Friday, March 16

Viongozi watano Chadema washindwa kufika polisi


Viongozi wawili wa Chadema leo Machi 16 wamewasili kituo kikuu cha polisi na wengine watano kushindwa kufika.
Viongozi waliowasili ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mboe na Naibu katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu.
Machi 13 Katibu Mkuu, Dk Vicenti Mashinji na Naibu Salum Mwalimu walifika wakati viongozi wengine watano ambao ni wabunge walishindwa kufika kutokana na kuwapo Dodoma kwenye vikao vya kamati za kudumu za bunge.
Wakili Alex Massaba amesema viongozi walioshindwa kufika ni wabunge na Katibu Mkuu  ni kiongozi wa chama.
"Tumekuja kuripoti kama tulivyoambiwa ila kama mnavyojua kamati zinaendele na vikao waliobaki ni wabunge na katibu mkuu yuko kwenye majukumu mengine," amesema Massaba.
Ameongeza kuwa tarehe 26 itakuwa ni mara ya mwisho kufika kituoni hapo kwani viongozi wote walishahojiwa na kama mashtaka yao yanafaa kuwafikisha mahakamani ni vyema wangepelekwa.
Mbali na katibu mkuu Mashinji wengine ambao hawakufika ni naibu katibu mkuu bara John Mnyika, mwenyekiti wa wanawake Halima Mdee, mwenyekiti wa kanda ya Serengeti, John Heche na mweka hazina wa kanda hiyo Ester Matiko.
Viongozi hao wametakiwa kufika tena kituoni hapo siku ya Alhamisi Machi 22 saa mbili asubuhi.
Viongozi hao walipokea wito Februari 20 na jeshi la polisi likiwataka kufika kituoni hapo baada ya maandamano ya Februari 16 walipokuwa wakielekea kudai viapo kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi ambapo Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwilini alifariki dunia akiwa kwenye daladala kwa kupigwa risasi eneo la Mkwajuni, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment