Sunday, November 5

Kamati Kuu ACT-Wazalendo kutuma wawakilishi polisi


Chama cha ACT-Wazalendo kimesema Kamati Kuu ya chama hicho haitakwenda kuripoti polisi kama ilivyoagizwa bali itawakilishwa na mwenyekiti na kiongozi wa chama hicho.
Novemba 2,2017 chama hicho kimesema kilipokea wito kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ukiwataka wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT -Wazalendo kesho Novemba 6,2017 wafike Kituo cha Makosa ya Fedha kilichopo Kamata, Kariakoo wilayani Ilala.
Alipopigiwa simu, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa kueleza kama anafahamu kuhusu wito huo, alitaka apigiwe simu DCI, Robert Boaz ambaye hakupatikana.
Wito huo ulitolewa siku tatu baada ya Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kuhojiwa Oktoba 31,2017 kuhusu masuala ya uchumi na takwimu.
Akizungumza leo Jumapili Novemba 5,2017 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja amesema kamati kuu ina wajumbe wengi walio kwenye mikoa tofauti.
"Ni vigumu kuwakusanya wajumbe wote na kuwapeleka polisi, hivyo tutawawakilisha mimi na Kiongozi wa chama (Zitto Kabwe)," amesema.
Maganja amehoji iweje kamati kuu iitwe kwenda kuhojiwa polisi. Amesema kamati kuu ni chombo cha kitaifa ambacho hakiwezi kwenda polisi kikiwa na wajumbe wote bali wawakilishi.
Amesema Kamati Kuu ni chombo cha kitaifa cha chama chenye mamlaka ya kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, hivyo polisi haina madaraka ya kushughulikia wala kuingilia uamuzi halali wa chombo hicho.
Akizungumzia hilo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Ado Shaibu amesema polisi watafute muda sahihi wa kuwahoji viongozi wa chama hicho lakini si kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Novemba 26,2017 katika kata 43 nchini.
“Tulitakiwa kuelekeza nguvu zetu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo badala ya mahojiano na polisi,” amesema.

No comments:

Post a Comment