Saturday, March 3

Vigogo Maliasili watoa kauli kinzani kifo cha faru

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi. 
Dar es Salaam. Licha ya mauaji ya faru mmoja katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kutokea Desemba mwaka jana, hadi sasa hakuna taarifa kamili iliyotolewa huku watendaji waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakitoa kauli zinazokinzana.
Wakati katibu mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akisema kunafanyika uchunguzi wa kawaida, Naibu Waziri Japhet Hasunga amekaririwa akisema unafanyika uchunguzi wa kina ukihusisha kuundwa kwa kamati maalumu.
Licha ya kusema kuna uchunguzi wa kawaida, Meja Jenerali Milanzi amekanusha pia madai ya kuhojiwa viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Chanzo cha taarifa kimelieleza Mwananchi kuwa baada ya wizara kupata taarifa iliundwa kamati ya kuchunguza tukio hilo ambayo pia iliwahoji maofisa wa Tanapa na kwamba kazi hiyo imekamilika.
Alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu suala hilo juzi, mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alimtaka mwandishi ampigie baada ya saa moja kwa maelezo hakuwa sehemu nzuri.
Baada ya muda huo kupita, meneja mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete alimpigia simu mwandishi akisema ametumwa na bosi wake kumsikiliza.
Alipoulizwa taarifa za mauaji ya faru huyo katika Hifadhi ya Serengeti na kwamba kuna maofisa wa Tanapa wamehojiwa na wizara, Shelutete alikiri kutokea kwa mauaji lakini alikanusha maofisa kuhojiwa.
“Taarifa hizo ni za kweli na ziko mikononi mwa vyombo vya dola zinashughulikiwa. Si kweli kwamba tulichelewesha taarifa, tulitoa mapema tu,” alisema Shelutete alipoulizwa ni kwa nini taarifa za kuuawa kwa faru huyo hazikutolewa mapema.
Shelutete alimwahidi mwandishi kuwa atampigia tena baadaye. Baada ya saa tano kupita bila simu kupigiwa, mwandishi alimpigia tena lakini hakupokea bali alituma ujumbe wa maandishi akiandika, ‘Nakupigia’.
Meneja huyo hakupiga simu badala yake alitoa taarifa kwa vyombo vya habari juzi kuhusu tukio hilo ikisema Tanapa inawashikilia watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwa miongoni mwa mtandao wa ujangili na mauaji ya faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Desemba mwaka jana.
“Pamoja nao, shirika pia limefanikiwa kukamata bunduki aina ya rifle inayoaminika kutumika katika tukio hilo. Shirika linaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya dola kukamilisha uchunguzi utakaopelekea kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika,” imesema taarifa ya Tanapa.
Jana alipopigiwa simu, Shelutete alisema lengo la kutotoa taarifa hiyo mapema ilikuwa ni kulinda uchunguzi unaoendelea.
“Hata hiyo taarifa unaiona tumeitoa kwa ufupi kwa sababu the more you reveal to the public, (kadri unavyotoa taarifa kwa umma) the more unapoteza chance (nafasi) za kuwakamata hao majangili, kwa sababu ni mtandao mkubwa. Naomba muwe wavumilivu, uchunguzi ukikamilika tutawapa taarifa,” alisema Shelutete.
Ufafanuzi wa wizara
Akizungumza kwa simu, Meja Jenerali Milanzi alikiri kutokea kwa mauaji akisema ni ya kawaida na kwamba kuna uchunguzi wa kawaida unaendelea kuhusu hilo.
“Ni kweli. Mara nyingi huwa ni ‘routine investigation’ inafanyika lakini si kuwahoji viongozi wa Tanapa. Ikitokea ‘incident’ (tukio) yoyote kama mnyama amekufa au ameuawa kunakuwa na ‘routine investigation’. Huwa ni kwenda field pale wanapotupa taarifa. It’s a normal investigation (ni uchunguzi wa kawaida).
Meja Jenerali Milanzi alisema Tanapa waliwapa taarifa mapema na walishaanza kufuatilia.
Alisema licha ya mauaji ya mnyama huyo, bado faru wapo wengi ijapokuwa hakutaja idadi.
“Faru bado wapo hawawezi kwisha. Hata tembo wanapokufa huwa tunachunguza ametoka familia gani. Mnyama akifa ni kawaida mzoga wake kuliwa, lakini hawa wakubwa tunawalinda hata wasiliwe na ‘predators’ (wanyama wanaokula nyama)”.
Alipoulizwa sababu ya Tanapa kuchelewesha taarifa kwa vyombo vya habari alisema, “Kwani ulitaka tufanyeje? Huo ukimya mimi sifahamu kwa nini, labda nitazungumza na Tanapa, lakini naona wametoa taarifa yao jana (juzi).”
Lakini Naibu Waziri Hasunga alisema baada ya kupata taarifa kutoka Tanapa waliunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
“Tuliunda kamati kupata taarifa za kina baada ya kupata taarifa ya Tanapa. Hawakuchelewesha taarifa, ila tuliona kuna haja ya kujiridhisha zaidi,” alisema Hasunga.

No comments:

Post a Comment