Saturday, March 3

Mbinu za kuwaepuka madalali wa mazao


Wiki iliyopita jarida hili lilichapisha makala kuhusu kilio cha wakulima, wakiwalalamikia madalali wa mazao kuwa ni kikwazo cha maendeleo yao.
Katika makala haya, wakulima wanaeleza jinsi ambavyo baadhi ya nyakati, wanavyoweza kuwaepuka madalali hao ambao uwepo wao katika masoko unaonekana kuwa kama mfumo rasmi wa uendeshaji wa masoko nchini.
Mkulima wa matunda kutoka wilayani Bagamoyo, Lucy Salema anasema : “Hawa mbona kuwaepuka ni kazi rahisi tu ilimradi tu kuwepo na utaratibu maalum kwenye haya masoko makubwa mfano Kariakoo ili madalali wasiwepo kabisa.”
Anasema kuwa kinachotakiwa kwa mkulima ni kutoa taarifa mapema kwa kiongozi wa soko kabla hajapeleka mazao sokoni, ili kiongozi huyo ajue kwamba ni wakulima wangapi wataingiza mazao sokoni na taarifa hiyo itolewe mwezi mmoja kabla.
Utaratibu huo utampa nafasi kiongozi wa soko kujua ni wakulima wangapi wataleta mazao ya aina moja na wangapi wataleta aina nyingine. Ni utaratibu ambao utasaidia kuondoa msongamano wa wingi wa watu wanaopeleka mazao.
“Wakulima tukienda sokoni wengi, madalali wanapata nafasi nzuri ya kutuumiza, kwa sababu wanajua mkulima hawezi kumkataa maana matunda ukikaa nayo sana yanaharibika, lakini kiongozi wa soko akisimama imara hatuwezi kunyanyaswa na watu hawa,” anasema.
Kwa mkulima, Salim Magege anayeishi mkoani Mwanza, anasema kinachotakiwa kufanywa ni ushirikiano kati ya mkulima, kiongozi wa soko na mnunuzi bila hivyo hawawezi kumaliza tatizo hilo la madalali sokoni wanaokandamiza haki za wakulima.
“Uwezekano wa kutotumia madalali sokoni upo tena mkubwa tu, yaani ni bora kama kuna ushuru mkulima nilipe moja kwa moja kwa uongozi wa soko na uongozi wa soko unikutanishe moja kwa moja na mnunuzi,” anasema.
Anasema kinachofanyika sasa ni kwamba madalali wanachukua fedha, uongozi wa soko nao wanachukua fedha kwa hiyo kuna mlolongo mkubwa ambao mkulima anapitia.
“Ukiangalia kiashiria kikubwa kuwa madalali wanatudhulumu ni kushusha bei. Kwa mfano, mkulima anaenda soko kuu la Kariakoo kwa lengo la kuuza vitunguu Sh 150,000 kwa gunia, lakini ukikutana na dalali unaambiwa uuze kwa 130,000,”anaeleza.
Anasema kuwa madalali wakipanga bei, hawataki mabishano kwani ukifanya hivyo huwezi kupata mteja na bidhaa yako itaoza.
Viongozi wa masoko wawazungumzia madalali
Saidi Mzuzure ni mjumbe wa kamati ya soko la Sterio wilayani Temeke anasema: “Sio kweli kuwa tunawabeba madalali kwa sababu kiongozi wa soko ni kiongozi wa mteja na mkulima kwani bila wao hakuna soko.’’
Akielezea taratibu za soko lao, anasema madalali nao ni wakusanya kodi, kwa kuwa mkulima anapouza bila ya kumtumia dalali Serikali ya wilaya inakosa mapato.
“Tukisema pia hawa wakulima wauze bila kupitia kwa dalali hatuwezi kukusanya ushuru, kwa sababu mkulima anapokuja hapa na kuuza mazao yake bila dalali akipata tu mtu akamuuzia utakuta mkulima yule anaondoka na yule mnunuzi anaondoka na mwishowe Manispaa haipati mapato,”anasema.
Isihaka Ofiole ambaye ni Kaimu Katibu wa soko la Buguruni, anasema wanatambua uwepo wa madalali katika soko hilo ila kuhusu wakulima kudhulumiwa hawalitambui hilo kwani makubaliano hufanywa kati ya wakulima wenyewe na madalali.
“Hilo la kudhulumiwa sijapata malalamiko, lakini kwa kucheleweshewa malipo inatokea mara kwa mara na hii ni kutokana na wakulima na madalali kutotoa taarifa kwa uongozi wa soko pindi wanapokabidhiana mazao yao,” anasema.
Ofiole hata hivyo, anasema madalali wanatokana na wakulima wenyewe kwa kuwa ndio wanaowapa mzigo. Anasema kilichozoeleka ni ule utamaduni waliojiwekea wakulima wa kuuza kupitia kwa dalali hasa kwa wale wanaoleata mzigo mkubwa.
“Lakini pia wakati mwingine mkulima ni mgeni, labda ametokea mkoani kwa hiyo huyu huwezi tu ukamwachia auze vinginevyo watu watamzunguka huko nje na hatimaye matapeli watamuibia, ndiyo maana tunamkabidhi kwa dalali,” anasema.
Anasema dalali anapokabidhiwa mzigo na mkulima na kuuhifadhi anabeba jukumu la kuulinda, kuuhifadhi na hata kulipia ushuru. Ni jukumu lake kwa kuwa yeye ndiye muuzaji.
Ofiole anawashauri wakulima kuwaona viongozi wa masoko kabla ya kuwapa mzigo madalali. Anasema kosa wanalolifanya wakulima ni kukabidhi mzigo kwa dalali bila kuwa na hati ya maandishi, hivyo uongozi unashindwa kuingilia kati kwa sababu hakuna uthibitisho unao onyesha kuwa wawili hao walikabidhiana mzigo.
Wenyewe wajitetea
Dalali wa mbogamboga katika soko la Temeke Sterio, Amosi Kimbute, anasema wanachakifanya wao ni utekelezaji wa majukumu yao, kwani hata kama wasingekwepo bado wakulima wangelalamika.
‘’Ukweli ni kwamba bila sisi hawawezi kuuza mazao yao. Nasema hivyo kwa sababu madalali tuna mtandao mkubwa na tunajua wapi kuna wanunuzi na yupi mnunuuzi wa kweli,”anasema.
Kuhusu bei anasema ni suala la makubaliano kati yao na wakulima na hata wanapopanga wao madalali, lazima wawaulize wenyewe wakulima kama wameridhia au hawajaridhia.
“Sawa tunapanga bei lakini huwa hatulazimishi mtu kukubaliana na bei ile kama akikataa basi na mara nyingi wakikataa tukiwaacha wanaanza kulalamika na ku tubembeleza,”anaongeza.
Anasema kwa mkulima anayelalamika kutapeliwa basi amekutana na dalali ambaye hatambuliki katika soko, kwa sababu madalali wanajuana na wanahakikisha hakuna mkulima anayedhulumiwa.
‘’Unakuta mkulima analeta tikiti zaidi ya 2000 na unapomtafutia mteja dalali anachukua Sh200 pekee sasa hapo namdhulumu vipi?anahoji.
Naye Omari Othman ambaye ni dalali wa matunda katika soko la Buguruni, anasema madalali hawapangi bei ila wanapanga pamoja kati yao na mkulima.
“Kwa wale wanaokwenda shamba sawa lakini sisi wa sokoni inategemea ila mara nyingi bei tunapanga pamoja na mkulima na tunauza pamoja hadi pale matunda yatakapokwisha,”anasema Othman na kuongeza:
“Changamoto iliyopo ni kwamba wanunuzi wanachelewa kulipa fedha, lakini pia hata matunda yanayokuja mengine hayana viwango hivyo unakuta tunayagawanya katika madaraja. Sasa lawama zinakuja unapomweleza kuwa matunda yako yapo daraja la mwisho, hivyo unatakiwa kuuza kwa bei hii. Sisi huwa tunayagawa katika madaraja matatu yaani la kwanza la pili na la tatu”

No comments:

Post a Comment