Baada ya Mwigamba Jumatatu, Oktoba 16,2017 kuandika barua ya kujizulu uongozi na kueleza atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa ACT Wazalendo, chama hicho kilipanga kukutana Ijumaa Oktoba 20, 2017 kujadili masuala kadhaa, likiwemo la kujizulu kwake.
Hata hivyo, leo Oktoba 19,2017 Mwigamba katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ametangaza kujivua uanachama wa ACT Wazalendo na kujiunga na CCM.
Mwigamba amesema baada ya kutafakari kwa kina ameamua pamoja na wanachama wengine 10 kukihama chama hicho.
Amezitaja sababu za kuhamia CCM kuwa ndicho chama kinachoakisi kwa karibu itikadi, falsafa na sera za ACT Wazalendo.
Amesema wanasukumwa na kufuata misingi ya azimio la Tabora ambayo kwa kiasi kikubwa CCM inalitekeleza. Pia, wamefanya hivyo ili kujiunga katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mwigamba ametaja sababu nyingine ni kujitenga na upinzani unaokerwa na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.
"Baada ya kutangaza kujivua uongozi baadhi ya viongozi wa ndani ya chama waligeuka vichaa wakinitukana kila aina ya matusi. Cha ajabu hata wale wanaofahamu na kuitetea misingi ya chama walitukanwa na viongozi wakiwepo na wamekaa kimya, hii inaonyesha wamewatuma," amesema Mwigamba.
No comments:
Post a Comment