleni vitahatarisha Amani na utulivu uliopo katika nchi wanachama.

“Amani na utulivu katika nchi wanachama ni kichocheo cha mabadiliko ili kupiga hatua za kimaendeleo kwenda mbele na kushirikiana kukuza uchumi katika nchi wanachama wa SADC, hivyo yatupasa wote kwa pamoja kuunga mkono harakati za kukomesha vitendo vya uhalifu katika nchi na mipaka yetu,” alisema Cardoso.

Aidha washiriki wa mkutano huo kutoka katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Swaziland, Malawi, Zimbabwe kwa pamoja walikubaliana kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama katika nchi zao kudhibiti matendo yote yanayohatarisha amani na utulivu.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, akizungumza wakati wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa,Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jorge Cardoso, akizungumza wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya hiyo,uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, akiongoza Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika,Kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk. Anna Makakala.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye ,akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC),uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini, Profesa Jean Kitembo Mbilika ,akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC),uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu kutoka Malawi,Michael Gama ,akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC),uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Mkuu wa Uhamiaji kutoka nchini Swaziland,Makhosi Simelane ,akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC),uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Balozi wa Zimbabwe nchini, Walter Sande akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC),uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya (wapili kulia), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Watatu kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk. Anna Makakala.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere,leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).

MTOTO WA MIAKA SITA, DARASA LA KWANZA AZINDUA KITABU KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

JUNI 16, 2017: Dar es Salaam, Tanzania. Katika maadhimisho ya Siku yaMtoto wa Afrika mwaka huu mtoto mwenye umri wa miaka sita Ethan Theodore Yona anayesoma darasa la kwanza amezindua zana(App) yake ya android ambayo inaonesha shujaa wa hali ya juu akiwa ni muhusika anayejulikana kama EthanMan. Mhusika anaegemea upande wake ni mwenye kipaji kikubwa, ameandika vitabu vya kuvutia, kubuni michezo ya kijifunza na kuwapelekea watoto katika safari za mafunzo.

Ethan alianza kujishughulisha na mradi huo alipokuwa na umri wa miaka mitano katika shule ya awali ikiwa ni matokeo ya mapenzi yake katika michezo na kujifunza. “Kila mara nilikuwa na nguvu , kufurahia kujifunza vitu vipya na kupenda kucheza michezo mbalimbali. Siku moja niliwaambia wazazi wangu ningependa kuanzisha mhusika mkuu jasiri kwa kuzingatia ubora wangu. 


Baadaye waliniuliza ubora huo ni upi na nikawaambia mimi ninakipaji kikubwa na ninaweza kuwa kitu chochote ninachokipenda , naweza kuwa mchezaji soka, nyota wa muziki, mhandisi n.k. Na hivyo ndivyo wazo la mhusika shujaa mkuu lilivyoanza.”
 

Ethan alifanya kazi hiyo na mshauri wa teknolojia ya elimu katika i-LearnEast Africa, na ambayo inatoa kozi kwa njia ya mtandao na mafunzo ya mabadiliko kuunda mhusika huyo na kuanzisha kitabu chake cha kwanza cha picha alichokiita “Nitakapokuwa Mkubwa”. Tulivutiwa sana kufanya kazi na Ethan katika mradi huu. 


Inafurahisha kwamba mtoto mdogo namna hii kutaka kufanya jambo hili kubwa tulitaka kuwa sehemu ya huu mradi tangu mwanzo. Ikiwa ni kampuni ya ushauri katika masuala ya elimu tuliona umuhimu wa kujifunza ambao mradi huu utawapatia watoto. Mchango wa Ethan katika kuandaa kitabu hiki ni wa kushangaza,” alisema Ofisa Mtendaji wa Learn Tech, Deus Ntukamanzina. 


Zana hiyo na michezo ilianzishwa kwa ushirikiana na kampuni ya Tujenge Technology ambayo imejikita katika kuanzisha masuluhisho ya kidijitali ambayo yatawezesha kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii.

 


“Tulipoombwa kuanzisha michezo ya EthanMan tulifurahi. Kuwa sehemu ya mradi huu wa kipekee ndicho kilichotufanya kuingia katika teknolojia na kuianzisha. Mchango wetu ilikuwa ni kuunganisha mhusika EthanMan na vipaji vyake vingi katika jukwaa ambalo itakuwa ni rahisi kufikiwa na kuanzisha uzoefu mkubwa wa kutumia miongoni mwa watoto. Mchango wa ethan katika kuanzisha michezo ni wa hali ya juu, kwa sababu kila kitu kimejielekeza katika maisha yake kama mhusika. Tulikuwa na muda mzuri wa wa kuunda kile ambacho tunaamini kuwa ni bidhaa ya kwanza ya mchezo katika anga ya teknolojia nchini Tanzania.

Zana (App) ya EthnMan inapatikana kwa kupakua katika hifadhi ya michezo ya android , watoto wataweza kusoma vitabu, kucheza michezo. Na kuwa pamoja na muundaji wa EthanMan, Ethan Theodore Yona.

IJUMAA KAREEM KUTOKA KWA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM MHE. PAUL MAKONDA


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe Paul Makonda amekutana na Masheikh na Viongozi wa Misikitini zaidi ya Mia sita (600) ya Mkoa wa Dar es salaam.

Hatua hii ni muendelezo wa Mikutano yake na Makundi ya watu mbalimbali, ambapo katika kuenzi mwezi wa Mfungo wa Ramadhani.

Mhe Makonda ametoa vitu mbalimbali kama SADAKA KWA KILA KIONGOZI vifuatavyo kwa kila Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam :-
1. Mchele Kg 25
2. Ngano Kg 25
3. Sukari Kg 25
4. Mafuta ya kupikia Lita 20

Akizungumza na Masheikh na  Viongozi wa Dini ya KIISLAMU, Mhe Makonda kwanza amewapongeza kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali pamoja na kumuunga mkono Mhe, Rais, Dot. John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo anatekeleza utendaji wake wa kazi kwa kuhakikisha anaipeleka Tanzania kwenye nchi ya Uchumi na kipato cha kati kupitia mapinduzi ya VIWANDA.

Mhe Makonda pia, amewaomba viongozi wa Dini kuutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuhubiri AMANI, UTULIVU NA KUVUMILIANA katika kila mambo wanayofanya waumini wao.

Katika hatua nyingi, Mhe Makonda amefanikiwa KUWASHAWISHI wafanyabiashara haswa wa SUPERMARKET Mkoa wa Dar es salaam kufanya kazi mpaka saa sita za usiku, ili kutoa fursa kwa wananchi kujipatia mahitaji yao muhimu kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.

Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
16/06/2017

KESI YA UHUJUMU CHUMI;KITILYA NA WENZAKE WAPOKEA AWAMU YA KWANZA YA VIELELEZO KUTOKA NCHINI UINGEREZA



Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu Mstaafu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake umeieleza mahakama kuwa wamepokea awamu ya kwanza ya vielelezo kutoka nchini Uingereza.

Hayo yameelezwa Leo na wakili wa Serikali, Christopher Msigwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Msigwa ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanatarajia awamu ya pili ya vielelezo kuwasili nchini Tanzania wakati wowote kuanzia sasa.

Hata hivyo wakili wa utetezi, Mwanahamisi Adam ameuomba upande wa mashtaka kueleza muda muafaka ambao utatumika kwa vielelezo hivyo kufika nchini.

Aidha Hakimu Mkeha amewaambia upande wa mashtaka huo muda wowote wanaoutaja wahakikishe unaangukia ndani ya siku 14 na ikishindikana basi Juni 30 mwaka huu waeleze vielelezo hivyo vitafika ndani ya siku ngapi.

Miezi miwili iliyopita upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upalelezi dhidi ya kesi hiyo uliokuwa unafanywa ndani ya nchi umekamilika na kuwa bado wanasubiri upepelelezi unaofanywa nje ya nchi.

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni Miss Tanzania, 1996, Shose Sinare na Sioi Graham Solomon.Wanadaiwa kutenda makosa nane likiwemo la utakatishaji wa fedha wa kiasi cha USD milioni sita.

Mbali na shtaka la utakatishaji wa fedha, watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kula njama, kutoa nyaraka za uongo na kughushi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa Mkopo wa USD 550 wa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKIANO NA WADAU


Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Mdemu akitoa maelezo wakati wa Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wadau ( hawapo pichani)kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Mkoani Tabora ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma. Madhumuni ya Kikao kazi hicho ilikuwa ni kukutana wa wadau hao kwa lengo la kujadiliana, kubadilishana mawazo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo wadau hao pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wanakumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Wadau walioshiriki kikao hicho ni kutoka Mahakama, Takukuru, Magereza, Polisi, Wakala wa Barabara, Maliasili, Halmashauri, Mawakili wa Serikali, Wanasheria na wanajamii. Kushoto kwa Naibu Mwanasheria Mkuu Wakili Mfawidhierikali Kanda ya Tabora Bw. Jackson Bulashi na kulia ni Kamanda wa Takukuru Tabora Bw. Fidelis Kalungura.
Sehemu ya wadau ambao wamekuwa na mazungumzo na majadiliano na Ujumbe wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulioongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bw. Gerson Mdemu. Majadiliano hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Takukuru Mkoani Tabora siku ya Ijumaa ( June 16) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Wadau kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Mahakama, Polisi, Takukuru, Maliasili, Magereza, Halmashauri, Wakala wa Barabara,Mawakili wa Serikali na Wanasheria wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha majadiliano baina ya wadau hao na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo wameazimia kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa katika kikao hicho na kisha kupeana mrejesho.

Na Maura Mwingira, Tabora 

Katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo ( Juni 16) imekutana na wadau mbalimbali mkoani Tabora kwa madhumuni ya kujadiliana na kubadilishana mawazo yenye lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kiutendaji.

Akitoa maelezo ya awali mbele ya wadau hao kutoka taasisi za serikali zinazofanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Mdemu pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu kwa wadau hao pamoja na Ofisi yake kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.

“ Nyinyi ni wadau wetu muhimu sana sana, ni kwa sababu hiyo, katika wiki hii ya maadhimisho ya Utumishi wa Umma tukaamua kuja Mkoani Tabora ili tukutane nanyi.

Ni tumie basi, kikao hiki cha kazi kusisitiza kwenu, haja na umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu ili kwa pamoja tuisaidie na kuiwezesha Serikali itekeleze majukumu yake kwa ukamilifu”. Akasema Naibu Mwanasheria Mkuu.

Akaongeza kwamba, ni kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu licha ya kwamba kutaisaidia serikali lakini kubwa zaidi kutapuguza lawama na kunyosheana vidole.

“ Ni vema tutambue kuwa hakuna Taasisi ambayo inaweza kutekeleza majukumu yake pasipo kushirikiana na Taasisi nyingine. Lakini hili halilengi au haina maana ya kuingilia majukumu ya Taasisi au Mihimili mingine bali ni katika kutekeleza misingi na maadili ya utumishi wa umma” akabainisha Bw. Mdemu.

Wadau waliohudhuria majadiliano hayo ni kutoka Jeshi la Polisi, Mahakama, Magereza, Takukuru, Halmashauri, Wakala wa Barabara, na Idara ya Misitu na jamii. Akifafanua ziaidi hoja hiyo ya ushirikiano. Naibu Mwanasheria Mkuu ambaye ameambata na Wakurugenzi kutoka Divisheni zinazounda Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Pia amewataka wadau hao kuelezea kwa uwazi ni ushauri wa aina gani na katika eneo gani ambao wanauomba kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu.

“Pale mnapoleta mikataba yenu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ushauri au maoni, ni muhimu sana mkaweka wazi katika barua zenu ni maeneo gani gani ya mkataba mnayotaka ushauri au maoni, na kwa sababu gani. Badala ya kuleta maelezo ya mstari mmoja kwamba mnataka ushauri”.

Kasisitiza “ Jukumu letu kuu na la msingi na ambalo limeainishwa katika Katiba ni kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na wadau wengine. Lakini ili ushauri huo uweze kutolewa kwa ukamili,utaalamu na kwa mujibu wa sheria inayosimamia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu . Hivyo ni lazima basi wadau wetu wawe tayari kutoa ushirikiano kwa kuweka wazi maeneo wanayotaka kushauriwa. Tukifanya hivi tutakuwa tunaisaidia sana Serikali”.

Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewashukuru wadau hao kwa kutenga muda wao na kuitikia wito wa kukutana na kubadilishana na mawazo ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wao wadau hao wameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuamua safari hii kukutana na wadau wa Mkoa wa Tabora na kwamba mikutano ya aina hiyo ni muhimu sana katika uboreshaji wa uhusiano, ushirikiano na utetekelezaji wa majukumu ya kila taasisi.

Wadau hao pamoja na kutoka maoni yao na michango yao pia wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya utoaji wa ushauri kwa wakati.

Chadema wataka Katiba Jaji ya Warioba irejeshwe


Dar es Salaam. Chadema imesema iwapo Tanzania inataka kunufaika na rasilimali zake na kushinda vita vya kutetea utajiri wake inapaswa kwanza kurejesha katiba iliyopendekezwa na Jaji Joseph Warioba na si vinginevyo.
Akitoa msimamo wa chama kutokana na kile kinachoendelea baada ya kutolewa kwa ripoti mbili za Rais kuhusu mchanga wa dhahabu, leo (Ijumaa) Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji amesema suluhisho la kudumu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa ni kurejea katika katiba ya wananchi.
“Chadema tunasema kuwa haya yote tunayoyapigia kelele itakuwa ni kazi bure iwapo haturejeshi hoja ya katiba mpya.
“Katiba ya Warioba iliweka mapendekezo ya jinsi ya kulinda rasilimali za taifa na kama tungefuata hayo yote hili la sasa halingepaswa kuwa na mjadala mkubwa kiasi hiki,” amesema wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni.
Pia, chama hicho kimeitaka CCM kujipima na kujitafakari kama kinafaa kuendelea kuaminika kuongoza dola kutokana kushindwa kutetea vyema rasimali za taifa kwa kuruhusu mikataba mibovu.