Friday, November 3

Lungu awaonya majaji Zambia wasiige majaji wa Kenya

Edgar LunguHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais Edgar Lungu
Rais wa Zambia Edgar Lungu amewatahadharisha majaji nchini humo kwamba kutazuka vurugu nchini humo iwapo watathubutu kumzuia kuwania katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021.
Amesema hawafai "kuwaiga" majaji wa Kenya ambao walitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti ambapo Rais Kenyatta alikuwa ametangazwa kuwa mshindi.
Bw Kenyatta Jumatatu alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Alhamisi wiki iliyopita baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kususia.
Kumezuka mjadala kuhusu iwapo Lungu anafaa kuwania au la, huku wakosoaji wake wakisema kwamba anahudumu muhula wa pili na hivyo hawezi kuwania tena.
Wanasema kipindi ambacho alihudumu baada ya kifo cha Rais Michael Sata mwaka 2014 kinafaa kuhesabiwa kama muhula wa kwanza.
Wafuasi wa Lungu wanasisitiza kwamba alimaliza tu muhula wa mtangulizi wake na kwamba muhula wake wa wkanza ulianza aliposhinda uchaguzi wa 2016, ambao ulikumbwa na utata.
Rais anaruhusiwa kuhudumu kwa mihula miwili pekee kwa mujibu wa katiba nchini humo.
Akiwahutubia wafuasi wake kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Bw Lungu amesema:
"Kwa wenzangu katika idara ya mahakama, ujumbe wangu kweni ni kwamba mfanye kazi yenu, mfasiri sheria bila woga au kupendelea upande wowote na mzingatie maslahi ya nchi. Msiwe watu wa kuiga na mfikirie kwamba mtakuwa mashujaa iwapo mtatumbukiza nchi hii kwenye vurugu.
Ningependa kumalizika kwa kusema kwamba wale watu ambao hawapendi amani na uhuru watasema kwamba Rais Lungu anatoa vitisho kwa mahakama za kisheria. Mimi sitoi vitisho kwa mahakama. Ninawatahadharisha tu kwa sababu nina habari kwamba baadhi yenu huenda mkapenda kujaribu mambo. Majaribio hayo yenu yasituingize kwenye fujo, tafadhali.
Watu wanasema kwamba mahakama za Zambia zinafaa kufuata mfano wa mahakama za Kenya...Watu wanasema mahakama za Zambia zinafaa kwua na ujasiri na kufanya maamuzi ambayo yanazingatia maslahi ya raia, lakini hebu tazameni yanayotokea Kenya sasa.
Mimi ninasema mahakama za Zambia zinafaa kutazama yanayotokea. Hazifai kuchukua hatua kana kwamba majaji hao si sehemu ya bara letu la Afrika. Jambo muhimu zaidi ninaweza kusema sasa ni kwamba, 2021, nipo na nitawania iwapo chama changu kitanichagua."
Mahakama ya Juu nchini Kenya ilisifiwa sana kwa kufanya uamuzi wa 'kijasiri' kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
Jaji wa makama ya juu David Maraga na wenzake watatu wameweka historia kwa kubatilisha uchaguzi wa urais wa mwezi AgostiHaki miliki ya pichaEPA
Image captionJaji wa Makama ya Juu Kenya David Maraga na wenzake watatu waliweka historia kwa kubatilisha uchaguzi wa urais wa mwezi Agosti
Majaji wanne wa mahakama hiyo waliunga mkono uamuzi huo ingawa wawili waliupinga.
Siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio hata hivyo, mahakama hiyo ya juu ilishindwa kusikiliza kesi ambayo ilihusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya kukosekana kwa majaji wa kutosha mahakamani.
Ni Jaji Mkuu David Maraga na Jaji Isaac Lenaola pekee waliofika kortini.
Kikao cha mahakama hiyo huhitajika kuwa na angalau majaji watano kwa mujibu wa Katiba.

No comments:

Post a Comment