Lugha ya Kiswahili ina utajiri mkubwa wa msamiati na istilahi anuwai. Msamiati ni jumala ya maneno yote yaliyomo katika lugha fulani, sio kama vile baadhi ya walimu wa shule za msingi wanavyowakaririsha wanafunzi wao kuwa “ msamiati” ni maneno magumu.
Pamoja na ukweli kwamba Kiswahili kina heshima kubwa kwa kuwa wazungumzajii wake wengi ni waungwana, wastaarabu na wenye heshima ya kutosha. Lakini ipo baadhi ya misamiati kadhaa wa kadhaa bado inayokanganya ikilinganishwa na uhalisia au dhana zinazorejelewa.
Kwa niaba ya familia ya ‘Wafia Kiswahili Tanzania (wakita)’, leo ninaomba kuchokoza mjadala kuhusu misamiati miwili tu katika lugha hii aushi ya Kiswahili. Kwa hakika misamiati hii si migeni katika masikio yetu. Mara nyingi tunaisikia na kuitumia misamiti hii katika muktadha mbalimbali. Misamiati yenyewe ni “ UPINZANI “ na “ USHINDANI “.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la pili, (TUKI), wameeleza neno upinzani kuwa ni “hali ya kupingana, ubishani au ukinzani, Pia wameeleza kama kuna kundi la upande unaopingana”
Kwa mantiki hii, hatuwezi kukosoa ikisemwa kuwa, upinzani msingi wake ni kupingana. Na huenda haitakuwa kosa ikiongezwa zaidi kwamba, mpingaji mzuri ni yule apingaye mwanzo mwisho na sio kubip kupinga.
Dhana hii ya kupinga inafanya kuwe na pande mbili zenye ukinzani wa dawamu hata kwa jambo lenye faida au matokeo bora kwa pande zote. Muda wa kuwa ni wapinzani, hakuna haja ya kukiri ubora wala ufanisi wa jambo lolote lile la mpinzani wako.
Kwa upande wa neno “ ushindani”. Neno hili limeelezwa katika ukurasa wa 443 wa kamusi tajwa kuwa, ni “ hali ya kushindana” kwa dhana ya kushindana wachache ndio pengine hawataelewa haraka kwamba, katika kushindana lazima pawapo na mshindi wa mashindano fulani. Matokeo ya mashindano hayo ni upande mmoja kushinda na mwingine kushindwa. Waswahili katika mawanda haya ya mashindano hawakutafuna maneno, Waswahili husema, “ asiyekubali kushundwa si mshindani” Msemo huu chambilecho kwa wanamichezo wote ulimwenguni.
Kwa msemo huu wa Waswahili, pengine huashiria uungwana na maafakiano yao katika kuridhia kushinda au kushindwa katika mashindano yao, hata kama mshindi atapewa zawadi kubwa au mshindwa ataadhibiwa. Kwa hoja na maelezo hayo, sina shaka haiwezi kukuchukua muda mrefu kutanabahi kuwa, kushindana si kupingana. Hata kama upo wakati fulani washindanao huhitajika kupingana , kupingana huko kutakuwa kwa minajili ya kufanya mashindano yao kuwa hai zaidi. Jambo hili litaingia akilini kwa kueleweka kama uhai wa mashindano si uhasama mchezoni.
Dhana hii ya uhai wa mashindano na sio uhasama mchezoni ndio ilifanya wadau wa michezo kuwa na dhana ya ustaarabu mchezoni “ fair play “ . kushindana bila ya uadui mchezoni.
Hali inakuwa tofauti kabisa tukizibeba dhana hizi mbili kutoka katika lugha ya kimombo kuzifanyia tafsiri sisisi (tafsiri ya moja kwa moja) kuwa katika Kiswahili.
Neno la Kiingereza “oppose “ lenye maana ya Kiswahili kupinga na “compete “ lenye maana ya Kiswahili shindana .
Katika medani ya kisiasa za nchi yetu, neno moja limekita mizizi zaidi ya jingine. Na kama kuna kosa tulilolifanya sisi Waswahili katika medani ya siasa zetu hapa nchini, basi ni pale mnamo mwaka 1992 wakati tulivyoridhia mfumo wa vya vingi, na kuviita vyama vipya vyote kwa neno hili la “upinzani” nitafafanua.
Hebu sasa tudodose kidogo uhai na uhalali wa neno“upinzani” katika tasnia ya siasa ya nchi sanjari na ukomavu wa demokrasia na maendeleo shirikishi katika nchi yetu.
Kwa kuwa imeshaelezwa hapo juu maana ya neno “ upinzani” ambalo likinyambuliwa zaidi linaweza kutupa maneno kama : pinga, pingana, pingia, pingania, pinzana, nk.
Msamiati huu huu mmoja tu, tena kwa haraka unaweza usionekane kama una madhara katika jicho la demokrasia na maendeleo ya taifa lakini ukitazamwa kwa jicho la tatu itabainika kuwa huu msamiati ni shida! Hususan katika siasa za nchi za Afrika.
Kwa mfano, ni mara ngapi walikaririwa hao wanaoitwa wapinzani, wakisema serikali hii iliyo madarakani haijafanya kitu cha maana ( rejea hotuba maarufu ya mchungaji mmoja ndani Bunge la awamu ya nne), na wakati mwingine kaenda mbali zaidi kiasi cha kusema, serikali haijafanya lolote tangu uhuru. Kwa upande wa chama ambacho kinaona kinapingwa nacho kinasikika kikieleza mafanikio yao ambayo hata mimi binafsi ninyaona pasi miwani ( kama : mtandao wa barabara nchi nzima, Chuo kikuu cha Dodoama, uhuru wa maoni , nk).
Kwa upande wa pili wa shilingi , ni mara ngapi hao waitwao wapinzani wameishauri serikali kwa namna bora zaidi kuhusu maendeleo ya nchi yetu, lakini serikali inakataa ushauru wao tena bila hoja za msingi. (Rejea ushauri wa kuahirisha uchaguzi mkuu, kutazamwa upya kwa mchakato wa katiba, kutofanya haraka kupitisha baadhi ya miswaada mbalimbali kama ya gesi na mafuta, nk).
Ni nani katika chama tawala anaweza kusema hadharani kuhusu ushauri mzuri uliyowahi kutolewa na waitwao wapinzani ambao serikali umeuchukua kwa manufaa ya nchi yetu? Iwapo halipo jambo lililozingatiwa na serikali kutoka upande wa vyama vinavyoitwa vya upinzani wala hakuna wa kulaumiwa. Kwani haitarajiwi Yanga itoe ushauri mzuri kwa Simba unaohusu mafanikio yao. Yanga ikiwa ina mchezo wa kimataifa, Simba ndio huona hiyo ni fursa nzuri zaidi ya kuikomoa Yanga kwa kushangilia wapinzani wa Yanga ili kuipa fedheha .
Ni mara ngapi, mwanachama mmoja akihama chama kimoja cha siasa na kwenda kingine kama ilivyokuwa hivi kwa mbunge mmoja kutoka NSSR kwenda chama cha ACT , NSSR wanaweza kumuona mbunge huyo ni msaliti hata kama alikuwa na sababu nzuri zaidi za kuhama kuliko kubaki katika chama chake cha zamani. Kwa nini? Bila shaka, ni dhahiri kuwa , mwanachama huyo hutafsiriwa kuwa amekwenda upinzani.
Cha kujiuliza, hapa ni kwamba, mbona vigogo hawa wa pande mbili za siasa, kwa maana wale wanaoitwa wapinzani na wanaona wanapingwa, nje ya uga wa siasa wanaunganishwa na mambo kadhaa, kama dini, makabila, kanda zao, na timu za michezo, nk. Lakini mara tu wanapokuwa ndani ya majukwaa ya kisiasa huwezi kuamami kama ndio hao hao wakutanao kanisani/misikitini au Jangwani na Msimbazi. Inachekesha kidogo, ukijiuliza unaweza kudhani kwamba, mkataba wa kupingana kwao ni katika siasa pekee.
Kwa vile msamiati huu wa “upinzani” hauwezi kuwapika wanasiasa katika chungu kimoja , ninatoa hoja kuwa tufikiri msamiati mbadala wa kufanya mijadala ya kiungwana, yenye afya njema kwa nchi yetu ili nchi inufaike na uweledi wa kila mwananchi kutoka upande wowote ule wa siasa aliyopo. Kwa maelezo hayo, sasa hoja yangu ni kwamba, msamiati “ushindani” unafaa zaidi katika mazingira ya hali ya siasa zetu za Kiafrika. Msamiati huu utafanya uwanja wa siasa uwe na upinzani usio na uhasama kuliko ilivyo sasa. Wasiwasi wangu kama wasemavyo Waswahili “ wasiwasi ndio akili “ likiachiwa zaidi neno hili -upinzani katika ya siasa zetu nchini, hatima yake haitakuwa njema kutokana na uzoefu wa miaka zaidi 20 ndani ya siasa za ushindani. Sina shaka ya kuwa neno ushindani wa siasa ni mwafaka zaidi kama tunataka maendeleo shirikishi katika taifa letu. Ndugu zangu ebu tuone , nchi ikiwa ni bingwa wa uchumi lakini nchi yetu haimtumii ipasavyo katika mambo ya uchumi …..kisa yeye ni mpinzani……. Kweli ni sawa katika nchi kama hii au kuwa na mtaalamu wa mambo ya sheria lakini hatumiki kikamilifu , maoni yangu ni kuwa, uwanja wa sheria ungemhitaji sana mtu wa namna hii katika maendeleo ya taifa letu, lakini wapii na wengine wengi tu…..tunakosa michango yao kikamilifu kwa msamiati wa upinzani!
Nimeshawishika kufikiri mbadala huu baada ya tafakuri ya kina, kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa Ninafikiri neno ushindani litatuweka pamoja sote na kushiriki kikamilifu katika harakati za maendeleo kama taifa huru.
Dhana hii ya ushindani itafanya wanaoshindana kuwa makini zaidi, kusoma mbinu za mchezo za mshindani wake, kutumia udhaifu wa mshindani, kuboresha pale penye upungufu, nk.
Kwa dhana hii ya ushindani inaweza kufanya siku moja kuwe hata na kamati ya pamoja ya kushughulikia namna ya kuendesha, kutathmini na kuboresha mashindano yao. Yaani kuwe na kamati ya mseto ya mashindano . jambo hili si rahisi kwa ile dhana upinzani kuwa na kamati ya mseto ya upinzani.
Tukifikia hatua hii, inafikiriwa, hapatakuwa na haja ya kukanusha mazuri yaliyofanywa na mshindani mwenzio. Haitapatikana haja ya kukataa ushauri wa mshindani mwingine.
Hivi ni nani katika hatua hii awezaye kupinga mchango wa Mtanzania mwingine iwapo mchango huo utaonekana una tija kwa jamii nzima ?, Lakini kwa dhana ile ya upinzani, ni nani hata kwa bahati nasibu atakayechukua mawazo ya anayempinga hata kama ni mazuri ? Ipo wazi kabisa, kama mtu anakupinga itatokeaje siku moja akupatie mbinu ifaayo? Kama si miujiza nini! Hivi kweli Yanga ipo siku itaamba mbinu ya ushindi Simba au kinyume chake ?
Kwa dhana ya ushindani, ni nani atakayechukia na kuchukiwa kwa kuitwa mshindani ?,
Kwa mantiki ile ile, ni nani atakayekataa kushindwa kama ikitokea bahati mbaya ya kushindwa? Lakini kwa kuwa kwa sasa katika siasa zetu kuna dhana ya upinzani, basi hata pale chama kitapoamua yasiyotarajiwa na wengi pana uwezekano wa kutokea kwa sintofahamu kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni mjini Dodoma. Kwa nini, kwa sababu katika dhana ya upinzani, hakuna ustaarabu wa kukubali kushundwa lakini katika kushindana inasemwa ,“ Asiyekubali kushindwa si mshindani”
Kwa dhana hii ya ushindani inaweza kutoa picha nzuri zaidi hata katika uwanja wa Bunge. Kwa mfano , anayeitwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, kwa taaluma ya semantiki (elimu maana) angeweza kuitwa mpinzani mkuu bungeni lakini kwa dhana hii ya ushindani, angeweza kujulikana kama kiongozi wa kambi ya ushindani bungeni, hivyo ni mshindani mkuu. Ni Mtanzania gani angemuona kiongozi huyu ni mpngaji wa kila jambo ndani ya Bunge kama ilivyo sasa ambapo kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni ndiye pengine huonekana kuwa ni mpinzani mkuu.
Iwapo atatokea mtu akasaili juu ya kitu gani kinashindaniwa. Pamoja na majibu mengine angeweza kujibiwa kuwa , Ikulu ndio inashindaniwa. Mwingine akihoji ni kwa vipi wanashindana, angeweza pia kujibiwa , ni kwa hoja wanashindana, na hoja zenyewe ni za nguvu, ambapo hoja za nguvu zaidi ndizo zitakazo shinda. Kinyume chake ni kwamba, hoja za nguvu zaidi ndizo zitakazopingwa kwa dhana ya upinzani.
Mfano hai, ni pale Mheshimwa Hamisi Kigwangwala baada ya kukosa ridhaa ya chama chake kuteuliwa kuwania nafasi ya urais mwaka 2015, mara moja aliandika katika ukurasa wake wa facebook pengine na sehemu nyingine kuwa , amekubali matokeo , hivyo anatazama mbele zaidi katika siasa kupitia chama chake ( huyu alishindana kisiasa ).
Pia kwa dhana ile ya upinzani, ninakumbuka zaidi maneno ya mchungaji mashuhuri pale bungeni aliposema ,“ Mimi kama mpinzani sikuja kupongeza hapa bungeni, ninakukosoa ufanye kazi yako vizuri”
Wakati washindani wapo tayari kukiri, kupongeza na kukubali hata matokeo lakini mpinzani hana cha kupongeza na upo uwezekano hata wa kukataa matokeo.
Ndugu zangu, kama hatuwezi kukubaliana, kuelewana na kuafikiana na kupeana mbinu za mafaniko kwa kigezo tu cha upinzani wa kisiasa. Kwa nini sasa isitafutwe busara ya kufikiri vinginevyo ?
Ninatoa hoja kuwa kwa vile upinzani haujatusaidia kwa zaidi miaka 20 hapa nchini, tugeukie katika ushindani. Sina shaka utatoa matokeo chanya kwa maendeleo na mustakabali wa taifa letu.
Upinzani hautakiwa Tanzania, sasa tufikiri ushindani wa siasa.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika.
Mwenyekiti wa Wafia KiswahiliTanzania (Wakita)
Majid Mswahili.