NI KWENYE MAGARI YA SERIKALI,TANESCO,MALIASILI,MABILIONI YA JK,AFYA NA MISHAHARA HEWA
Daniel Mjema Dodoma na Fidelis Butahe
WABUNGE jana waliijia juu Serikali kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na ufisadi ulijitokeza kwenye taasisi zake mbalimbali katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana.
Hasira za wabunge hao zilitokana na ripoti tatu za Kamati za Bunge; Mashirika ya Umma (POAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC) kuonyesha upotevu wa mabilioni ya shilingi yaliyotumika katika nyanja mbalimbali ikiwemo mishahara hewa na mikataba mibovu.
Mbunge wa Longido (CCM), Michael Laizer alisema ni aibu kila mwaka kuwa na ripoti za wizi wa mali za umma lakini Serikali inakaa kimya.
Alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, mmoja wa maofisa wake aliidhinisha Sh11 milioni kwa ajili ya matengenezo ya gari. “Labda Serikali imechoka sasa inafanya makusudi fedha za wananchi zinaliwa lakini yenyewe inakaa kimya. Serikali itujibu hizi fedha zinazopitishwa kila mwaka zinakwenda wapi?” alihoji Laizer
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Magdalena Sakaya alisema Serikali inapaswa kuona aibu kwa kutekeleza pendekezo moja tu kati ya 12 yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Alihoji suala la mishahara hewa kuendelea kujitokeza huku Serikali ikikaa kimya na kila mwaka CAG anatoa ripoti yake… “Kuna vitabu vya halmashauri za wilaya ambavyo CAG hakuvikagua kwa kuwa havikuonekana vilipo, sasa hapo tunakwenda wapi? Kuna Sh8 bilioni hazikufika katika halmashauri husika zimekwenda wapi? Wabunge tunatakiwa kuhoji na kupewa majibu sahihi.”
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alisema sasa Tanzania imekuwa kama Saccos kwa kuwa fedha za umma zinatafunwa bila utaratibu huku vielelezo vikitoweka kusikojulikana.
“Wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, mawaziri walijaa bungeni ila sasa tunajadili hatima ya Watanzania hawaonekani. Wabunge tuwe kitu kimoja tuibane Serikali itueleze hizi fedha zimekwenda wapi?” alisema Nassari.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema chama tawala kisipokuwa makini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kitahukumiwa na vijana.
“Serikali ndiyo chanzo cha fedha kutafunwa… inakuwaje Naibu Waziri wa Maji anasimama na kuahidi mambo mengi wakati anajua wazi kuwa fedha za kutekeleza miradi hazipo?” alihoji.
Alisema mwaka 2015, utakuwa mgumu kwa CCM kwa kuwa wakati huo vijana watakuwa asilimia 85 na wanaweza kukinyima kura kutokana na Serikali yake kushindwa kusimamia masuala ya msingi ya maendeleo.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliwataka wabunge kuacha kulalamika kwa kuwa wao ndiyo wenye rungu la kuishikisha adabu Serikali: “Tukilalamika wananchi waliotuchagua nao watatushangaa kwa kuwa wametutuma kuwawakilisha na si kulalamika.”
Alisema umefikia wakati wa wabunge kuweka itikadi za vyama vyao pembeni na kuwashughulikia mawaziri wa wizara husika ambazo zinaonekana kuwa tatizo.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola alimlipua Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo akisema alihusika katika uuzaji wa mali ya Serikali katika Kiwanja namba 10 Barabara ya Nyerere na kwamba anaingilia utendaji wa mashirika ya Serikali.
Alisema kuwa kiwanja hicho awali, ilikuwa kiuzwe kwa Shirika la Tanzania Motors chini ya Kampuni ya Mashirika Hodhi ya Umma (CHC) kwa Sh1.3 bilioni lakini baadaye Mkurugenzi Mkuu wa CHC alipewa barua kusitisha uuzwaji wa jengo hilo na kumtaka kuitisha mazungumzo upya na Morad Sadik, ambaye alikuwa akitaka kununua eneo hilo awali.
“Inakuwaje wizara inaingia utendaji wa taasisi au kampuni zilizopo chini yake?” alihoji.
Awali, baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu, Wenyeviti wa Kamati hizo za Bunge; Zitto Kabwe (POAC), John Cheyo (PAC) na Augustine Mrema (LAAC), waliwasilisha ripoti za kamati zao zinazoonyesha kukithiri kwa vitendo vya ufisadi serikalini na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kamati ya PAC
Cheyo alisema kamati yake imebaini kuwapo kwa matumizi ambayo hayakupitishwa na Bunge na kutaja Maonyesho ya Sabasaba, Nanenane na Utumishi kama sehemu ambako fedha hizo zilitumika.
Alisema mwaka 2009/2010 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitumia fedha za matumizi ya jumla ya Sh1.10 bilioni kwa ajili ya Maonyesho ya Nanenane ambazo hazikuwamo kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Alisema hata matumizi ya Sh21.63 bilioni zilizotumika kuendesha Mfuko wa Kukwamua Wananchi kiuchumi maarufu kama ‘mabilioni ya JK’ hazikuwapo katika bajeti iliyopitishwa na Bunge. Alipendekeza kuwa ili kuondoa hali hiyo, mfuko huo unatakiwa kuwa na mtu au taasisi ya kuusimamia badala ya kuachwa bila usimamizi.
Alisema kuwepo kwa udanganyifu na ukwepaji kodi kumeisababishia Serikali hasara ya Sh15.4 bilioni na Dola 2.6 milioni za Marekani.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii na ilipoteza Sh874,853,564 baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrabaha kwa mazao ya misitu.
Kuhusu magari ya Serikali, Cheyo alisema kumekuwa na matumizi yasiyo ya lazima katika uendeshaji na ukarabati wa magari hayo. Hadi Juni 30, 2010 Serikali ilikuwa inamiliki magari yenye thamani ya Sh5 trilioni.
Alisema mwendelezo wa ununuzi wa magari unaofanywa na Serikali unaongeza gharama za uendeshaji na kusisitiza kwamba matumizi hayo si ya lazima kwa Serikali yenye uchumi mdogo uliozidiwa na madeni.
Kuhusu ukaguzi wa magari uliofanywa na wakala chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), PAC imependekeza kuwajibishwa kwa ofisa masuuli wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuisababishia Serikali hasara ya Dola 18,343,540 za Marekani ambazo ni karibu Sh30 bilioni na kusisitiza: “Sh30 bilioni zilitumika kufanyia ukaguzi wa magari ambao haukuwepo.”
Alisema pia wamegundua kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kukodi majengo ya wizara na kusisitiza kuwa moja inaweza kulipa kodi ya Sh485 milioni.
Alisema kuna watumishi hewa takriban 3,000 na kwamba Serikali haifahamu lolote kuhusu hali hiyo… “Kuna Sh1.8 bilioni ambazo hutumiwa na Serikali kwa ajili ya kulipa watumishi hewa. Pia imebainika kuwa Serikali haijui thamani ya majengo yake yaliyopo ndani na nje ya nchi.”
POAC
Zitto kwa upande wake, alielezea maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi ya fedha ambayo yanahusisha ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake.
Alitola mfano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo kwa mwaka mmoja wa fedha linafanya ununuzi wenye thamani ya kati ya Sh300 bilioni hadi Sh600 bilioni.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2009/2010, Tanesco ililitumia Sh1.8 bilioni ukilinganisha na Sh65 milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati mojawapo katika Kituo cha Bwawa la Mtera.
“Ongezeko hilo la gharama za ununuzi kwa ajili ya ukarabati, ni kiasi kikubwa na Kamati haikuridhika na majibu ya menejimenti hivyo kuagiza uchunguzi wa ndani ili kubaini uhalisia wa ununuzi huo,”alisema na kuongeza:
“Tumependekeza Tanesco ianze kutumia vyanzo vyake vya umeme na iache kununua umeme hasa wa kampuni ya IPTL kwani inatumia Sh62.4 kununua umeme katika kampuni hii kwa mwaka.”
Alisema Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (MUCE) kilishindwa kuthibitisha kwa wakaguzi wa hesabu uwepo wa vifaa vya maabara vilivyonunuliwa ambavyo vina thamani ya Sh267 millioni.
Katika ripoti hiyo, Zitto alisema imebainika pia mkataba kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), na Kampuni ya Startimes unatakiwa kupitiwa upya ili uinufaishe TBC.
Pia aliugusia matumizi mabaya ya fedha katika Bodi ya Pamba ambako alisema kuwa kiasi cha Sh2 bilioni zilizotolewa na Serikali hazijulikani zilipo na wala hazikuwafikia wakulima wa zao hilo.
LAAC
Kwa upande wake, Mrema aliitaka Serikali ivunje mtandao wa wezi wa mali za umma na kuhoji inakuwaje inawakumbatia mafisadi?
Alihoji majalada ya watuhumiwa wa ufisadi kukaa zaidi ya miaka 10 katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) na ile ya Makosa ya Jinai (DCI) wakati kesi za uchaguzi zimewekewa kikomo.
Alisema ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2010, inaonyesha kuwa Sh583.2 milioni zililipwa kama mishahara hewa kiasi ambacho alisema kingetosha kujenga madarasa 194.
Mrema alisema katika ripoti hiyo, imebainika kwamba Sh8 bilioni zilitumika katika ununuzi usiokuwa na nyaraka na ama wenye nyaraka pungufu hali inayoashiria kuwapo kwa wizi.
Aliwataja watumishi wa Halmashauri ya Kishapu akisema ni vinara wa ubadhirifu wa Sh6 bilioni na kudai kuwa walishirikiana na baadhi ya watumishi wa Benki ya NMB Tawi la Manonga, Shinyanga kuiba fedha hizo za umma.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni Mweka Hazina, Muhdin Mohamed, Mtunza Fedha wa Halmashauri hiyo, Walugu Mussa, Boniface Nkumiming na Mhandisi wa Halmashauri, Leonard Mashamba.
Alisema fedha hizo zilitafunwa kwa kutumia nyaraka feki, uhamisho wa fedha bila idhini na kuzitumia kinyume cha malengo, uhamisho wa fedha ambao haukufika kwenye akaunti husika na malipo kwa walipaji wasiofahamika.
Mrema aliilaumu Serikali kwa kuwahamisha kutoka halmashauri moja kwenda nyingine na Serikali Kuu, watumishi wanaotuhumiwa kwa ufisadi badala ya kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamati hiyo imependekeza Bunge likubali kuitaka Serikali kutoa maelezo ya kuridhisha ni kwa nini ubadhirifu huo umeachwa ukishamiri kwa miaka mitatu mfululizo bila wahusika waliotajwa na CAG kuchukuliwa hatua.
“Shida iliyopo hapa ni Serikali kuonekana inawakumbatia wahusika kwa kisingizio cha uchunguzi unaendelea… nini kinachochunguzwa badala ya kupeleka watu mahakamani na kumuita CAG kama shahidi?”