LIKIZO isiyo ya lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi kwenye Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kwa sababu ya ugonjwa COVID 19 ilisababisha wasichana 50 wasiendelee na masomo yao kutokana na kufungwa shule kwa takribani miezi mitatu mwaka jana.
Inaelezwa kuwa wanafunzi hao walishindwa kurudi masomoni kutokana na kuolewa au kupata ujauzito kutokana na baadhi ya wazee wa jamii ya kifugaji kutumia fursa hiyo ya likizo na kuwaoza mabinti hao.
Wanafunzi 50 wa shule ya msingi Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliacha shule kwa kuolewa wakiwa wadogo au kupata ujauzito kutokana na kuwa majumbani mwao kipindi cha likizo ya takribani miezi mitatu ya Covid 19.
Ofisa elimu wa shule za msingi Wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema likizo hiyo iliyotokana na Covid 19 ilisababisha wanafunzi hao kuacha masomo yao na hawakurudi shuleni baada ya shule kufunguliwa.
Tairo amesema shule zilifungwa kutokana na Covid 19 Machi 17 mwaka 2020 na kufunguliwa Juni 29 mwaka 2020 na wakabaini baadhi ya wanafunzi hawakurudi masomoni.
Mmoja kati ya viongozi wa kimila wa (Laigwanani) Yohana Ole Tiamongoi amesema, viongozi wa kimila wa eneo hilo wamekuwa wakikubaliana kwenye vikao vyao kila mara kuwa suala la watoto wa jamii ya kifugaji kupatiwa elimu liwe ni kipaumbele.
“Jamii yetu imekuwa na mwamko wa kuwapatia elimu watoto wote wakifugaji wakiume na wakike japokuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wenzetu wanamtazamo hasi kwa mtoto wa kike kuwa bado ni wakuolewa na siyo kupata elimu,” amesema Ole Tiamongoi.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Arusha Mashariki, Usharika wa Purana, Enock Paulo amesema hivi sasa jamii ya kifugaji imebadilika kwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.
Mchungaji Paulo amesema jamii ya kifugaji inawasomesha watoto wakiume na watoto wakike wasidhani ni wakuolewa pekee kama walivyokuwa wana dhana potofu miaka iliyopita.
Amesema watoto wa kike wana msaada mkubwa kwa jamii ya kifugaji na anapaswa kuolewa akifikisha umri wa miaka 18 kwa asilimia kubwa wengi wameelimika kwenye suala la kusomesha watoto wao.
“Jamii ina kazi kubwa kuwapeleka shule watoto wao hasa wa kike kwani wanakuwa na uwezo mkubwa wa kusababisha mabadiliko kwenye familia na hata taifa kwa ujumla,” amesema mchungaji Paulo.
Amesema hivi sasa jamii ya kifugaji imekuwa na mwamko mkubwa wa kusomesha watoto wao ili kuhakikisha wanakuwa na chachu ya maendeleo kwa miaka inayokuja.
Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni anasema kwenye kijiji chake hakukuwa na mwanafunzi hata mmoja ambaye aliacha masomo kipindi cha likizo ya Covid 19 mwaka jana kwani wazazi na walezi, walishaelezwa kuwa wanafunzi wanapaswa kupatiwa elimu na siyo kuozeshwa wakiwa wadogo.
"Kwa kweli jamii ya kifugaji ya kimasai kwa upande wa Naisinyai imebadilika kwenye mtazamo wa kusomesha watoto hasa wakike kwani tunaona faida kubwa ya elimu hivi sasa" amesema Makeseni.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera, hivi karibuni alikutana na wakuu wa idara ya elimu na kuwaagiza kuandaa na kuweka mpango mkakati wa kupunguza na kukabiliana na tatizo la utoro na mimba za utotoni kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Dkt Serera amesema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakikatisha masomo yao kutokana na kupata ujauzito na wengi kushindwa kuhudhuria masomo baada ya kubebeshwa mimba bado wakiwa wanasoma.
"Wakuu wa idara za elimu mnapaswa kuweka mpango mkakati ambao utatekelezeka ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari," amesema Dkt Serera.
Ametoa rai kwa wataalamu hao wa idara ya elimu, kuwashirikisha wazawa waliopata fursa ya kupata elimu, kushawishi wazazi na walezi wa eneo hilo, kuwapeleka watoto wao shule.
Pia, amewaagiza wahahakikishe wanafunzi wanahudhuria masomo kwa vipindi vyote vya muhula wa masomo na kuimarisha mfumo wa elimu kwa watu wazima (MEMKWA).
No comments:
Post a Comment