Saturday, May 16

Mashine ya kupima virusi vya corona iliyotolewa na Rostam yawasili Zanzibar



MASHINE ya kupima virusi vya corona yenye uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa nane ambayo iliagizwa nchini Korea Kusini kwa ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, hatimaye imewasili visiwani humo.
Mashine hiyo ina uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa nane kwa vipimo vya watu 96 na kwa saa 24 ina uwezo wa kutoa majibu kwa watu 496.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Zanzibar, Juma Mohammed Salum jana ilieleza kuwa mashine hiyo ni miongoni wa tatu zilizokuwa zimeagizwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Itakumbukwa Machi 25 Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein aliiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha ndani ya miezi mitatu wanakamilisha maabara ya kupima magonjwa ya mripuko.
Shein alikuwa amefanya ziara ya kuangalia ujenzi wa Maabara ya Uchunguzi ya Microbiology katika kijiji cha Binguni na kuagiza Wizara ya Afya kuanza mara moja ujenzi wa maabara itakayochunguza maradhi yanayosababishwa na virusi (Virology Laboratory).
Zaidi alitaka ujenzi wa maabara hiyo ukamilike haraka iwezekanavyo ili Zanzibar iweze kuwa na mashine za kupima virusi vya corona.

No comments:

Post a Comment