Wednesday, August 16

Wananchi waandamana kudai ‘chao’ mgodi wa Acacia





Picha na Maktaba
Picha na Maktaba 
Wananchi wanaoudai mgodi wa Acacia North Mara fidia ya maeneo yao kwa kukaa muda mrefu bila kuwalipa, wameandamana kwenda mgodini kushinikiza malipo yao.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema maandamano hayo yanafanyika mara kwa mara kutokana na baadhi ya  majina kuondolewa kwenye orodha ya waliohakikiwa.
Kamanda Mwaibambe amesema kuwa majina ya watu hao yaliondolewa kwenye orodha hiyo na mgodi huo baada ya kukutwa yameongezeka wakati wa kuwasilishwa mgodi hapo kwa malipo yaliyotakiwa kutolewa na kufanya shughuli ya ufidiaji kukwama.
Hata hivyo, kundi hilo la wananchi limetawanywa na polisi waliokuwa na gari la maji ya kuwasha ambalo limesimama kwenye lango mkuu la kuingia mgodi .
"Nina taarifa ya kuwepo kwa maandamano hayo siku za nyuma, lakini kwa siku ya Leo sina hiyo taarifa labda nifuatilie utanicheki baadaye," amesema Kamanda Mwaibambe.
Ameongeza kuwa baada ya mgodi huo kubaina kuwepo kwa ongezeko la idadi ya wanaodai wafidiwe maeneo yao, waliandika barua kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga ili kulishughukikia.
"Mkuu wa wilaya ndiye anayeweza kulisemea hilo vizuri maana nijuaavyo mimi alikabidhiwa orodha hiyo kwa ajili ya kuishughulikia," amesema.
Hata hivyo, simu ya mkononi ya Mkuu wa Wilaya, Luoga ilipopigwa kujua hatua iliyofikiwa kwa wananchi hao kupata haki yao, haikuwa hewani.
Hivi karibuni kundi la wananchi lilivamia kwa siku mbili mfululizo mgodi huo likitaka kuokota mawe ya dhahabu ambapo watu zaidi ya 60 walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uvamizi na hadi sasa wapo rumande.

No comments:

Post a Comment