Dar es Salaam. Serikali imesema ni wakati mwafaka mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) kutumia mfumo wa taa zilizopo katika barabara zake badala ya kuongozwa na askari wa barabarani.
Hatua hiyo hiyo itasasidia mabasi hayo kufika kituoni kwa wakati kuliko hivi sasa yanachelewa njia kutokana na kuongozwa na askari wa barabarani.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi wa mabasi hayo kuanzia eneo la Morocco hadi Kivukoni.
Kutokana na hatua hiyo, Jafo amewagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Mhandisi Ronald Lwakatare kuwasiliana na uongozi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuangalia uwezekano wa polisi kuacha kuyaongoza magari hayo.
Amesema taa za kuongozea magari zilizopo kwenye mfumo wa barabara za mabasi hayo ziachwe zifanye kazi ya kuongezea magari badala ya askari.
“Kuna umuhimu mkubwa wa mabasi haya yakatumia taa za barabarani kuliko kuongozwa na askari ili yaweze kukidhi mahitaji na malengo yaliyokusudiwa,’’ amesema Jafo.
Kuhusu mabasi ya ‘Express’ yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya kutoa huduma ya moja kwa moja kutoka kituo kikuu cha Kivukoni hadi Kimara na kutochukua abiria pindi yanaposhusha yanaposhusha wasafiri Kivukoni, hatua hiyo imekuwa kero kwa wanaotumia usafari huo hasa wanaotaka kwenda Kimara.
“Unaweza kukuta mabasi yanashusha abiria Kivukoni na kuna kundi la abiria wanaohitaji kwenda moja kwa moja Kimara, lakini hayachukui abiria, jambo hili linapaswa kurekebishwa kwani linasababisha kero kwa abiria,” amesema
Mbali na hilo, amewataka madereva wa bodaboda kutokukatisha katika barabara za mfumo na mabasi hayo na kwamba kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wao na abiria wanaotumia mfumo wa mabasi.
No comments:
Post a Comment