Msanii mkongwe wa muziki wa asili nchini Tanzania, Mrisho Mpoto baada ya kufanya vizuri na wimbo ‘Sizonje’ ambao ulipendwa na watu wa rika zote ndani ya nchi na kimataifa, hatimaye Jumatatu hii (tarehe 1 August 2017) anatarajia kuachia wimbo wake mpya ‘Kitendawili’ akiwa amemshirikisha mkali wa nyimbo za mahaba, Kassim Mganga.
Wimbo uliopita ‘Sizonje’ wa muimbaji huyo uliacha maswali mengi kwa wapenzi wa muziki wake kutokana namna maishiri ya wimbo huo yalivyokuwa magumu huku wengi wakidai huwenda wimbo huo alimuimbia Rais John Pombe Magufuli kitu ambacho hakuwahi kukiweka wazi licha ya Rais huyo kutamka mara kadhaa katika mikutano yake kwamba wimbo huo alikuwa kwaajili yake.
Sasa mshairi huyo ametangaza ujio wake mpya na wimbo ‘Kitendawili’ akiwa Kassim Mganga ikiwa ni wimbo wa kwanza ambao unawakutanisha wawili hao ambao kila mmoja ni mkali kwa upande wake.
Mpoto amesema amerekodi wimbo wake huo mpya katika studio za Combination Sound chini ya producer mahiri, Man Walter ili kupata ladha tofauti ya muziki wake.
“Mimi naamini muziki ni ladha, nyimbo zangu nyingi nimefanya ndani ya studio yangu chini ya producer Alan Mapigo na zilifanya vizuri. Lakini katika project hii mpya nikaona sio mbaya kama nikibadili dhala ya beat na kupata kitu tofauti na kweli Man Walter amefanya kitu kizuri sana, menejimenti pamoja na watu wangu wa karibu wamefurahishwa na kile ambacho amefanya ,” alisema Mpoto.
Aliongeza, “Pia katika wimbo huu utamsikia Kassim Mganga, huyo ni mtu mpya kabisa katika nyimbo zangu, amefanya kitu kikubwa sana ambacho bila shaka kitawashangaza mashabiki wengi wa muziki. Kwahiyo napenda kuwaambia mashabiki wakae mkao wa kula, Mpoto nimerudi upya na kazi ni nzuri.”
Mjomba amewataka mashabiki wake wa muziki kuusubiria kwa hamu wimbo huo ambao utaachiwa siku ya Jumatatu (tarehe 1 mwezi August) kupitia mitandao ya kijamii (blogs) pamoja na redio.
Pia mshairi huyo amesema siku hiyo ataachia kwanza audio na baada ya siku kadhaa atatoka video ambayo amedai ndani yake kuna mambo mengi mapya ambayo hayajazoeleka kwenye muziki wake.
Kwa upande wa muimbaji Kassim Mganga ambaye ameshiriki ndani project ya namna hiyo kwa mara ya kwanza na Mrisho Mpoto, amesema amefurahishwa na namna wimbo huo ulivyoandaliwa huku akiwataka mashabiki kusubiria muziki mzuri.
“Kusema kweli hii ni mara yangu ya kwanza kufanya kazi ya namna hii na Mrisho Mpoto ambaye hata mimi ni shabiki wa muziki wake. Nimefurahishwa sana na kile tulichokifanya, binafsi nafarijika kuona ushirikiano wetu jinsi ulivyozalisha kitu kikubwa katika muziki, natamani ngoma itoke hata kesho ili mashabiki waone kitu ambacho nakizungumzia. Kwahiyo mashabiki wa muziki kwa umoja wetu tusubirie muziki mzuri ambao utateka fikra na kutoa burudani kwa mashakibiki,” alisema Kassim Mganga.
No comments:
Post a Comment