Ametoa wito huo leo Novemba 5 wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Amewataka wananchi wa Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” amesisitiza.
“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” amesema.
Amesema uamuzi huo wa Bakwata ulitangazwa kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua kuadhimisha sherehe hizo kwenye ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao makuu kila mwaka.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimekwishapatikana.
“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,” amesema.
Amesema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa na mahubiri ya viongozi wa dini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed Mtopa amesema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa. “Tunakuhakikishia wewe Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa Mufti waliopo hapa kwamba tumepokea hiyo heshima,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki kutoka Bakwata Makao Makuu na Msimamizi wa Malidi za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye amesema wana Ruangwa na wana Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe hizo.
Waziri Mkuu anatembelea vijiji vya jimboni mwake ambako atahutubia wananchi.
No comments:
Post a Comment