Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani kile ilichokiita "mashambulizi ya kikatili na woga" dhidi ya makao makuu ya jeshi la ubalozi wa Ufaransa katiika mji mkuu wa Burkina Faso, Ougadougou.
Taarifa ya Baraza hilo imetaka waliohusika na mashambulizi hayo ya Ijumaa (2 Februari) yaliyouwa wanajeshi wanane, kukamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Katika mashambulizi hayo pia washambuliaji wanane waliuawa, wanne kwenye makao makuu ya jeshi na wengine wanne karibu na ofisi za ubalozi wa Ufaransa, kwa mujibu wa wizara ya mawasiliano ya Burkina Faso.
Serikali pia ilisema idadi hiyo ya waliouawa haijumuishi raia ambao nao wanahofiwa kupoteza maisha kwenye mkasa huo unaohusishwa na kundi la al-Qaida magharibi mwa Afrika.
Waziri wa Ulinzi, Clement Sawadogo, alikiambia kituo kimoja cha redio kwamba kiasi cha watu 80 walijeruhiwa, baadhi yao wakiwa na hali mbaya sana.
Mapema hapo Ijumaa, msemaji wa serikali, Remis Dandjinou, aliyaita mashambulizi hayo kuwa ni ya "kigaidi", bila ya kutaja washambuliaji waliohusika.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliyalaani mashambuliz hayo na alizungumza na mwenzake wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore, siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa Ikulu ya Ufaransa.
"Ufaransa imedhamiiria kupambana na makundi ya kigaidi kwa kushirikiana na mataifa ya Sahel," ilisema taarifa ya Kasri la Eylsee.
Meya wa Ougadougou, Armand Beouinde, aliliambia gazeti la Le Monde la Ufaransa kwamba mashambulizi hayo yanawezakana sana kufanywa na wapiganaji wa siasa kali. Hata hivyo, hakuna kundi lililodai kuhusika nayo kwa haraka.
Jinsi mashambulizi yalivyotokea
Watu wenye silaha na wasiofahamika walianza kurusha risasi majira ya saa 4:00 asubuhi siku ya Ijumaa, wakiilenga ofisi ya waziri mkuu, jengo la mkuu wa jeshi na ubalozi wa Ufaransa mjini Ougadougou.
Moshi ukifuka kutoka jengo la makao makuu ya jeshi la Burkina Faso kufuatia mashambulizi mjini Ougadougou.
Wanajeshi na maafisa wa kikosi maalum baadaye waliyazingira majengo hayo na kuanza msako, kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio.
Wizaya ya Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa iliwataka raia wake wanaoishi Ougadougou kubakia kwenye maeneo salama, kufuta safari zao kwenye mji huo na kufuata maelekezo kutoka mamlaka za Burkina Faso.
Mwandishi huyo wa dpa aliripoti kuona moshi mkubwa ukifuka kwenye ofisi ya mnadhimu mkuu wa jeshi, huku magari kadhaa ya wagonjwa yakielekea kwenye jengo hilo.
Shahidi mmoja aliiambia dpa kwamba aliona washambuliaji watano wakishuka kwenye gari na kuwarushia watu risasi kabla ya kuelekekea kwenye ubalozi wa Ufaransa.
Wakati huo huo, wanajeshi waliweka ulinzi maalum kwenye majengo ya ofisi ya mnadhimu mkuu wa jeshi, waziri mkuu na ubalozi wa Ufaransa.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa likikumbwa na ghasia za washambuliaji wa itikadi kali kutokea Mali katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo mwezi Agosti 2017, mashambulizi kwenye mkahawa mmoja mjini Ougadougou yaliuwa watu 18.
Mwaka 2916, kiasi watu 30 waliuawa wakati wapiganaji hao wa siasa kali walipouvamia mkahawa mwengine kwenye mji huo mkuu.
No comments:
Post a Comment