Wakati katibu huyo wa CUF akisema uamuzi huo ulifanywa kwa kupata maelekezo ya “mabosi” bila ya kufuata ushauri wa kitaalamu wa wanasheria waliokutana mjini Dodoma juzi, wabunge wanane wanawake na madiwani wawili waliotimuliwa, jana walifungua kesi mahakamani wakiitaka isitishe uamuzi wa Baraza Kuu la upande wa Profesa Ibrahim Lipumba wa kuwavua uanachama.
Kabla ya wabunge hao kufika mahakamani, Lipumba alikutana na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa kamati ya maadili itaendelea kuwaita wabunge wanaotuhumiwa kwa utovu wa nidhamu, pamoja na Maalim Seif kwa ajili ya kuwahoji na wakikutwa na makosa wataadhibiwa.
Siku ya jana ilianza kwa Profesa Lipumba, ambaye alijivua uenyekiti na nyadhifa nyingine zote mwaka 2015 kabla ya kufuta uamuzi huo mwaka mmoja baadaye, kufanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba alielezea hatua walizochukua na wanazotarajia kuchukua dhidi ya wanachama wao, akisema hata katibu huyo mkuu ataitwa na kamati hiyo kuhojiwa.
Baadaye, ilifuata taarifa ya NEC iliyotaja majina ya wanachama wa CUF watakaoshika nafasi zilioachwa na wabunge waliotimuliwa uanachama.
Taarifa iliyofuata ilikuwa ya Maalim Seif aliyesema kitendo cha kuwafukuza uanachama wabunge halali wa CUF, kingekuwa sahihi kama kingefuata taratibu zote za kisheria na kikanuni za Bunge kujiridhisha kwanza.
Taarifa hiyo ilijaa tuhuma dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa, wakuu wa wilaya, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, NEC, Jeshi la Polisi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), akisema taasisi hizo zinashiriki kutaka kuiua CUF.
“Polisi ndiyo waliomuingiza kwa nguvu na kumlinda (neno tumeliondoa) Ibrahim Lipumba katika Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CUF uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza siku ya tarehe 21 Agosti, 2016 kwa lengo la kuuvuruga,” inasema taarifa ya Maalim Seif.
“Polisi pia wakamuongoza na kumlinda Lipumba na genge lake kwenda kuvamia na kuvunja Ofisi Kuu ya chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, siku ya tarehe 23 Septemba, 2016.”
Kuhusu tuhuma dhidi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Maalim Seif anasema “Ilijitwisha uwezo na madaraka (ambao Mahakama Kuu ya Tanzania ilishawahi kutamka kwamba haina) ya kutengua uamuzi wa vikao halali vya chama ambavyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Taifa uliokubali barua ya Ibrahim Lipumba kujiuzulu Uenyekiti wa Chama; na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo lilimfukuza uanachama Ibrahim Lipumba na kuwasimamisha uanachama waliokuwa viongozi wengine kadhaa wa chama”.
Pia, ameituhumu Rita kuwa imekubali kuvunja Sheria ya Wadhamini huku ikijua na ikiwa na taarifa zote ilizopewa na CUF kwa barua ya Juni 17, kwa kusajili wajumbe wasio sahihi wa Bodi ya Wadhamini.
Alisema Rita imefanya hivyo, “Ili waweze kutumika kufuta kesi ambazo chama kimezifungua Mahakama Kuu kupinga hujuma hizi zinazoendelea na pia kuweza kufanikisha kuchota fedha za ruzuku ya chama zilizobakia ambazo zimezuiwa kutolewa kupitia zuio la Mahakama Kuu”.
Kuhusu Ofisi ya Spika, Maalim Seif amesema kitendo cha Spika Ndugai kukubali haraka kufukuzwa uanachama kwa wabunge wanane wa chama hicho, “Ni msimamo kutoka juu kwamba wabunge wa CUF wafukuzwe”.
Anasema katika taarifa hiyo kwamba suala hilo limefanyika mara nyingi tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporejeshwa nchini mwaka 1992. Hata hivyo, anahoji kwa nini mara hii Spika ameridhia haraka uamuzi huo ikiwa haijazidi hata siku moja na hata bila ya kuwasiliana na katibu mkuu wa CUF ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF, ndiye mtendaji mkuu wa chama.
“Lakini kama hiyo haitoshi, nilimuandikia rasmi barua Spika Ndugai, Julai 25, 2017 nikimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu,” anasema Maalim Seif.
“Angekuwa na nia ya kweli ya kutaka kujiridhisha, hapo ndipo pangekuwa pa kuanzia kwa kuwepo kile wanasheria wanachokiita shaka inayoweza kuingia akilini yaani ‘reasonable doubt’.”
Maalim Seif anadai Spika Ndugai amepuuza yote hayo kwa sababu ni kinyume na mkakati wa dola kuihujumu CUF na kuua upinzani nchini.
“Kwa kifupi, yanayofanyika ni mchezo wa kuigiza tu, lakini maamuzi yameshafanywa na Dola na waliobaki wanatekeleza tu,” anasema Maalim Seif.
Anadai kuwa Julai 26 kulikuwa na kikao cha wanasheria wapatao 12 wa Serikali kutoka Bunge, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, NEC na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambao walitakiwa kumshauri Spika kwa kumuandikia maoni ya kisheria kuhusu suala la wabunge wa CUF.
Anasema wanasheria hao walishauri kuwa Bunge lisiingilie mgogoro wa chama ambao tayari uko Mahakamani kwa kukubali uamuzi wa upande mmoja kuwafukuza wabunge wakisema kitendo hicho kitashusha hadhi ya Bunge, kuifedhehesha NEC na kuitia aibu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo ina jukumu la kuishauri Serikali.
“Walipoambiwa waeleze maelekezo ya mabosi wao, wote walieleza kuwa wametakiwa kufuata msimamo wa kutoka juu kwamba wabunge wa CUF wafukuzwe, isipokuwa wanasheria wa Bunge tu ndiyo ambao hawakuwa na maelekezo hayo,” amedai Maalim Seif.
“Baada ya hatua ya jana ya Spika Ndugai, na kwa utaratibu huohuo wa mwendokasi, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshapewa maelekezo na leo au kesho watatekeleza maelekezo hayo kwa kutangaza majina ya watakaowaita ‘wabunge wapya’ wa kujaza nafasi hizo. Bila shaka ilivyokuwa Dola imeshaamua hivyo, basi taasisi zote hizo zitaendelea kutekeleza mpango huo.”
Hata hivyo, Maalim Seif amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kuendelea kuwa watulivu na kusubiri uamuzi wa Baraza Kuu ambalo linakutana leo mjini Zanzibar.
“CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi katika historia yake tokea ilipoasisiwa mwaka 1992. Tulishinda dhoruba na misukosuko hiyo na tutaushinda huu uliopo na hatimaye kuibuka tukiwa imara zaidi,” anasema Maalim Seif.
Kaimu Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alisema hawezi kuzungumzia suala hilo bila ridhaa ya Spika, huku kaimu katibu wa Spika, Athuman Kwikwima akisema Ndugai na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila wapo nje ya nchi kikazi.
Lipumba kuita wabunge wengine
Mapema jana, Profesa Lipumba, ambaye anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kamati ya nidhamu na maadili ya chama hicho, ipo katika mchakato kuwaita wabunge na viongozi akiwamo Maalim Seif kwa ajili ya mahojiano dhidi ya tuhuma za kuihujumu CUF.
Alisema awamu ya kwanza imekamilika ya kuwaita wabunge 10 na madiwani wawili wa viti maalumu kwa ajili ya mahojiano ambao hata hivyo, hawakutokea na Baraza Kuu la Uongozi Taifa kuazimia kuwafukuza uanachama wabunge wanane kati ya hao.
Mbali na hilo, mchumi huyo alisema nafasi za wabunge hao wanane zitajazwa wakati wowote baada ya Spika Ndugai kuridhia maombi yao na kwamba hawajapeleka majina mapya NEC, bali yatatumika yaliyo katika orodha iliyopelekwa mwaka 2015.
“Ngwe ya pili inakuja, kamati ya maadili ilianza kwa wabunge 10 na madiwani iliowafanyia uchunguzi na ulipokamilika Baraza Kuu la Taifa la Uongozi likafanya uamuzi. Sasa kamati hii inaendelea na awamu ya pili,” alisema.
“Kati ya watu watakaoitwa ni Maalim Seif, Naibu Katibu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, wabunge na wanachama wengine wenye makaosa kama haya.”
Alisisitiza kuwa Maalim Seif lazima ataitwa katika kamati hiyo kwa madai ya kwamba ni miongoni mwa watu waliowaponza wabunge hao wanane.
“Wabunge wengine nawaambia msiwe mnafuata kila anachokisema huyu bwana (Maalim Seif). Si kila anachosema, unakifuata kwa sababu unaogopa, atawaponza kama alivyowaponza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyewazuia wasiende mahakamani kudai haki yao,” alisema.
Kuhusu majina kupelekwa NEC, Profesa Lipumba alisema mchakato wa kutafuta majina mapya utachukua muda mrefu hivyo wamekubaliana kwamba wabunge hao wapya watateuliwa kulingana na orodha iliyowasilishwa na chama hicho mwaka juzi.
“Jamani majina yaliyopelekwa ni mengi atakayekosa naomba asikate tamaa asubiri wakati mwingine,” alisema Profesa.
Pamoja na hayo, Profesa Lipumba alidai kuwa kikao kitakachofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa hajapewa taarifa.
Akizungumzia uteuzi huo, mkurugenzi wa uchaguzi wa upande wa Maalim Seif, Shaweji Mketo alisema majina hayo ni sahihi yaliyopelekwa mwaka juzi, lakini utaratibu haukufuatwa.
“Kulingana na utaratibu, nilitegemea Kuruthumu Mchuchuri angeteuliwa katika mchakato huu kwa kuwa jina lake lilikuwa namba 11, lakini wameamua kudonoa donoa na kuwachagua wajumbe wanaowataka wao,” alisema Mketo.
Mketo alidai mchakato huo umefanyika kwa upendeleo wa watu wanaoumuunga mkono Profesa Lipumba na undugu huku akitolea mfano wa jina la Shamsia Aziz Mtamba, akisema ni ndugu na mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma.
Watinga mahakamani
Sakata hilo liliendelea alasiri wakati wabunge wanane waliosimamishwa na upande wa Lipumba walipofungua kesi Mahakama Kuu kuomba ibatilishe uamuzi huo.
Wakiwakilishwa na wakili Peter Kibatala, wamefungua maombi hayo kwa hati ya dharura wakitaka Mahakama Kuu isimamishe utekelezaji wa uamuzi uliowavua uanachama kwa muda kusubiri uamuzi wa kesi yao ya msingi.
Katika kesi hiyo namba 143/2017, wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CUF, mwenyekiti na kaimu katibu mkuu wa chama hicho.
Wadai wanaiomba mahakama itamke kuwa uamuzi wa kuwavua uanachama na hivyo kupoteza nafasi zao, kuwa ni batili kwa kuwa haujazingatia kanuni za haki za msingi.
Pia, wanaiomba mahakama itamke kuwa mchakato wa kuwashughulikia kinidhamu uliohitimishwa kwa kuwavua uanachama, ni batili kwa kuwa unakiuka kanuni na kisheria.
Wanadai hawakupewa fursa ya kutosha kujitetea kwa kuwa taarifa kamili haikutolewa kwao kuhusu tuhuma dhidi yao na wameadhibiwa licha ya kuwa walishakata rufaa Mkutano Mkuu. Adhabu waliyopewa wanadai ni kubwa mno kulinganisha na makosa wanayotuhumiwa na kwamba, uamuzi umechukuliwa bila kuzingatia hasara si tu watakayoipata wao, bali kwa chama na uchumi wa nchi katika mchakato wa kujaza nafasi hizo.
Waliotimuliwa walonga
Wabunge waliovuliwa uanachama waliilaumu Serikali kwa uamuzi huo.
Akizungumzia kufukuzwa kwao, mmoja wa wabunge hao, Riziki Shahali Mngwali alisema kinachoendelea ni mchezo unaofanywa na dola na siyo uamuzi wa Spika Ndugai peke yake au Profesa Lipumba.
Alisema ni wazi kwamba Serikali imekuwa ikimtumia Profesa Lipumba kukigawa chama hicho ili kukipunguza nguvu. Alisema baadhi ya matukio ambayo yanadhihirisha Profesa Lipumba kuungwa mkono na Serikali kuwa ni kuvamia Mkutano Mkuu wa mwaka 2016 akiwa na askari wa Jeshi la Polisi.
“Sisi hatuna nguvu za kupambana nao. Mimi binafsi, I am very disappointed (nimevunjika sana moyo). Sikutarajia kama tunaweza kuwa na dola ya namna hii,” alisema Mngwali na kusisitiza kwamba wataendelea kupigania haki hata wakiwa nje ya Bunge.
Nyongeza na James Magai
No comments:
Post a Comment