Thursday, August 3

JPM ameiagiza JKT kurejesha ardhi kwa wanakijiji baada ya kushindwa kuiendeleza


Rais John Magufuli ameagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kurejesha eneo la eka 50 walilopewa na Kijiji cha Mkata, baada ya kushindwa kuliendeleza kwa miaka saba.
Rais ameagiza hatua hiyo ichukuliwe leo Alhamisi, Agosti 3 wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkata akiwa njiani kuelekea mkoani Tanga, ambapo alimwita Mkuu wa JKT wa eneo hilo na kumhoji kuhusu kuendeleza eneo hilo.
“Hili eneo tangu mmepewa ni miaka mingapi sasa? Mliomba ili mjenge muwekeze kwa kujenga kiwanda, lakini mmeshindwa sasa leo hii mrejeshe kwa wananchi ili waweze kumpa hata mwekezaji mwingine,” ameagiza Rais Magufuli na kushangiliwa na wananchi.
Amemweleza mkuu huyo wa JKT kwamba wakajenge kiwanda hicho kwenye kambi yao kwa kuwa wana eneo kubwa ambalo linatosha pia kwa uwekezaji huo.
Awali aliwataka wananchi hao kuwa na subira kuhusu ujenzi wa hospitali katika eneo hilo, kwa kuwa kuna shaka kwamba Sh500 milioni zilizotolewa kwa awamu ya kwanza zilitafunwa, hivyo kabla ya kuleta nyingine wanapaswa kujiridhisha na matumizi yaliyofanywa.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipopewa nafasi ya kulitolea ufafanuzi jambo hilo amesema wanaunda kamati ambayo itachunguza matumizi ya fedha hizo ndipo waweze kuruhusu fedha zingine zipelekwe ili kuendeleza mradi huo.
Rais Magufuli yupo safarini ambapo Agosti 5 atakutana na Rais Yoweri Kaguta Museveni  kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa bomba la kusafirisha mafuta Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

No comments:

Post a Comment