Saturday, March 3

SERIKALI YATOA TAMKO KUIJIBU MAREKANI, UE


SERIKALI imeutaka Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na nchi ya Marekani kutotoa matamko pasipo kuwa na taarifa za kutosha juu ya matukio ya watu kuuawa, kupigwa risasi na kutekwa.
Kauli hiyo ya serikali imekuja ikiwa ni takribani wiki moja tangu EU na kabla ya hapo ubalozi wa Marekani kutoa tamko kukemea na kutaka uchunguzi wa kina juu ya matukio yenye viashiria vya ukatili na vitisho hapa nchini ikiwamo watu kuuawa, kupigwa risasi na kutekwa.
Katika tamko lake lililotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, ambalo liligusia shutuma zinazoelekezwa Tanzania kushirikiana kibiashara na Korea Kaskazini na hivyo kudaiwa kuvuja mkataba Umoja wa Kimataifa ambayo imeiwekea vikwazo nchi hiyo, serikali pia ilieleza kushangazwa na haraka ya nchi hizo kutoa matamko katika wakati ambao vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wake.
Zaidi serikali ilikwenda mbali na kuhoji EU pamoja na Marekani kutoa matamko hayo sasa na ikishindwa kufanya hivyo wakati yalipotokea mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji Mkoani Pwani tena yakiwagusa viongozi wa chama tawala.
“Matamko mbalimbali yanaonesha ukosefu wa uelewa wa usalama na changamoto ambazo serikali imekuwa ikikumbana nazo katika miezi 18 iliyopita, taarifa hizo zilizotolewa hazikuzingatia ukweli wa mwenendo wa kisiasa na usalama nchini” lilieleza tamko hilo la serikali.
Serikali pia ilieleza udhaifu iliouona katika matamko hayo kushindwa kutambua hatua kubwa na muhimu zilizochukuliwa na Rais Dk. John Magufuli katika kapambana na rushwa, dawa ya kulevya, ukwepaji kodi, ujangili  na uwajibikiaji wa mamlaka za ulinzi na usalama.
“Wageni wetu washirika wanapaswa kujitahidi kuelewa mazingira haya magumu ambayo nchi inakabiliana nayo kabla ya kutoa taarifa zenye hisia zisizothibitishwa ambazo zinaweza kuleta ushawishi mkubwa kwa umma…kwa upande wetu tunakaribisha mazungumzo ya wazi kutoka kwa marafiki zetu na washirika juu ya masuala ambayo yanahitaji ufafanuzi ili waweze kupatiwa taarifa bora zaidi” lilieleza tamko hilo
Wiki iliyopita EU kupitia ofisi zake hapa nchini ilitoa tamko kukemea matukio yenye viashiria vya ukatili na vitisho hapa nchini ikiwamo kuuawa kwa Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Daniel John,  kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi, Akwilina Akwilini na mengine.
Tamko hilo la EU lilitolewa kwa ushirikiano na mabalozi wa nchi wanachama wenye uwakilishi hapa nchini na kuungwa mkono na mabalozi wa nchi za Norway, Canada na Uswisi.

No comments:

Post a Comment