Tuesday, March 6

Madiwani Chadema kujiunga CCM kwaibua utata

Serengeti. Wakati madiwani wawili wa Chadema kutoka halmashauri ya wilaya ya Serengeti wakitangaza kujivua uanachama na nyadhifa zao kuunga mkono kazi inayofanywa na Serikali, uongozi wa halmashauri hiyo inayoongozwa na chama hicho umesema haujapokea taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo.
Madiwani waliotangaza kuondoka Chadema na kujivua nyadhifa zao kupitia taarifa zinazosambaa kupitia mitandao ya kijamii ni Michael Kunani wa kata ya Ikoma na John Mongita ambaye ni diwani wa kata ya Manchira.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Dk Tito Kagize alisema hajapata taarifa  rasmi zaidi ya kusoma kwenye mitandao
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa ya simu leo Machi 6, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti Juma Porini na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk Tito Kagize wamesema nao wamesikia, kusoma na kuona taarifa za madiwani kutangaza kujiuzulu kupitia mitandao ya kijamii.
“Tunajua wako mkoani Arusha kwa muda mrefu wakijadiliana na viongozi wa CCM wa Kitaifa wanaofanya ziara mkoani humo kuhusu wao kujivua uanachama na kujiuzulu udiwani; tunasubiri taarifa yao rasmi,” amesema Porini.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya inayoongozwa na Chadema amesema ni hiari na haki ya kikatiba na kisheria kwa kila mtu kujiunga na chama chochote cha siasa na kuongeza kuwa wakipokea taarifa rasmi chama kitaheshimu uamuzi wa madiwani hao.
“Taarifa za wao kuondoka Chadema na kuhamia CCM zilisikika hata wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Serengeti mwezi uliopita; nadhani walikuwa hawajafikia makubaliano ndio maana hawakufanya hivyo wakati ule,” amesema Porini.
Amesema kwa muda sasa, madiwani hao hawahudhurii vikao kikiwemo kile cha kujadili na kupitisha bajeti cha wiki iliyopita.
Halmashauri ya wilaya ya Serengeti yenye jumla ya madiwani 43, inaongozwa na Chadema yenye madiwani 25 na wabunge wawili inayofanya idadi yao kufikia 27 huku CCM ikiwa na madiwani 16.

No comments:

Post a Comment