Sunday, November 5

Wasaudia wafurahia kukamatwa wanawafalme kwa ajili ya rushwa

Mwanamfalme mrithi wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman akihudhuria mkutano wa uwekezaji mjini Riyadh, Saudi Arabia, Oct. 24, 2017.
Wasaudia wamepokea kwa furaha tanagzo la Jumamosi la kukamatwa kwa wanawafalme 11 mawaziri wanne wa utawala wa hivi sasa na mawaziri kumi wa zamani katika kampeni mpya ya kupambana na ulaji rushwa na ufisadi katika taifa hilo la kifalme.
Tukio hilo ni la kwanza la aina yake kwa wanawafalme, matajiri na watu mashuhuri kukamatwa kwa kosa lolote na inachukuliwa ni sehemu ya mageuzi makubwa yanaoongozwa na mwanamfalme Mohammed bin Salman, na babake Mfalme Salman.
Akizungumza na Sauti ya Amerika mwandishi habari wa Redio ya Saudia Abdullah Muawiya anasema miongoni mwa walokamatwa ni tajiri mwenye ushawishi mkubwa mwana mfalme Miteb bin Abdullah bin Abdulaziz, ambae alikua waziri wa jeshi la ulinzi wa taifa na mtoto mkubwa wa mfalme aliyefariki miaka miwili ilyiopita.
FILE - Mwanamflame Miteb bin Abdul Aziz,kijana wa mfalme wa zamani Abdullah bin Abdul Aziz al-Saud.
FILE - Mwanamflame Miteb bin Abdul Aziz,kijana wa mfalme wa zamani Abdullah bin Abdul Aziz al-Saud.
Tajiri mwengine mashuhuri anaesemekana ndiye bilionea mkuu wa Mashariki ya Kati ni mwanamfalme Alwaleed bin Talal, mwenye makampuni makubwa katika nchi za Ulaya Magharibi na Asia na mwenye mradi wa kutaka kujenga jengo refu kabisa duniani huko Jeddah.
Vyombo vya habari vya serikali havijaeleza lolote kuhusu kukamatwa kwa maafisa hao. Hata hivyo kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Saudi Arabia Al-Arabiya imetangaza kwamba watu hao wanashikiliwa ndani ya hoteli ya fahari ya Ritz Carlton mjini Riyadh.
Mwandishi Muawiya anasema tukio hili linazidisha mvutano wa ndani uliyopo katika familia ya kifalme huko Saudia lakini anasema inachukuliwa kama mbinu ya kuhakikisha mwanamfalme Mohammed bin Saman anachukua uwongozi bila ya matatizo yeyote lakini anasema pia ni hatua ya ujasiri mkubwa kuwakamata watu hao.

No comments:

Post a Comment