Thursday, September 9

KESI YA MBOWE KUENDELEA KUUNGURUMA KESHO

 


KESI ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu itaendelea kusilizwa  kesho Septemba 10, 2021 mbele ya Jaji Mustapha Siyani baada ya kupangiwa Jaji huyo mpya kufuatia kujitoa kwa Jaji Elinazer  Luvanda aliyekuwa akiisikiliza mwanzo.

Leo Septemba 9,2021 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Magdalena Ntanda kesi amesema, kesi itaanza kuanzia saa 3 asubuhi na kwamba muda kamili utategemea magereza watawapeleka washitakiwa hao saa ngapi.

Awali, kesi hiyo ilipaswa kuanza kwa kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi lakini upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala ulipinga hatua hiyo kwa kuwasilisha mapingamizi yenye hoja nne kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba hati ya mashitaka ni batili na kuomba mahakama iwaondolee washitakiwa mashtaka hayo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga hoja hizo ukidai mahakama hiyo inayo mamlaka na hati ya mashtaka iko sahihi.

Kutokana na hali hiyo Jaji Elinazer Luvanda alitupilia mbali mapingamizi yote lakini kesi hiyo haikuweza kuendelea baada ya Mbowe kudai hana imani na jaji huyo katika kutenda haki na kumuomba ajitoe.

Katika Maelezo ya Mbowe ya kwa niniJaji ajitoe Katika  shauri Hilo  ametoa madai Mbalimbali ikiwa Ni Pamoja na  kutupilia Mbali kila Mapingamizi yanayowasilishwa na Upande wa Utetezi.

 Pia  amedai Kuwa  Mapingamizi yanayowasilishwa na upande wa Utetezi  hayazingatiwi na kwamba hata vifungu vya sheria wanavyotumia kama mfano kwenye kutetea mapingamizi yao havizingatiwi wakati wa kutoa  uamuzi  wake  jambo ambalo anadaia ni ukiukwaji wa haki za Msingi.

Mbowe alidai "Mheshimiwa Jaji naomba kunukuu taarifa....Jaji Elinaza Luvanda ni Mserikali na Tiss, yupo Mahakama ya Mafisadi kimkakati, anaelekezwa kumfunga Mbowe huku msajili akishughulika na Chadema, Rais atamuachia baada ya muda kila pingamizi atalitupilia mbali, haijalishi uhalali wake.'' mwisho wa kunukuu..." 

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni   Halfan  Hassan, Adamu  Kasekwa, Mohamed Abdillahi Ling'wenya ambao wanakabiliwa na mashitaka sita katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.

Mbowe anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili fedha kwa ajili vitendo vya kigaidi.

Inadaiwa washitakiwa kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Mei Mosi, 2020 na Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, walitenda kosa hilo.

Washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa walikula njama za kulipua vituo mbalimbali vya mafuta na katika mikutano isiyokuwa ya kisiasa na kusababisha hofu kwa wananchi kwa lengo la kuutishia umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mashitaka ya pili yanayomkabili  Mbowe inadaiwa katika tarehe hizo, katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, Mbowe aliwafadhili Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya, huku akiwa na lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo ya mafuta na mikusanyiko ya wananchi.

No comments:

Post a Comment