Tatizo liko wapi? Binafsi naona kuwa hatua ya kufungia nyimbo hizi haitamaliza tatizo kwani hatua iliyofanyika ni kubandika tu bandeji kwenye kidonda kilichooza. Pengine tujiulize kwanini nyimbo ambazo zinasemekana ‘hazina maadili’ ziliweza kutungwa na kurekodiwa? Kwanini ziliweza kurushwa kwenye vyombo vya utangazaji bila kuonekana shida yoyote mpaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na TCRA waingilie kati? Kwanini vijana wengi hawaoni tatizo la nyimbo hizo?
Kuna usemi maarufu usemao ‘Sanaa ni kioo cha jamii’. Ukiangalia kwenye kioo na kukuta sura mbaya inakuangalia basi ujue hivyo ndivyo ulivyo, kuvunja kioo au kubadili kioo hakutabadili sura yako.
Unaweza ukaikubali sura hiyo au ukaanza mkakati wa kutumia vipodozi kujipa mvuto unaoutaka. Kazi za wasanii zinaonyesha tu jamii ilivyo.
Mtoto aliyelelewa na wazazi wenye mdomo mchafu haiwi taabu kwake kuwa na mdomo mchafu, tena anashangaa sana akianza kukatazwa kutoa maneno machafu, anaona anaonewa kwa kuzibwa mdomo bila sababu za msingi. Hivyo kutunga wimbo uliojaa matusi au dalili za matusi kwake si tatizo, ndivyo jamii yake ilivyomlea.
Na wimbo huo utapokelewa vizuri tu na jamii yake kwani hayo ndio maisha yao ya kila siku. Niliwahi kuongea na mzazi wa mwanamuziki mmoja ambaye wimbo wake umeingia katika orodha ya kupigwa marufuku, mama yule alikuwa anajisifu kuwa yeye ndiye aliyeutunga wimbo anaoimba mwanae.
Turudi nyuma miaka 23 iliyopita. Uongozi wa awamu ya tatu ulipoingia madarakani, Wizara ya Utamaduni ilipata pigo ambalo matokeo yake yanaonekana sasa. Katika awamu hii maofisa utamaduni, mkoa na wilaya walifutika. Na baadaye kufufuka kinyemela wakiwa chini ya Idara ya Elimu katika halmashauri mbalimbali.
Hata huko walifufuliwa baada ya kuonekana kunahitajika mtu atakayekuwa akishughulikia kuratibu shughuli kama za Mwenge na sherehe mbalimbali.
Ofisa Elimu alimteua mwalimu aliyemuona anapenda sanaa na kumpa cheo cha uofisa utamaduni.
Maafisa hawa hadi leo bado ni utata, hawana bajeti, hawahusishwi kwenye vikao mbalimbali vya halmashauri, kila wilaya au halmashauri ikiwa na utaratibu wake. Mfano hapa Dar es Salaam kuna halmashauri za Ubungo, Kinondoni, Ilala na Temeke, ni halmashauri ya Kinondoni tu yenye sheria ndogo zinazohusu mambo ya sanaa na burudani, na sheria hizo zinahusiana zaidi na utoaji vibali tu kwa shughuli mbalimbali. Ukiona mkanganyiko huu kwa maofisa utamaduni wa jiji hili tu, je hali ikoje katika halmashauri za nchi nzima?
Waziri anayehusika na Utamaduni hawaongelei maofisa utamaduni hawa kwani hawako katika wizara yake na Waziri wa Tamisemi hawaongelei kwani hawana umuhimu huo kwake. Lakini hawa watu ndio kiungo muhimu sana katika kulinda na kuelekeza ‘maadili’ ya Kitanzania.
Awali walikuwa chini ya Wizara ya Utamaduni walikuwa ndio watekelezaji wa Sera ya Utamaduni, kwa sasa hawawajibiki kwa hilo, hivyo sera ya Utamaduni ni kitabu kiko katika makabati ya Wizara ya Utamaduni tu. Katika miaka hiyo ya nyuma nchi ilikuwa japo na maono kuwa inataka kwenda wapi kimaadili, na ikawa na utekelezaji wa pamoja wa maono hayo.
Kupotea kwa maofisa hawa kulikuja wakati mmoja na kuongezeka kwa vyombo vya utangazaji, luninga na redio.
Vyombo hivyo ndivyo vikaanza kubeba pengine bila kujua au kwa makusudi nafasi ya kulea maadili ya watoto wa Kitanzania. Malezi ya miaka mingi sasa yanatoa matunda, vijana waliokuwa na umri wa miaka 10 au chini zaidi mwaka 1995 na waliozaliwa baada ya hapo, ndio hao watunzi wa nyimbo ambazo zinaonekana hazina maadili, ni vigumu kwao kueleza au kujua maadili ya Kitanzania ni yepi.
Wanamuziki, watangazaji, waandishi, maproducer, mameneja wa wanamuziki na kadhalika wengi ndio waliozaliwa katika kipindi hiki.
Teknolojia imewezesha kazi ya muziki kuwa rahisi sana, ukiwa na kompyuta na microphone moja unaweza kujifungia chumbani kwako ukarekodi wimbo na kuutuma kwa barua pepe mpaka kwa mtangazaji na wimbo ukaanza kurushwa hewani katika kipindi cha masaa kadhaa.
Hivyo kama hakuna aliyelelewa kuona ukakasi katika wimbo basi umma bila kujali umri au uhusiano unajikuta ukisikiliza maneno ambayo kwa kawaida huwa faragha na kwa watu wazima wenye aina fulani ya mahusiano tu, maneno hayo yanatamkwa hadharani bila kumumunya.
Kuna haja kubwa ya Wizara inayohusika na Utamaduni kujiangalia upya na kujipanga upya ili kukabiliana na hali hii na si kuishia kufanya kazi rahisi ya kufungia nyimbo tu.
No comments:
Post a Comment