Mwili wa mfanyabiashara huyo uliokutwa ukiwa umefungwa kwenye viroba ukielea ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda mkoa wa Mara na Busega mkoani Simiyu umewasili asubuhi ya leo Machi 16 ukitokea Hospitali ya Rufaa Mara ulikohifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi tangu juzi.
Tangu asubuhi, mamia ya waombolezaji kutoka jijini Mwanza na maeneo jirani wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa marehemu wakitumia mabasi ya kampuni aliyokuwa akimiliki.
Mabasi ya kampuni nyingine pia yanatumika kusafirisha waombolezaji kutoka jijini Mwanza bila malipo.
Marehemu Josia aliyezaliwa mwaka 1968 alipotea tangu Februari 27 kabla ya gari lake kukutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara Machi 9.
Ibada ya mazishi inaongozwa na Mchungaji Jackson Meza kutoka Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) huku kwaya ya kanisa ambayo marehemu alikuwa mfadhili wake ikiimba nyimbo za maombolezo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed, watu wanne wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho kilichoibua hofu na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa jiji la Mwanza ambako marehemu alikuwa akiendesha shughuli zake za kibiashara.
No comments:
Post a Comment