Maelfu ya watu wameandamana katika mitaa ya Barcelona, Uhispania, baada ya mahakama nchini humo kuamuru viongozi wawili wa jimbo la Catalonia lenye utawala wa ndani kutiwa mbaroni. Catalonia yataka kujitenga.
Msemaji wa mji wa Barcelona amesema kiasi ya waandamanaji 200,000 waliokuwa wameshika mishumaa mikononi mwao walisikika wakipaza sauti za kudai uhuru kabla ya kukaa kimya kwa dakika chache. Maandamano mengine ya watu waliokuwa wameshika mishumaa mikononi yalifanyika katika miji mingine ya jimbo la Catalonia kupinga kushikiliwa kwa viongozi wawili wa jimbo hilo ambao ni Jordi Cuixart na Jordi Sanchez wanaotuhumiwa kwa makosa ya uchochezi.
Mmmoja wa waandamanaji aliyefahamika kwa jina la Elias Houriz alisikika akisema " Wanataka tuogope ili tusifikirie juu ya uhuru wetu lakini hiyo itakuwa ni kinyume chake kwani tunazidi kuwa na mwamuko kadiri siku zinavyosonga na mwishoni tutafikia lengo letu" mwisho wa kumnukuu.
Naye kocha wa kilabu ya Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya England, Pep Guardiola anayetokea pia katika jimbo la Catalonia alisema ushindi wa timu yake hapo jana dhidi ya Napoli hapo jana usiku katika michuano ya kilabu bingwa barani Ulaya ameutoa maalumu kama ishara ya kuwaunga mkono viongozi wawili waliotiwa mbaroni na kutaka waachiwe huru haraka. Guadiola ambaye amewahi kuinoa kilabu ya Barcelona alisema utaifa ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Maandamano hayo ya jana yamefanyika huku muda ukizidi kukaribia kabla ya hapo kesho Alhamisi ambayo ni tarehe iliyowekwa na serikali kuu ya mjini Madrid inayomtaka kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont kutamka wazi iwapo anakusudia au kutokusudia kutangaza rasmi uhuru wa jimbo la Catalonia kufuatia kura ya maoni iliyofanyika Oktoba 1 ambayo ilipigwa marufuku na serikali ya mjini Madrid kwa maelezo kuwa ni kinyume cha katiba.
Puigbemont ataka majadiliano na Waziri Mkuu Mariano Rajoy
Hata hivyo kiongozi huyo amekataa hadi sasa kuitikia mwito huo akimtaka Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy kukaa naye pamoja katika meza ya majadiliano jambo ambalo Rajoy hakubaliani nalo hali ambayo inaweza kuzidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipojikomboa kutoka katika utawala wa kiimla mwaka 1977.
Hayo yanajiri huku pia wabunge 50 katika bunge la nchi hiyo wakiwemo wanaotoka katika jimbo la Catalonia wakibeba mabango ndani ya bunge hilo kushinikiza kuachiwa huru viongozi waliotiwa mbaroni wakiwataja kuwa ni wafungwa wa kisiasa.
Wakati huohuo sekta ya utalii ambayo ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hiyo inaonekana kuathirika kutokana na kukosekana kwa uthabiti tangu kufanyika kura hiyo ya maoni hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mariano Rajoy wakati alipolihutubia bunge la nchi hiyo akitetea hatua ya serikali yake inayochukua katika kushughulikia mgogoro huo.
Mji wa Barcelona ambao ni mji mkuu wa Catalonia ni moja ya miji ambayo inatembelewa na watalii wengi nchini humo kila mwaka.
No comments:
Post a Comment