Saturday, March 3

Baraza la Maaskofu : Majadiliano ndio nyenzo ya kupambana na ubinafsi


Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuheshimu matakwa ya wananchi na kuonyesha dhamira yake ya dhati kwa kuendeleza maongezi ya mchakato wa Katiba Mpya nchini, na kuwa majadiliano ndio nyenzo ya kupambana na ubinafsi.
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Daniel Dulle, alisema hayo Ijumaa wakati akifungua kongamano la kujadili Katiba na ujenzi wa amani wakati wa uchaguzi lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mjini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja kwa TEC kutoa kauli kama hiyo, kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa Februari 11 mwaka huu, Baraza hilo katika ujumbe wake wa Kwaresma lilitoa msimamo katika masuala matatu kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo lilionya madhara ya kutozingatia matakwa ya Katiba katika kuendeleza shughuli za kisiasa.
Amesema ili imani iendelee kuwepo nchini ni lazima majadiliano yawe ndio nyenzo kuu itakayosaidia kuhuisha mchakato wa Katiba mpya.
Historia ya mchakato wa katiba mpya
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa nchini Tanzania marekebisho ya Katiba 2011, yanalalamikiwa sana kwa kutungwa bila kuwapa watanzania nafasi ya kushiriki na pia kumrundikia Rais madaraka yote bila hata kuwashirikisha wapiga kura wake.
Wanadai kuwa katika jamii tuliyo nayo hivi leo demokrasia na utawala wa kidemokrasia ni moja ya dhana muhimu sana zinazoleta mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yoyote.
Pia wanasema kuwa demokrasia na utawala wakidemokrasia sio tu vichochezi vya maendeleo bali ni mihimili mikubwa yakupambana na umaskini hasa katika nchi kama Tanzania na nyinginezo.
TEC yahimiza kuwepo majadiliano
Gazeti la Mtanzania limeripoti kuwa Padri Dulle, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TEC Padri Raymond Saba , alisema baada ya mchakato wa Katiba Mpya kukwama sasa ni fursa kuendeleza majadiliano juu ya suala hilo ili kudumisha amani nchini.
“Majadiliano ni nyenzo ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga umoja huo lazima kuwepo na upendo, mshikamano na maridhiano ya watu na kila mtu kupewa nafasi ya kutoa maoni hata kama yanapingana na mtu mwingine na ukiwa unapatanisha kwa njia hiyo unaitwa mwana wa Mungu.
“Ndilo lengo la kukaa hapa na kujadiliana ili kujenga Taifa letu kwa lengo la kupata Katiba Mpya ambayo kila mmoja anaitamani. Kunapotokea mtafaruku ndipo kunakuwa na chuki kama kikundi kingine hakishirikishwi. Haki na amani ni matunda tu, kwani ukosefu wa haki ni chanzo cha vita inayoacha makovu na chuki za kisiasa kwenye chaguzi. Kama tunataka kukwepa haya makovu lazima watu tujenge tabia ya kujadiliana,” alisema.
Historia ya Kanisa Katoliki
Alisema tangu miaka ya 1800, Kanisa Katoliki limekuwa likitoa miongozo kuhusu masuala ya utawala ili kudumisha amani.
“Suala la Katiba ni nia ya watu wote si ya mtu mmoja, ni sauti ya watu na kadiri watu wanavyohitaji sheria na miongozo. Pengine kikundi kikubwa kinahitaji kidogo hakihitaji cha msingi ni kuangalia wananchi wanahitaji nini kwani kwa mujibu wa ibara ya nane ya Katiba ya sasa, Katiba ni mali ya wananchi,” alisema.
Kituo cha Demokrasia (TCD)
Wakati huohuo Profesa Mwesiga Baregu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), James Mbatia, aliitaka Serikali kuhakikisha kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020, Katiba Mpya inapatikana.
Baregu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ni vema kukamilisha kiporo hicho cha Katiba.
Ameongeza kuwa kuna ishara za viashiria vya hatari zimekwisha onekana katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni hususani Jimbo la Kinondoni, na ni vema tukaanza mchakato huo.
Njia Tatu zakuendeleza mchakato
Aidha, Profesa Baregu, alipendekeza njia tatu za kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hali iliyopo lazima kuwepo na njia ya kuishawishi Serikali.
“Kwanza twende kwenye kura ya maoni, tunaweza kutangaza kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa ila sijui kura ya maoni kama itaendeshwa kwa uhuru au haki. Kwa sababu hata katika Katiba pendekezwa tumeona asilimia 85 ya maoni ya wananchi yamenyofolewa.
“Pili kuundwe Bunge la Katiba lenye wajumbe wasiokuwa wabunge kwani hawa waliopo bungeni watatengeneza Katiba ya kuwalinda na tatu kuundwe tume ya wataalamu wa Katiba kama walivyofanya wenzetu Kenya, kwani mahali tulipofika lazima tutoke kwenye ujumla ujumla tuwe na mashinikizo ya kuitaka Serikali ifanye nini kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Pamoja na mambo mengine alieleza kushangazwa na baadhi ya mawaziri wanaodai kuwa rasimu ya pili ya Katiba Mpya iliwalisha wananchi maoni jambo ambalo si kweli.
“Baadhi ya mawaziri wanasema mambo ya kipumbavu eti watu wamelishwa maneno na tume, kusema kweli hiyo ni dharau kwa watu kuwa hawawezi kusema Rais apunguziwe madaraka na mambo mengine,” alisema.
Chama cha ACT- Wazalendo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo, Yeremia Maganja, alisema hitaji la Katiba ni tangu vizazi na vizazi hivyo Serikali haitakiwi kupuuza takwa la wananchi.
“Pia tunaona tatizo linaloikabili nchi yetu ni taasisi ya rais kutokuwa na mamlaka inayoisimamia, ndiyo maana rais anaonekana kuwa amegeuka Mungu mtu,” alisema.
Aidha, Rais mstaafu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), John Seka, alisema ili kuwepo na chaguzi za kidemokrasia lazima kuwepo na mfumo wa kisheria unaozingatia kutibu vidonda vya chaguzi zilizopita.
“Pia kuwe na miundombinu za kuwezesha vyama vyote ikiwamo kupatiwa gharama za uchaguzi pamoja na mambo mengine,” alisema.

No comments:

Post a Comment