China imepongeza itikadi ya kisiasa ya Rais Xi Jinping iliyozinduliwa jana katika mkutano mkuu wa chama cha Kikomunisti ishara kwamba huenda ikaingizwa katika katiba ya chama hicho na kuimarisha nguvu za kiongozi huyo.
Maafisa wa chama tawala cha Kikomunisti nchini China walishangilia kwa kuimba na kucheza huku wengine wakibubujikwa na machozi wakati wakipongeza itikadi hizo, siku moja baada ya kuufungua mkutano ambao unafanyika kila baada ya miaka mitano na kuahidi kujenga ''mafanikio ya kisasa ya kijamaa'' kwa ajili ya ''zama mpya''.
Kwa mujibu wa shirika la habari la China, Xinhua, wajumbe watatu wanaomaliza muda wao katika kamati kuu ya watu saba ambayo Xi anaiongoza, wamesema wanayaheshimu mawazo ya kiongozi huyo kuhusu ujamaa na China mpya. Wachambuzi wanasema kauli kama hizo zinaonyesha Xi ataimarishia nguvu katika madaraka yake kwa kutumia kaulimbiu yake mpya na kuingizwa katika katiba ya chama.
Hakuna kiongozi mwingine ambaye itikadi yake iliingizwa katika katiba wakati akiwa mdarakani, tangu utawala wa Mao Zedong, mwanzilishi wa China ya sasa. Huenda wiki ijayo Xi akachaguliwa tena kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano mingine ijayo.
Maafisa wa chama hicho wamempongeza Xi kama kiongozi mwenye hekima na busara, heshima ambayo walipewa viongozi wawili tu, akiwemo Mao Zedong na mrithi wake Hua Guofeng.
Gazeti la kila siku la Beijing limeripoti kuwa Katibu Mkuu wa chama cha Kikomunisti mjini Beijing, Cai Qi, anasema Xi amepewa mapenzi na heshima ndani ya chama hicho, jeshi na watu wote kwa ujumla na anastahili kuitwa kiongozi mwenye hekima. Qi ni mmoja wa washirika wa karibu wa Xi.
Wachambuzi wanasema, kitendo cha maafisa kumsifu na kumpongeza kiongozi wa juu wa chama katika mkutano mkuu sio cha ajabu, lakini kitendo cha kuonyesha hisia au mapenzi binafsi sio kitu cha kawaida.
Xi amekiimarisha chama
Xi mwenye umri wa miaka 64 amekiimarisha chama hicho tangu alipochukua madaraka mwaka 2012, na kuziba mianya yote ya rushwa, kudhibiti vikali mashirika ya kiraia na kuipandisha nafasi ya China katika ngazi ya kimataifa.
Itikadi iliyopewa jina la Xi kuiongoza China na chama, itaongeza mamlaka yake, anasema Ryan Manuel, mtaalamu wa masuala ya siasa za China katika Chuo Kikuu cha Hong Kong. Watangulizi wa Xi, Hu Jintao na Jiang Zemin, walikuwa na dhana zao za itikadi ambazo zilitajwa katika katiba, lakini sio majina yao.
Mwaka uliopita, chama hicho kilimpa Xi cheo cha ''Kiongozi Imara'', hali iliyomuimarishia nafasi yake kabla ya mkutano huo mkuu. Na kulingana na uvumi, Xi anaweza kubakia madarakani zaidi ya muda wa kawaida wa vipindi viwili na hata kukumbushia cheo cha mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Mao Zedong.
No comments:
Post a Comment