Friday, July 28

TIMU YA RIADHA CHINI YA MIAKA 17 YAREJEA NCHINI NA MEDALI YA SHABA

Na Shamimu Nyaki –WHUSM
Timu ya riadha ya vijana chini ya miaka 17 imeleta heshima kubwa kwa nchi yetu baada ya kurejea na medali ya shaba aliyoshinda kijana Francis Damasi katika  mbio za mita 3000 kwenye mashindano ya  Jumiya ya Madola yaliyomalizika hivi  karibuni huko nchini India.
Medali ya shaba katika mahindano ya riadha  iliyoletwa na kijana Francis imerejea tena baada ya miaka 19 tangu Tanzania ilivoshinda medali hiyo mwaka 2008 katika michezo hiyo.
Timu hiyo iliyorejea nchini leo imepokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel katika uwanja wa  ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo  ameeleza kufurahishwa na matokeo hayo mazuri waliyopata wanariadha hao ambao wameitangaza vyema Tanzania.
“Vijana mmefanya vizuri sana katika mashindano haya Serikali tunawapongeza sana  kwa kuitangaza nchi yetu lakini pia kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika mashindano haya nawaahidi kuendelea kushirikiana na uongozi na wadau wa riadha nchini ili tufike mbali zaidi” Alisema Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha riadha nchini Bw. Filbert Bayi  amesema kuwa mchezo wa riadha kwa sasa ni mchezo ambao umeitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa kutokana na kushiriki  mashindano mengi ya Kimataifa hivyo ni vyema wadau wakajitokeza kwa wingi kuwekeza katika mchezo huo ambao umeendelea kuletea heshima Taifa.
“Riadha imeitangaza Tanzania na itaendelea kuitangaza hivyo wadau wanapaswa kuona fursa hii na kuwekeza katika mchezo huu ili ufike mbali,kila mtu katika eneo lake aone fursa hii na aitumie kwa manufaa ya kizazi hiki na kitakachokuja” Alisema Bw. Bayi.
Naye Kijana Francis Damian aliyepata medali hiyo baada kushinda mbio za mita 3000 ameeleza kufurahishwa na ushindi huo kwani alijiandaa na alizingatia maelekezo ya walimu wake yaliyompelekea kupata ushindi huo na ameshauri vijana kama yeye kuthubutu na kuamini kuwa wanaweza kwani mchezo huo ni mzuri na una mafanikio makubwa.

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akimpongeza mwanariadha Francis Damas leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kupata ushindi wa medali ya shaba baada ya kushinda mbio za mita 3000 katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas
 Katibu Mkuu chama cha Riadha nchini Bw. Filbert Bayi (aliyesimama) akizungumza  na wanariadha na wadau wa mchezo huo mara baada ya timu ya riadha ya vijana chini ya miaka 17 kurejea nchini na medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyoalizika hivi karibuni huko Bahamas.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akipokea Bendera ya Tanzania kutoka kwa  mwanariadha  Regina Mpigachai mara baada ya kurejea nchini na ushindi wa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas.Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya michezo wa Wizara hiyo Bw. Alex Nkenyenge.
Mkuu wa Msafara na mwalimu wa wanariadha Bibi Mwinga Mwanjala akitoa neno la shukrani  mara baada ya kurejea nchini na  ushindi wa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas.

No comments:

Post a Comment