Sheria namba 14 ya mwaka 2017 iliyopitishwa na Bunge iliridhia kuanzishwa kwa Shirika la Wakala wa Meli (Tasac) ambalo lilitajwa kuanza kazi, Februari 2018.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa Tasac, Japhet Loisimaye alisema hayo alipokutana na wadau wanaotoa huduma za bandari na meli wakati wa kupitia kanuni mpya zilizoundwa.
Alisema chombo hicho kimeanzishwa ili kuleta ufanisi zaidi kwenye masuala ya bandari na usafiri wa majini ili kama kuna yaliyosahaulika au kuwekwa tofauti yashughulikiwe.
“Tumekutana ili kupitia kanuni kabla chombo hiki hakijaanza kazi rasmi, kama kuna lililowekwa tofauti liweze kurekebishwa na kama kuna lililosahaulika liweze kuingizwa,” alisema Loisimaye.
Alifafanua kuwa uamuzi huo umefikiwa ili kuboresha huduma na kupunguza muda wa mteja kukaa na kusubiri mizigo pamoja na kuboresha huduma za bandari na meli.
Loisimaye alisema kitaanzishwa chombo ambacho kitashughulikia masuala ya barabara hivyo kwa sasa wataendelea kutumia kanuni zilizopo na jina la Sumatra.
Wakala wa Forodha wa Kampuni ya Fly Shipping, Edward Urio akizungumzia sheria mpya za Sumatra, alisema wao wakiwa wadau hawapingi sheria zilizoletwa ila wanamuongezea Mtanzania ugumu wa kuendesha huduma kutokana na adhabu zilizowekwa.
Alisema wanapoanzisha kampuni ya kutoa huduma mtaji wake ni Sh50 milioni lakini kwa mzigo wa mteja utakaopotea watatozwa faini ya Sh40 milioni na kwa kosa litakalofanyika ni Sh60 milioni.
“Tunamuomba Rais atutengenezee mazingira mazuri ya kufanya biashara kwani adhabu iliyowekwa ni kubwa” alisema Urio.
Alisema sheria mpya zinawabana kuagiza baadhi ya bidhaa ikiwamo mashine kubwa za migodi hivyo wameomba ifanyiwe marekebisho waruhusiwe kuagiza.
Hawa Ally, mwakilishi kutoka TCCA alisema wakala wadogo kwenye sheria mpya wameongezewa malipo ya ukataji leseni na itakuwa vigumu kupata leseni mpya inapoisha muda wake.
“Changamoto yetu kubwa ni kuongezwa kwa malipo ya kukata leseni sisi wakala wadogo tutapata ugumu wa kupata leseni mpya” alisema Hawa.
No comments:
Post a Comment