Saturday, July 22

Tajiri wa Mererani ahukumiwa vifungo vya maisha

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Kilimanjaro, imemhukumu vifungo vya maisha jela, mfanyabiashara mashuhuri wa madini wa Mererani, Benedict Kimario (43), kwa makosa mawili ya ubakaji na ulawiti.

Mahakama hiyo ilimhukumu mfanyabiashara huyo vifungo vya maisha mara mbili kwa makosa hayo mawili.

Hukumu ya kesi hiyo ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Mrau wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, ilitolewa mjini Moshi na Hakimu Mkazi, Idan Mwilapo.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme, mshitakiwa alikuwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya ulawiti na kubaka mtoto mwenye umri wa miaka minane.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwilapo alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashitaka, umeweza kuithibitishia Mahakama pasipo kuacha shaka kuwa alitenda makosa hayo.

Hakimu Mwilapo alisema kitendo kilichofanywa na mshitakiwa huyo ni kibaya na kwa vile vitendo hivyo vinaongezeka katika jamii, Mahakama inalazimika kutoa adhabu kali ya kifungo cha maisha.

“Kwa hiyo kwa kosa la kwanza la kubaka utatumikia kifungo cha maisha jela na pia shitaka la pili la kulawiti nalo utatumikia kifungo cha maisha jela,” alisema Hakimu Mwilapo katika hukumu yake.

Awali Wakili Mndeme alidai mahakamani kuwa, mshitakiwa alitenda makosa hayo Mei 10 mwaka jana katika kijiji cha Mrau katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

 Tangu siku ya kwanza ya kesi, Novemba 30, 2016, mshitakiwa alikuwa akitetewa na Wakili Joseph Peter.

Wakili huyo alimtetea mshitakiwa kuanzia mwanzo wa kesi hadi shahidi wa nne wa upande wa mashitaka alipowasilisha ushahidi wake.

Hata hivyo, ilipofika shahidi wa tano, mtuhumiwa alibadili wakili na kuanza kumtumia Wakili Mussa Mziray.

No comments:

Post a Comment