Thursday, October 12

Mama Maria Nyerere awaasa vijana kuzingatia utamaduni


Dar es Salaam. Mama Maria Nyerere, amewaasa vijana kuzingatia utamaduni na michezo ili kuweka sawa akili zao.
Amesema michezo hukutanisha watu wengi na kuwawezesha kubadilishana mawazo yenye kujenga katika maisha.
Mama Maria amesema hayo leo Alhamisi alipozungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbasi nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Maelezo imesema Mama Maria amesema michezo ni hatua muhimu ya ukombozi wa fikra kwa vijana kwa kuwa wakiizingatia wataweza kufanya kazi na kujipatia mahitaji muhimu kama vile chakula na kuondokana na dhana ya utegemezi.
“Vijana wamejikita katika mambo maovu, sasa kitakachoweza kusaidia ni michezo kwa kuwa inawachangamsha, kuwakutanisha na kubadilishana mawazo mazuri na kwa sasa wanaendelea vyema na masuala haya ya michezo ambayo yanadumisha pia utamaduni,” amesema.
Mama Maria, ambaye ni mjane wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere amesema kwa sasa vijana wameanza kujirudi katika kudumisha utamaduni kwa kuwa walitaka kupotoka na kuacha utamaduni wao.
Amesema watoto wanazaliwa bila ukomavu wa akili katika utamaduni, lakini pia hawapati elimu ya kutosha kutoka kwa wazazi kuhusu utamaduni, hivyo matokeo yake ni kuishia kuwa na watu wenye tabia za ajabu.
Mama Maria amesema jukumu la ukombozi wa vijana kutoka katika vitendo vibovu ni la Watanzania wote kuwaelimisha vijana kuhusu michezo ili kuweka akili zao sawa.
Amesema kujitegemea kwa vijana na hasa katika kufanya kazi kutawawezesha kutimiza ndoto zao na za Taifa lenye kipato cha kati kwa kutegemea uchumi wa viwanda.

No comments:

Post a Comment