Wednesday, August 16

Mashirika yasiyo ya kiserikali kusomesha elimu ya juu


Zaidi ya wanafunzi 50,000 ambao wamekosa ufadhili wa masomo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya ufadhili wawapo vyuoni, watanufaika na mikopo  kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Mkopo huo utalipwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Social Support Foundation (TSSF) kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kifaida la kimaitaifa la Cosmopolitan Development Foundation (CDF International) .
Kwa pamoja, mashirika hayo yamezindua mpango kabambe wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini ambao wanatokea katika mazingira duni.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TSSF, Donati Salla imeeleza kwamba mpango huo utatumia zaidi ya Dola1 milioni za Marekani na kutoa fursa kwa zaidi ya wanafunzi 50,000 ambao watanufaika kuanzia mwaka huu.
Mpango huo ambao ni mpya na pekee kwa hapa nchini na una utaratibu ambao unaelekeana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa ELimu ya Juu (HELSB) umelenga kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao wana uhitaji hasa wale ambao wamekosa ufadhili wa masomo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Akibainisha malengo ya mpango huo, Salla alisema  mpango huo utafungua madawati ya huduma kwa wanafunzi hao katika taasisi ambazo zinatoa elimu ya juu ambapo kwa mwaka huu taasisi za elimu ya juu 98 ndizo zilizoidhinishwa kutoa elimu hiyo kwa ngazi ya shahada.
Pia, alieleza kwamba wanufaika wa mpango huo watakuwa ni wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma kwenye taasisi za elimu ya juu zilizopo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zaidi ya wanafunzi 59,378 wa elimu ya juu hukosa mikopo kutoka serikalini kila mwaka, jambo ambalo limesababisha mpango huo uanzishwe ili kuwapa fursa.
Katika kuhakikisha kwamba malengo yanatekelezwa kikamilifu, mashirika hayo mawili yameanzisha mfuko wa elimu ya juu unaoitwa Tanzania Social Support Foundation ambao utajikita kutelekeza malengo ya mpango huo.
Salla aliwaomba wanafunzi, taasisi na wadau wote wa elimu ya juu kushirikiana pamoja ili malengo ya mpango huo yaweze kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment