Wednesday, August 16

Kairuki wa Kenya ashtakiwa kwa udanganyifu wa mamilioni

Mkurugenzi wa Kampuni ya Candy& Candy, Josiah Kiman Kairuki (38), Mkazi wa Mikocheni Jijini Dar es Salaam juzi alipandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Longido mkoani Arusha, kujibu tuhuma za kujipatia Sh336 milioni   kwa njia ya udanganyifu.
Kairuki anatuhumiwa kujipatia fedha hizo baada ya kudai  kuwa ana kontena  la simu za I- Phone 7 ambalo limezuiwa katika bandari ya Dar es Salaam.
Kairuki ambaye ni raia wa Kenya, Julai 26 mwaka huu  mahakama hiyo ilimwachia huru katika shtaka hilo la kujipatia fedha hizo kwa njia ya  udanganyifu, kutoka kwa  Yusuph Mohamed  kutokana na maombi ya Jamhuri yaliyowasilishwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa polisi Anastazia  Mutatina.
Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aziza Temu alikamatwa na polisi akiwa nje ya mlango wa mahakamani na kurejeshwa kituo cha polisi cha wilaya ya Longido kwa mahojiano zaidi.
Juzi, mkurugenzi huyo aliunganishwa na Abdinasiri Adamnuru na mbele wa Hakimu Mfawidhi wa wilaya, Aziza Temu na walisomewa mashtaka mawili ya kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu na kosa la pili lilimhusu Adamnuru kujifanya ofisa forodha kutoka Tanzania.
Mwendesha Mashtaka Mkaguzi wa Polisi, Anastazia Mutatina alisema watuhumiwa hao walifanya makosa hayo  kati ya Januari 23 na Juni 10, 2017 na upelelezi wa shtaka hilo bado haujakamilika.
Hata hivyo, aliomba watuhumiwa hao wasipewe dhamana kutokana na kiasi kikubwa cha fedha wanachotuhumiwa na pia wote kutokuwa na makazi wa kudumu hapa nchini.
Hakimu alikubali maombi ya upande wa mashtaka na watuhumiwa hao walirejeshwa katika mahabusu ya Kisongo mjini Arusha hadi Agosti 23 kesi yao itakapotajwa tena. 

No comments:

Post a Comment