Sunday, November 5

Mali yenye thamani Sh 81.98 milion yakamatwa Namanga


 Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA), kituo cha forodha Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wamekamata mali zenye thamani Sh 81.98  milioni, zilizokuwa zinaingizwa nchini kwa njia za magendo zikiwepo simu za mkononi 1155.
Kuanzia Januari hadi  Septemba bidhaa zilizokamatwa  zilikua na thamani ya sh 132.2 milioni, ambapo baada ya kutozwa  kodi zimepatikana kiasi cha Sh milioni 56.8 milioni
Iwato amesema ,  kodi ambazo Serikali itapata kwa simu hizo ni Sh  40.03 milioni, endapo mmiliki wake atazikomboa kabla ya siku 21 lakini zikikaa zaidi ya siku hizo gharama zitaongezeka pia na baada ya siku 90 zitapigwa mnada.
Meneja msaidizi wa  TRA Namanga, Edwin Iwato amesema  pamoja na simu hizo bidhaa nyingine walizokamata ni pamoja na katoni za vipodozi, dawa za binadamu na mifugo, maziwa ya paketi pamoja na mafuta ya kupikia.
Meneja huyo amesema,  katika operesheni iliyofanyika Octoba pekee pia wamekamata magari 10 yaliyohusika kusafirisha bidhaa hizo na kufanikiwa kuokoa kiasi Sh 43.3 milioni, ambazo wafanyabiashara hao walikua wakikwepa kuzilipa na kuamua kupitisha bidhaa zao kwa njia za magendo.
Akizungumzia operesheni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Longido Daniel Chongolo ametoa onyo kwa wafanyabiashara kuacha kutumia njia za panya kukwepa kodi kwani kutokana na udhibiti uliopo hivi sasa wataendelea kupata hasara kwa mizigo yao kukamatwa.
‘’Natambua wafanyabiashara wengi wanakopa fedha ili kuboresha biashara zao lakini kama  wanataka kupiga hatua wasifanye biashara za magendo ambazo zitawafilisi na kuwafanya wateseke kulipa mikopo yao kwani hivi sasa udhibiti katika mpaka huo wa Namanga ni mkubwa’’ amesema 
Mkaguzi wa Mamlaka ya chakula na dawa(TFDA) katika mpaka wa Namanga, Elia Nyaura amesema miongoni mwa bidhaa zilizokamatwa hazijasajiliwa hapa nchini na nyingine hata hazifahamiki ni bidhaa za aina gani na zimetengenezwa wapi hivyo kushindwa hata kuthibitisha ubora wake.
Amesema kwa bidhaa hizo ambazo zimekiuka hata taratibu za awali za kuingiza hapa nchini hawawajibiki hata kuzipeleka kwa mkemia kuzipima na kutoa wito kwa wafanya biashara kuwa makini na kufuata taratibu pindi wanapotaka kuagiza bidhaa kutoka nje.
Mpaka wa Namanga ni miongoni mwa mipaka ambayo inatumiwa na wafanyabiashara wengi kuingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi bidhaa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment