Thursday, August 3

Kodi ya Acacia yapungua asilimia 45


Kodi ya huduma inayotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Acacia Bulyanhulu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita imepungua kwa zaidi ya asilimia 45 kutokana na Serikali kuzuia usafirishaji wa mchanga (makinikia) kwenda nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Carlos, Gwamagobe amesema kupungua kwa mapato yatolewayo na Acacia itaathiri bajeti kwasababu  wanategemea mwaka wa fedha 2017/18 kukusanya zaidi ya Sh800 milioni kama kodi ya huduma kutoka katika mgodi huo.
“Kushuka kwa mapato haya yataathiri bajeti yetu kwakuwa kuna miradi haitatekelezwa mwaka jana tulizielekeza kwenye sekta ya elimu sasa inabidi juhudi za makusudi zifanyike fedha hizi zilikua zikitusaidia sana kwenye miradi ya maendeleo na miradi ya kijamii,”amesema Gwamagobe.

Amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kujenga madarasa 12 ya shule ya msingi, manane ya shule za sekondari na kujenga hosteli ya Shule ya Sekondari Kakola pamoja na kujenga ghala la kuhifadhia chakula.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Hamimu Buyama amesema kodi ya huduma inayotolewa na Acacia imesadia kusukuma maendeleo ya halmashauri hiyo na kusema katika maendeleo lazima ziwepo changamoto kama zilivyowakuta Acacia sasa.

Amesema suala la makinikia limekua kikwazo kwa kampuni lakini pia kwa halmashauri zinazotegemea kodi ya huduma kutokana na mapato kushuka na kusema anaimani suala hilo litafika mwisho mwema na wao kuendelea kufanya kazi kama ilivyokuwa awali.

Akikabidhi hundi kwa uongozi wa Wilaya ya Nyang’wale Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu, Grahama Crew amesema kwa kipindi cha miezi sita iliyopita  kodi ya ushuru wa huduma ni zaidi ya Sh687 milion ambazo zimegawanya katika Halmashauri ya Msalala iliyopata asilimia 67 na Nyang’wale iliyopata asilimia 33.

Amesema kuanzia mwaka 2000 hadi sasa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu umelipa zaidi ya Sh10.2 bilioni kama kodi ya huduma katika maeneo wanayofanya kazi ambapo amesema ni matarajio yao kuendelea kuimarisha sekta ya viwanda kwenye uchimbaji wa madini katika Wilaya ya Nyang’wale.

Akizungumza katika makabidhiano hayo mbunge wa Nyang’wale, Hussein Nassoro amesema wananchi wa Nyang’wale wanauhusiano mzuri na kampuni, lakini bado wanamahitaji makubwa.

Amesema wilaya hiyo bado iko nyuma katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara na kuiomba kampuni hiyo kuendelea kuisaidia huduma za kijamii kwa wananchi ili waweze kuona faida ya uwekezaji katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment