Thursday, July 27

Profesa Mwaghembe akiri kuendelea kwa ujangili nchini


Tanga. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema licha ya vita kubwa ya kupambana na ujangili nchini, bado unaendelea.
Akizungumza leo Alhamisi, Julai 27 katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari nchini Profesa Maghembe amesema wiki tatu zilizopita aliona mizoga mitatu ya tembo katika Rifadhi ya Taifa ya Ruaha.
“Lakini majangili wengi waliokamatwa, kesi zao zimeisha na wamehukumiwa vifungo jela. Tunavishukuru vyombo vya habari kwa kushiriki vita hii, kwani imefanikisha kulipunguza kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Akizungumzia suala la kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Maghembe amesema sheria iko wazi inakataza, lakini watu wanaikaidi kwa makusudi.
“Hatari ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi ni kubwa kwa sababu wanyamapori huambukizwa magonjwa mengi. Kama kukiwa na mlipuko wa magonjwa kama ya bonde la ufa, ni hatari kwa mifugo kama ng'ombe kuambukizwa kirahisi na hii inaweza kuwaathiri hata binadamu licha ya watu kuliona kuwa ni jambo dogo,” amesema.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuielimisha jamii juu ya hilo, ingawa wafugaji huvutiwa na mzingira ya hifadhi wakidhani kuwa wamepata malisho, lakini akasema ni hatari kwa jamii na mifugo yao.
Amesema yapo magonjwa mengi kama ya homa za vipindi ambazo husababisha wanyama kuharibu mimba.

No comments:

Post a Comment