Serikali ya Saudi Arabia imewakamata vigogo kadhaa wakiwemo wana wa kifalme, mawaziri na wafanyabiashara wakubwa katika kile inachosema ni vita dhidi ya ufisadi vinavyoongozwa na mrithi wa kiti cha ufalme.
Bilionea mkubwa, Al-Waleed bin Talal, ni miongoni mwa wana wa kifalme 11 waliokamatwa usiku wa jana (Jumamosi, 4 Novemba 2017), mara tu baada ya kamisheni mpya ya kupambana na ufisadi inayoongozwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman kutangazwa kwa amri ya kifalme.
Katika tukio jengine, mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Taifa, ambaye aliwahi kuwa mmoja wa waliotazamiwa kurithi kiti cha ufalme, na pia mkuu wa jeshi la pwani na waziri wa uchumi waliondolewa kwenye nafasi zao, ikiwa sehemu ya wimbi la ufutwaji kazi katika Ufalme wa Saudia.
Kituo cha televisheni cha Al Arabiya kinachomilikiwa na Saudi Arabia kiliripoti kwamba wana wa kifalme hao, mawaziri wanne wa sasa serikalini na mawaziri wengine kadhaa wa zamani walikamatwa, huku kamisheni hiyo ikianza uchunguzi juu ya visa vya zamani kama vile mafuriko yaliyoukumba mji wa Jeddah mwaka 2009.
Shirika la habari linalomilikiwa pia na serikali ya Saudia, SPA, lilisema lengo la kamisheni hiyo ni "kulinda fedha za umma, kuwaadhibu mafisadi na wale wanaoutumia vibaya nafasi zao."
Hisa zaporomoka
Hisa kwenye kampuni ya Kingdom Holding, ambazo zinamilikiwa kwa asilimia 95 na Mwanamfalme Al-Waleed, zilishuka kwa asilimia 9.9 wakati maduka ya hisa yalipofunguliwa asubuhi ya Jumapili, kukiwa tayari na taarifa za kukamatwa kwake.
Ofisi yake haikupatikana mara moja kuzungumzia suala hili.
"Kwa msako huu, ufalme unaanza enzi mpya na sera ya uwazi, usafi na uwajibikaji," alisema Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia, Mohammed al-Jadaan, kwa mujibu wa shirika la habari la SPA.
"Maamuzi haya magumu yatalinda mazingira ya uwekezaji na kuinua imani kwenye utawala wa sheria."
Baraza kuu la maulamaa la nchi hiyo liliisifia pia hatua hiyo kuwa ni "muhimu", kauli ambayo inachukuliwa kama baraka za kidini kwa msako huo.
Chanzo kimoja kutoka usafiri wa anga kililiambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya usalama vimezizuwia ndege binafsi kuruka kutoka viwanja vyote vya ndege vya nchi hiyo, yumkini ikikusudiwa kuwazuwia vigogo kukimbia nchi.
Hatua hizi za kushitukiza zinakuja katika wakati ambapo taifa hilo lenye uhafidhina wa kiwango cha juu likianzisha mageuzi makubwa kwenye masuala ya kijamii na kiuchumi, kufuatia kutangazwa kwa Mwanamfalme Mohammed kuwa mrithi rasmi wa nafasi ya baba yake, Mfalme Salman, ambaye alimuondoa kwenye mstari wa urithi binami yake, Mwanamfalme Mohammed bin Nayyaf, aliyemuweka kwenye kizuizi cha ndani tangu mwezi Juni.