Lissu, ambaye alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake, Area D mjini Dodoma, anapata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na kwa mara ya kwanza picha na sauti aliyorekodiwa zilitolewa kwa umma, Jumatano.
Tangu alipopigwa risasi, Lissu ameibua mijadala mingi huku watu wakijiuliza ni nani hasa aliyehusika katika jaribio la kutaka kumuua na kwa maslahi gani. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesisitiza kwamba linaendelea kuchunguza tukio hilo.
Chadema inavituhumu vyombo vya ulinzi na usalama na kusisitiza kwamba kuna haja ya kuruhusu vyombo vya uchunguzi kutoka nje ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Siku za nyuma wafuasi wa Lissu walijitokeza kumwombea, lakini walidhibitiwa na polisi kwa madai kwamba wanahatarisha amani.
Mikusanyiko yote ya kumwombea Lissu ilipigwa marufuku na wafuasi hao kutakiwa kufanya hivyo kwenye nyumba za ibada.
Matibabu ya Lissu yanagharamiwa na michango ya wananchi na wafuasi wa chama hicho na tayari zaidi ya Sh400 milioni zimetumika.
Oktoba 17, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa taarifa ya maendeleo ya matibabu ya mbunge huyo na kusema sasa ameimarika na muda wowote atasafirishwa kwenda nje ya Afrika kwa ajili ya awamu ya tatu ya matibabu yake.
Mbowe alibainisha kwamba mpaka kufikia Oktoba 10, matibabu ya Lissu yalikuwa yamegharimu Sh413 milioni.
Alisema sasa Lissu anakula mwenyewe na ameondolewa mashine za oksijeni zilizokuwa zikimsaidia kupumua.
Picha na sauti ya Lissu zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuvutia watu kuziweka kwenye kurasa zao. Wanasiasa nao waliandika kwenye kurasa zao za mitandao ya Twitter na Facebook.
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Mjomba tunashukuru kwa tabasamu hili la matumaini! Nakuombea afya iimarike kabla hujasema mengi. Tulia mjomba upone kabisa kwanza.”
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliandika waraka mrefu akifurahishwa na maendeleo ya afya ya Lissu. “Jana (Jumatano) nimefarijika kukusikia tena sauti yako tangu nikusikie nilipokuja kukusabahi hospitalini.”
“Sauti yako sasa imeboreka na kurudi sauti ileile uliyokuwa nayo kabla hujashambuliwa kwa risasi nyumbani kwako Dodoma. Watanzania wamefarijika sana kuwa bado uko hai na utaweza kuungana nasi tena kuendeleza mapambano ya kujenga demokrasia yetu.”
Si hao tu bali mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete naye aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Mungu hutenda wema siku zote. Ashukuriwe yeye kwa kazi ya kurejesha tabasamu katika sura yako na afya kwa wanaokuuguza.”
“Nimefurahi kukuona tena msomi, kiongozi wangu na mwanakamati mwenzangu wa Bunge ukitabasamu na mwenye afya njema. Mungu akulinde na akusimamie katika matibabu yako. Looking forward to see you back into your good shape (nataraji kukuona ukirudi tena ukiwa na siha njema).”
Mbali na wanasiasa hao, wananchi wa kawaida pia waliweka picha tofauti tofauti za Lissu alizopigwa akiwa kwenye kiti cha magurudumu na nyingine akiwa kitandani katika Hospitali ya Nairobi.
Mkazi wa Mwanza, Anthony Kasota aliandika katika ukurasa wake wa Facebook akiambatanisha na picha ya Lissu: “Hero, welcome back. Quick recovery (shujaa, karibu tena. Pona haraka).”
Akizungumzia suala la Lissu kuwa gumzo hasa wiki hii, katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema linatokana na ushujaa wake na mazingira ya tukio lenyewe la kupigwa risasi.
Muabhi alisema watu wameungana kumwombea kwa sababu wanatambua kwamba kila binadamu ana haki ya kuishi lakini zaidi ni kutokana na ujasiri wake wa kupaza sauti kwa niaba ya wengi ambao hawawezi kusema.
“Uwepo wa uhai wake ni muujiza, kila mtu lazima aguswe. Mbowe alieleza kwamba haijawahi kutokea mgonjwa aliyeongezewa damu nyingi katika hospitali anayotibiwa katika kipindi cha miaka 20,” alisema Muabhi.
Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa wapo watu wachache aina ya Lissu duniani na thamani zao huwa ni kubwa.
Muabhi alisema Lissu alijitoa muhanga kuikosoa Serikali waziwazi katika mambo mbalimbali.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Gideon Masika alisema sauti ya Lissu iliyosambazwa iliongeza matumaini mengi kwa wananchi kwa sababu kuambiwa tu anaendelea vizuri haitoshi mpaka waonyeshwe anaendeleaje.
Masika alisema tukio la mwanasiasa huyo kupigwa risasi na kunusurika kifo lilikuwa la kustaajabisha ndiyo maana kila mtu ana shauku ya kujua maendeleo yake.
Aliongeza kuwa Lissu anapata huruma ya umma kwa sababu alishajipambanua kama shujaa asiyeogopa.
“Nadhani akipona atakuwa na ushuhuda mkubwa wa kuieleza jamii, halikuwa tukio la kawaida. Matumaini ya Watanzania yanarejea baada ya kusikia sauti ya Mtanzania mwenzao na kuona anapata nafuu,” alisema mwanazuoni huyo.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo akizungumza na Mwananchi juzi alisema alibubujikwa machozi baada ya kuisikia sauti hiyo ya mwanasheria wa Chadema.
“Nilijikuta natoka machozi niliposikia sauti ya Lissu,” alisema Dk Shoo, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.
Dk Shoo alisema kupona kwa Lissu ni onyo kwa waliohusika katika tukio hilo.
No comments:
Post a Comment