Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi alisema uamuzi wa kuagiza kuahirishwa kwa uzinduzi huo ulichukuliwa na mkuu wa mkoa, Ezekiel Kyunga ili kutoa fursa ya kusikiliza hoja na malalamiko kutoka GGM baada ya kubainika kuwa sehemu ya maudhui ya filamu inaigusa kampuni hiyo kwa taswira hasi.
Wambura alifika Geita mchana wa Julai 27 tayari kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo iliyochezwa na wasanii wa mkoani hapa wakiwamo Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Leonard Bugomola ambao ulipangwa kufanyika saa moja usiku katika ukumbi wa Desire Park.
Filamu hiyo inaelezea maisha ya wachimbaji wadogo wanavyotegemea magwangala.
“Nilifika kwa mkuu wa mkoa kama mwenyeji wangu ndipo nikapata taarifa kuwa GGM wamelalamikia picha (filamu) kuwa si nzuri kwao. Tulikaa kujadili lakini hatukufikia mwafaka ndiyo maana leo (juzi) asubuhi nimeamka kuingia kwenye kikao kati ya mkuu wa wilaya, wasanii na mwakilishi wa GGM,” alisema.
Katika mazungumzo hayo, naibu waziri alisema GGM walitishia kwenda mahakamani. Hata hivyo, hakufafanua zaidi huku akisema amegundua kwamba kuna tatizo kubwa kati ya ofisa utamaduni na bodi ya filamu; ofisa utamaduni na mkuu wa mkoa; na pia ofisa utamaduni na wasanii.
“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana niliacha kuizindua ili tumalize kwanza haya mambo na wananchi wasiwe na wasiwasi tutakuja tena kwa ajili ya kuizindua,” alisema naibu waziri.
Lakini Kanyasu alipinga hatua hiyo ya kuzuiwa kwa uzinduzi huo akisema waliolalamika hawakufanya hivyo kwa maandishi na hakuna eneo wanaloonyesha kuwa linawahusu. Alisema inasikitisha Serikali ya mkoa kusikiliza maneno ya mdomo na kuzuia uzinduzi wa filamu hiyo.
Mbali ya mbunge huyo, wasanii waliocheza filamu hiyo, Rose Michael na Michael Kapaya nao walieleza kushangazwa kwao na uamuzi wa Serikali ya mkoa kumzuia naibu waziri kuizindua kwa kuwa waliipeleka kwa ofisa utamaduni miezi miwili iliyopita na hawakuelezwa kama ina kasoro yoyote.
“Filamu hii imesajiliwa na Bodi ya Filamu na imepewa daraja 16. Tumeileta kwenye ofisi ya mkoa miezi miwili iliyopita wanayo na hata kualika mgeni rasmi tuliwashirikisha. Tunashangaa tumeshajipanga na mgeni amefika Geita ndiyo wanazuia bila kujali gharama kubwa iliyotumika kuiandaa,” alisema Kapaya.
Rose alisema filamu hiyo ingekuwa na makosa ingezuiwa na bodi, hivyo wameshangaa kusikia malalamiko kutoka GGM ilhali filamu imezungumzia uhalisia wa maisha ya wachimbaji wadogo ambao ndiyo wananchi wengi wa Mkoa wa Geita.
Meneja Uhusiano wa GGM anayehusika na masuala ya jamii, Manase Ndoroma alisema si lengo la kampuni kuzuia filamu hiyo lakini kuna maeneo ambayo yanaeleza mgodi kuua na kunyanyasa watu jambo ambalo si la kweli.
Alisema mgodi unafanya kazi kwa mujibu wa sheria chini ya Serikali ya mkoa na endapo wangekuwa wanafanya shughuli zao kinyume cha sheria wangechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Agizo la Rais Magufuli
Julai mwaka jana, Rais John Magufuli akihutubia wakazi wa Geita mjini akitokea Kahama aliagiza masalia ya mawe hayo wapewe wananchi maskini.
Aliagiza viongozi wa mkoa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) waandae utaratibu wa kuwagawia wananchi magwangala hayo ili yawasaidie kuendesha maisha yao.
Pia, alipiga marufuku kuwanyima wananchi udongo huo wenye masalia ya dhahabu ambao humwagwa na mgodi wa GGM kwa kuwa wamiliki wa mgodi walikuja kutafuta dhahabu na si magwangala.
“Natoa wiki tatu, mchakato wa kuyagawa magwangala uanze mara moja, naagiza NEMC (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) kwa kushirikiana na taasisi nyingine, waanze utaratibu wa kuyagawa magwangala mara moja na asije akajitokeza mtu kuzuia agizo langu,” alisema.
Baada ya agizo hilo, Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo aliingia katika mzozo na wanasiasa wa Mkoa wa Geita alipowashutumu kuwa wanamchongea yeye na viongozi wa mkoa kwa Rais Magufuli ili waonekane hawatekelezi agizo hilo la kuwagawia wananchi magwangala.
Akitangaza utaratibu wa kuanza kugawa magwangala hayo, Profesa Muhongo alisema wanasiasa wa Mkoa wa Geita wamekosa subira na badala yake kwenda kwa Rais kuwachongea ili viongozi wa mkoa na wizara waonekane hawafanyi kazi.
Profesa Muhongo ambaye Mei 24 aliondolewa katika wadhifa huo na Rais Magufuli mara baada ya kupokea ripoti ya kamati ya kwanza aliyoiunda kuchunguza shehena ya makontena yenye mchanga wa dhahabu (makinikia) yaliyozuiliwa katika bandari tangu Machi alisema:
“Wanasiasa tuliwaeleza wazi kwamba kwa kushirikiana na Nemc tunatafuta maeneo ambayo ni rafiki na hayana madhara ya kimazingira, lakini nyinyi wanasiasa mkapeleka kilio kwa Rais mara ya tatu mkidai mpewe magwangala,” alisema Profesa Muhongo“Mmekosa uvumilivu.
Tulisema mvumilie tukague na tuone hakuna madhara, lakini hamkukubali. Tunakubaliana hapa baadaye nyie mnaenda kudai kwa Rais wakati huku kuna zebaki yenye madhara makubwa. Lakini kutokana na nyie kutokuwa wavumilivu, ndio imesababisha haya yote.”
Maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya kumwaga magwangala hayo ni Nyamikoma, Lwenge, Kasota na Samina B.
Hata hivyo, Kanyasu alijibu shutuma hizo za Profesa Muhongo akisema wabunge walilazimika kumweleza Rais suala hilo kutokana na muda mrefu kupita bila ya ahadi hiyo kutekelezwa.
Msimamo wa mkoa
Kuhusu uamuzi huo, Kapufi alisema mkuu wa mkoa alifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka GGM kwamba, “Kuna kipande (cha filamu) kinamwonyesha mtu anayeigiza kama ofisa uhusiano wa GGM akiwahonga waandishi wa habari ili taarifa mbaya za kampuni hiyo zisiripotiwe; ingawa ni maigizo, maudhui hayo yakienda kwa jamii yanaweza kuibua hisia kuwa ndiyo hali halisi.”
Hoja nyingine aliyosema inalalamikiwa na GGM ni suala la malipo ya fidia na baadhi ya maeneo yanayotajwa kwenye filamu kuwa fidia haijalipwa, malipo hayo yalishafanyika.
“Baada ya kikao cha pamoja kilichoongozwa na naibu waziri na kuhudhuriwa na pande zote pamoja na wadau wakiwamo wabunge, tumekubaliana kukutana saa tisa alasiri ya Jumatatu Julai 31, kufikia muafaka wa jambo hili,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kikao hicho kitakachofanyika ofisini kwake pia kitajadili suala la mabadiliko ya jina la filamu kutoka ‘Tuijenge Geita Yetu’ iliyosajiliwa katika ofisi ya utamaduni, kwenda ‘Magwangala’ ambayo ndiyo iliyokuwa imetarajiwa kuzinduliwa.
Kapufi alisema kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa, uzinduzi huo utafanyika siku itakayopangwa baada ya majadiliano na maridhiano kati ya wadau na marekebisho ya kasoro hizo zilizobainika.
Alisema GGM ambao ndiyo wanaolalamikia kasoro hizo, watalazimika kubeba dhamana ya kulipia gharama za marekebisho na hafla ya uzinduzi wa filamu hiyo ambayo pia inalenga kutangaza fursa za kiuchumi zinazopatikana mkoani Geita kupitia sekta za uchimbaji madini, uvuvi na kilimo pamoja na vita dhidi uvuvi haramu.
Nyongeza na Peter Saramba
No comments:
Post a Comment