Friday, April 17

SUMATRA yatangaza nauli mpya za Mabasi Ya Mikoani.......Nauli za Daladala Hazitabadilika



Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu jana imetangaza nauli mpya za usafiri ambapo Mabasi ya abiria ya masafa marefu nauli zake zikipungua huku daladala nauli zikibaki vile vile.

Akitangaza Viwango hivyo vipya vitakavyoanza kutumika tarehe 30 mwezi huu Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Gilliadi Ngewe alisema baada ya mchakato wa kupanga bei kukamilika, bei za mabasi ya Masafa ya mbali zimeshuka kwa asilimia 5.8 hadi 7.8 kwa kilometa kulingana na daraja la basi.
  
Ngewe amesema kuwa mabasi ya daraja ya chini yamepungua kutoka shilingi 34.8 hadi 34 kwa kilometa, Daraja la kawaida toka shillingi 46.1 hadi 42.5 kwa kilometa na daraja la kati toka shilingi 53.2 hadi 50.1 kwa kilometa huku dalalada zikishuka kwa shillingi 23 lakini kwa usumbufu wa chenji Nauli zitabaki vile vile.
  
Kwa Upande wa wamiliki wa daladala kupitia kwa mwenyekiti wao Sabri Mabrouk wao wanataka nauli iongezeke toka 400 ya sasa mpaka 600.

------

TAARIFA KWA UMMA
NAULI ZA MABASI YA MASAFA MAREFU NA MIJINI

1.0 UTANGULIZI

Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2014 bei ya mafuta yatumikayo katika vyombo vya usafiri wa abiria nchini ilianza kushuka. Kufuatia kushuka huko kwa bei, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ilikuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango vya juu vya nauli ambavyo viliwekwa na Mamlaka mwezi Aprili, 2013. Hivyo SUMATRA ikaamua kuandaa mikutano ya wadau kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu haja ya kurekebisha viwango vya nauli zilizopo.

Aidha, tarehe 09 Machi, 2015, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na SUMATRA (SUMATRA Consumer Consultative Council (SCCC)) liliwasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) maombi ya kushusha nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini.Katika maombi hayo Baraza liliainisha sababu za kuomba punguzo hilo kuwa ni kushuka kwa bei za mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya kutoka asilimia 25 hadi 10; punguzo hilo lilianza Julai, 2014.

1.1 MAOMBI
  1. Usafiri wa Mijini: Katika usafiri wa mijini, maombi yalikuwa ni kupunguza nauli kwa asilimia 25; hivyo kwa njia yenye umbali wa kilomita 10, nauli iliyopo sasa ya TZS 400 ilipendekezwa kushushwa hadi kufikia TZS 300.
  2. Usafiri wa Masafa Marefu: Maombi yalikuwa ni kushusha nauli iliyopo kwa kilometa moja anayosafiri abiria katika basi la kawaida kutoka TZS 36.89 hadi TZS 28.05; punguzo la asilimia 23.96. Aidha, kwa basi la hadhi ya juu (luxury bus) kushusha kutoka TZS 58.47 hadi TZS 47.19; punguzo la asilimia 19.29.

    2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MAPITIO YA NAULI
    SUMATRA iliyafanyia kazi maombi hayo kwa mujibu wa Sheria yaUdhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Sheria ya Bunge Na.9 ya Mwaka 2001, na Kanuni za Tozo za Mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma, watumiaji wa huduma pamoja na wananchi kwa ujumla ili kupata maoni yao. Ushirikishwaji huo ulifanywa kupitia mikutano iliyofanyika tarehe 9 Machi, 2015 Mkoani Mwanza; tarehe 12 Machi, 2015 Mkoani Kigoma; na tarehe 18 Machi, 2015 Jijini Dar es Salaam. Maoni yaliyotolewa katika mikutano hiyo yalizingatiwa katika tathmini na Mamlaka. 

    Taarifa ya tathmini na mapendekezo ya viwango vipya vya nauli iliwasilishwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA kwa ajili ya maamuzi.

    3.0 NAULI ZA MIJINI
    Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA ilikutana Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili, 2015 ili kupitia taarifa ya tathmini na mapendekezo ya viwango vya nauli kwa ajili ya maamuzi.

    3.1 Masuala Yaliyobainika
    Kufuatia tathmini iliyofanywa ya usafiri wa mijini, BODI ilibaini kwamba:
  1. Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati viwango vilivyopo sasa vilipoanza kutumika Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa lita katika vituo ulishuka mpaka TZS 1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
  2. Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili, 2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
  3. Gharama za mafuta zilikuwa muhimu kuzingatiwa pamoja na gharama nyinginezo, ambazo zilifikia asilimia 70 ya gharama za uendeshaji.
  4. Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na thamani ya shilingi na mabadiliko hayo yalipaswa kuzingatiwa katika kukokotoa viwango vya nauli.
  5. Punguzo la ushuru wa forodha kwa uagizaji wa mabasi mapya ulikuwa na faida katika kuchochea uingizaji wa mabasi mapya nchini ili kuboresha hali ya usafiri nchini. Hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo nchini kwa sasa hayakupata punguzo hilo kwa kuwa yaliingizwa kabla ya Julai, 2014 punguzo hilo lilipoanza kutumika.
  6. Mazingira ya uendeshaji na utoaji huduma za usafiri mijini yanapaswa kuzingatiwa ili kufikia viwango vya nauli ili kuifanya huduma ya usafiri kuwa endelevu. Kwa upekee, ongezeko la msongamano wa magari mijini na athari zake katika utoaji wa huduma za usafiri mijini zinapaswa kuzingatiwa.
  7. Gharama za utoaji huduma za usafiri mijini zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na punguzo la bei ya mafuta, ili kufikia viwango vya nauli vinavyostahili.
  8. Baada ya kuzingatia vigezo muhimu katika ukokotoaji wa nauli, punguzo lililojitokeza katika viwango vya nauli kikomo ni kama inavyobainishwa hapa chini: 

    Viwango Vya Nauli Kutokana na Ukokotoaji

Njia
Nauli ya Sasa
Nauli iliyokokotolewa
%
0 - 10 km (+CBD)
400
376.77
5.8
11 - 15 km
450
448.62
0.3
16 - 20 km
500
485.34
2.9
21 - 25 km
600
583.34
2.8
26 - 30 km
750
742.74
1

3.2 Maamuzi ya BODI
Baada ya kutafakari viwango vilivyotokana na ukokotoaji uliozingatia masuala muhimu yaliyoainishwa, BODI imeridhia viwango vya nauli vilivyopo sasa kuendelea kutumika.

Uamuzi huu unatokana na punguzo lililokokotolewa Kuwa dogo ikilinganishwa na viwango vilivyopo sasa. Aidha, viwango vilivyokokotolewa iwapo vitapitishwa vitasababisha usumbufu katika malipo.
  1. Viwango vya Nauli Mpya kwa Watu Wazima
    Viwango vipya vya nauli kikomo vya mabasi ya mjini vilivyoridhiwa kwa watu wazima ni kama ifuatavyo: 
    Viwango Vya Nauli Mjini Vilivyoridhiwa
Njia
Nauli ya Sasa


(TZS)
Viwango Vilivyoridhiwa


(TZS)
0 - 10 km (+CBD)
400
400
11 - 15 km
450
450
16 - 20 km
500
500
21 - 25 km
600
600
26 - 30 km
750
750

  1. Viwango vya Nauli Mpya kwa Wanafunzi 
    BODI imeamua kuwa nauli ya mwanafunzi nayo ibaki kama ilivyo nauli ya sasa ambapo mwanafunzi analipa TZS 200.
     
  1. VIWANGO VYA NAULI ZA MABASI YA MASAFA MAREFU
    BODI ilipokea tathmini kuhusu nauli za usafiri wa masafa marefu.

    4.1 Masuala Yaliyobainika
    Kufuatia tathmini iliyofanywa ya nauli kikomo za usafiri wa masafa marefu, BODI ilibaini kwamba:
  1. Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati viwango vya sasa vilipoanza kutumika Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa lita katika vituo ulishuka mpaka TZS 1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
  2. Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili, 2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
  3. Gharama za ununuzi wa mafuta zilikuwa muhimu kuzingatiwa pamoja na gharama nyinginezo, ambazo zilifikia asilimia 70 ya gharama za uendeshaji.
  4. Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na thamani ya shilingi na kwamba mabadiliko hayo yalipaswa kuzingatiwa katika kufikia viwango vya nauli.
  5. Punguzo la ushuru wa forodha kwa uingizaji wa mabasi mapya lilikuwa na athari chanya katika kuchochea uingizaji wa mabasi nchini. Hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo nchini kwa sasa hayakupata punguzo hilo kwa kuwa yaliingizwa kabla ya punguzo hilo kuanza kutumika.
  6. Katika ukokotoaji wa nauli ni muhimu kuzingatia madaraja ya mabasi kama yalivyoelekezwa katika Kanuni za Huduma za Abiria, 2014 (The Road Transport (Passenger Service) Regulations, 2014 zinazoainisha madaraja manne ya mabasi;daraja la kawaida la chini, daraja la kawaida la juu, daraja la hadhi ya kati na daraja la Juu.
  7. Gharama za utoaji huduma za usafiri kwa ujumla wake zinapaswa kuzingatiwa kwa madaraja mbalimbali ili kufikia viwango vya nauli vinavyostahili.
  8. Udhibiti wa nauli unapaswa kujielekeza katika madaraja matatu yafuatayo: (1) daraja la kawaida la chini, (2) daraja la kawaida la juu na (3)daraja la hadhi ya Kati ili kutimiza wajibu wa kuwalinda watumiaji wenye kipato cha chini.

    4.2 Maamuzi ya BODI
    Baada ya kutafakari tarifa iliyowasilishwa BODI iliridhia viwango vipya vya juu vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu kuwa kama vinavyoonyeshwa hapo chini: 
    Viwango Vipya vya Nauli za Mabasi ya Masafa Marefu

Daraja la Basi
Nauli ya Sasa


(TZS/Abiria/Km)
Viwango Vipya vya Nauli Vilivyoridhiwa


(TZS/Abiria/Km)

Daraja la Kawaida la Chini

(Lower Ordinary bus -Lami
36.89
34.00

Daraja la Kawaida la Chini

Lower Ordinary Bus) - Vumbi
46.11
42.50

Daraja la Kawaida la Juu

(Upper Ordinary Bus)
-
44.96

Daraja la Kati

(Semi-Luxury Bus)
53.22
50.13


BODI pia imeamua kwamba nauli za mabasi ya hadhi ya juu ( luxury bus) hazitadhibitiwa ili kuchochea ubunifu katika utoaji huduma na ushindani kati ya huduma za barabara na njia nyinginezo za usafiri.

Mamlaka imeandaa majedwali ya nauli kwa kuzingatia viwango vipya. Majedwali hayo yanaweza kupatikana katika tovuti ya Mamlaka www.sumatra.go.tz.

HITIMISHO

Viwango hivi vipya vinapaswa kuanza kutumika siku 14 baada ya taarifa kutolewa kwa umma. Hivyo basi viwango hivi vitaanza rasmi tarehe 30 Aprili, 2015.

Wamiliki wa mabasi pamoja wafanyakazi wao wanaagizwa kutoza viwango vya nauli vilivyoridhiwa na Mamlaka.

Aidha, abiria na wananchi kwa ujumla wanahamasishwa kutoa taarifa SUMATRA kupitia namba za simu za bure ambazo ni 0800110019 na 0800110020 pale wanapotozwa nauli ya juu zaidi ya nauli kikomo iliyoridhiwa.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
SUMATRA
15 Aprili, 2015 

Zitto Kabwe: Sitaki kulumbana na CHADEMA

Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawezi kulumbana na viongozi wa chama chake cha zamani cha Chadema kwa kuwa anachofanya sasa ni kutafuta wanachama wa chama chake kipya. 
 
Zitto alisema hayo juzi mjini Morogoro wakati wa mkutano wa ziara ya uzinduzi wa chama hicho uliofanyika katika kiwanja cha ndege mjini hapa.
 
Akihutubia huku akishangiliwa na wananchi, Zitto aliwataka kumpima na kumchuja yeye kwa matendo yake na kwamba kwa sasa jitihada zake amezielekeza mikoani kupata wanachama.
 
“Nimekuwa nikisikia maneno maneno mengi kutoka kwa viongozi wangu wa zamani lakini nawaheshimu na sitoweza kuwajibu kwani siasa za chuki kwa sasa zimepitwa na wakati, ninachofanya ni kukijenga chama,”alisema Zitto.
 
Kiongozi huyo alisema Morogoro ni moja ya mkoa unayoifanya nchi kukosa maendeleo kutokana na viwanda vingi kubinafsishwa na hivyo kutokuwa na faida kwa wananchi.
 
“Morogoro ni mkoa wa sita katika kuchangia pato la Taifa na takribani Sh2.2 trilioni zimekuwa zikipatikana kwa ajili ya maendeleo ya watu wa mkoa huo,” alisema Zitto.
 
Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira aliwataka wanawake nchini kuacha kushiriki siasa za vurugu na malumbano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
 
Mghwira alisema ni vyema wakaangalia namna gani nchi inakua kiuchumi na watoto na vijana wanapata elimu iliyo bora ambayo itawafanya kufanya kazi kwa uzalendo.
 
Aliwataka wananchi kuwa na taratibu za kuwakumbuka mashujaa wa Taifa hasa kwa mambo mema na mzuri waliyoyafanya wakati wa uhai wao.
 
Mpaka sasa chama hicho cha ACT kimefanya mikutano yake ya uzinduzi katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa na Morogoro 

Mkwara wa Gwajima kwa Polisi wazaa matunda.....Mahojiano Yasitishwa Kusubiri Uamuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali



Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda. 
 
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam la kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo limesitishwa kusubiri utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
 
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima alimweleza mwandishi jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi mteja wake leo hatafika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa imepangwa mpaka hoja hizo za kisheria zitakapotolewa uamuzi.
 
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa na kiongozi huyo akieleza kuwa hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu barua aliyoliandikia kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
 
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka za helikopta ya kanisa.
 
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
 
“Siwezi kuwasilisha kwa mdomo kwa kuwa hizi si mali za Gwajima… ni mali ya taasisi na si vitu vyake binafsi,” alisema wakili huyo.
 
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya alisema: “Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi nyaraka mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi kutaka nyaraka hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
 
Kauli ya Kova
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo, Kamanda Kova alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo alivyoagizwa na Polisi siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea hakuja navyo ndipo nitakapotoa tamko langu la mwisho.
 
“Nitazungumziaje hili? Si hadi itokee hakuja na vielelezo na kama akija navyo halafu mimi nimeongea tofauti, nimeona italeta malumbano kati yangu na yeye na mimi sitaki ifikie huko.
 
“Kuna mambo mengi ya kufanya hivyo nitalitolea tamko la mwisho kwa waandishi wa habari kuhusu mchungaji Gwajima kama itatokea hivyo ili tuendelee na mambo mengine.”
  
Kwa msisitizo zaidi
Mallya alisema nchi inaongozwa kwa sheria, hivyo kila kitu kinatakiwa kiwe cha kisheria na kwamba wameiandikia polisi kuitaka waombe nyaraka hizo kimaandishi na kuonyesha vifungu vya sheria vinavyowaongoza kuziomba badala ya kusema kwa mdomo kwa sababu vitu hivyo ni vya kanisa na siyo vya Gwajima peke yake.
 
Askofu Gwajima alihojiwa na Polisi, Kanda ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtolea maneno makali Polycarp Kardinali Pengo baada ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kutoa tamko lililotofautiana na la viongozi wa Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu suala la Katiba