Sunday, November 5

UVCCM wadai Uchaguzi 2020 utakuwa mwepesi kwa Rais Magufuli


Tanga. Jumuiya ya vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imesema uchaguzi mkuu  wa mwaka 2020 utakuwa mwepesi kwa CCM kwa kuwa kazi iliyofanywa na Rais John Magufuli  inapendwa na wananchi wengi.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa ,Shaka Hamdu Shaka amesema hayo leo Novemba 5  jijini hapa wakati wa maadhimisho ya tathmini ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
Amesema utendaji kazi uliofanywa na Rais John Magufuli katika kipindi cha miaka miwili haujawahi kufanywa na watangulizi wake wote jambo ambalo linaifanya CCM ijivunie kuwa itashinda kiti cha Urais, majimbo na kata nyingi zilizo chini ya upinzani hivi sasa vitarejeshwa.
“Ndani ya miaka miwili ya utendaji kazi wa Magufuli yametokea mabadiliko makubwa katika sekta ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ambayo yamewezesha wananchi kujenga imani kubwa dhidi yake na huo ndiyo mtaji mkubwa kwa CCM” amesema Shaka.
Amesema  kutokana na utendaji kazi wa Rais Magufuli, viongozi ambao hawakuwa wasafi, wameanza kujiengua wenyewe ndani ya CCM na kwamba hata vyama wanavyokimbilia vina ugomvi wa ndani kwa ndani ambao unafukuta.
“Huko jirani kuna ugomvi mkubwa unafukuta ndani kwa ndani, hata kiongozi aliwahi kuwa Waziri Mkuu kwa miaka miwili anatamani kurejea CCM anashindwa kupata mlango wa kuingilia” amesema Shaka katika mkutano huo ulioandaliwa na UVCCM Wilaya ya Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa katika taarifa yake ya tathmini ya utendaji kazi wa Rais Magufuli kwa kipindi cha miaka miwili amesema amewezesha kujengwa kwa bomba la mafuta na kiwanda kikubwa kwa nchi za Afrika Mashariki  cha saruji  ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

“Agosti 5 mwaka huu Tanga iliandika historia ya viwanda kwa kupokea Marais John Magufuli na Yoweri Museveni waliozindua ujenzi wa bomba la mafuta, lakini Rais wetu atakuja tena hivi karibuni kuzindua ujenzi wa kiwanda kikubwa kwa nchi za Afrika Mashariki cha saruji”amesema  Mwilapwa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Allan Kingazi amesema uchaguzi wa chama hicho na jumuiya zake katika ngazi za kuanzia mashina hadi Wilaya tisa zilizopo umekamilika huku kukiwa na rufaa tatu za kuonyesha kutokubaliana.
Amesema rufaa hizo ni chache na zinaashiria kwamba chaguzi hizo ziliendeshwa kwa kufuatwa taratibu jambo linaloashiria kuwa hata uchaguzi wa ngazi ya mkoa utakufanyika kwa amani.

No comments:

Post a Comment