Tuesday, March 22

Pengo la CUF lajitokeza wazi Pemba

https://youtu.be/LCY1dmtFE1E
Pemba. Kitendo cha CUF kususia uchaguzi kimeelezwa kuwa kwa kiwango kikubwa kimesababisha watu wachache kujitokeza katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.
Wasimamizi wa vituo vya uchaguzi, wapigakura, ambao hawakupiga kura na baadhi ya viongozi waliozungumza na gazeti hili kisiwani Pemba walisema pamoja na mambo mengine, kitendo cha CUF kutoshiriki uchaguzi huo kimechangia hali hiyo.
Uchaguzi huo wa marudio umefanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya udiwani, uwakilishi na urais Oktoba 28 mwaka jana kwa maelezo kuwa ulikuwa na kasoro nyingi.
Mwandishi wetu alitembelea vituo zaidi ya 10 katika mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba na kukuta idadi ndogo ya wapigakura, jambo ambalo liliwafanya wasimamizi wa vituo hivyo kutumia muda mwingi kupiga stori.
Mbali na wasimamizi hao, hata mawakala wa vyama waliokuwapo katika vituo hivyo wengi walikuwa wa CCM na wachache wa ADC na Tadea, tofauti na idadi ya vyama vilivyotangazwa kushiriki uchaguzi huo.
Pemba kuna vituo vya uchaguzi 463 na kila kimoja kilipaswa kuwa na wapigakura takribani 1,000 hadi 3,500, lakini mpaka kufikia jana saa sita mchana vingi vilikuwa tupu huku wasimamizi wakikiri kuwa idadi ya waliojitokeza ni ndogo.
Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Wawi A, Kusini Pemba, Ismail Issa Juma alisema jambo pekee lililojitokeza katika kituo hicho ni idadi ndogo ya wapigakura.
Alisema kituo hicho kina wapigakura 1,400 na waliokuwa wamejitokeza mpaka kufikia saa nne asubuhi walikuwa hawajafika robo ya idadi hiyo.
Mgombea urais kwa tiketi ya ADC, Hamad Rashid Mohamed ambaye alipiga kura katika kituo hicho alisema kutoshiriki kwa CUF ni sababu ya wananchi kutojitokeza.
“Hapa Pemba CUF wana nguvu. Hii ni ngome yao, hivyo usitegemee kuona watu wengi hapa ila binafsi ninaamini asilimia 40 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura watajitokeza leo (jana) kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema Hamad ambaye alivuliwa uanachama wa CUF na kuanzisha ADC.
Alisema anaamini atashinda urais katika uchaguzi huo kutokana na CUF kujitoa, huku akisisitiza kuwa kasoro zilizopo ZEC na Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ), zitamalizwa likipatikana baraza la wawakilishi na rais na si kususia uchaguzi.
Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Wawi B ambacho mgombea urais wa AFP, Said Sudi Said alipiga kura, Mussa Abdallah Kilindo alisema si rahisi wapigakura 950 katika kituo hicho wote wakapiga kura.
Mkazi wa Wawi, Omar Mohammed Hassan alisema idadi ya watu waliojitokeza ina tofauti kubwa na ya uchaguzi wa Oktoba 25 kauli ambayo iliungwa mkono na mkazi mwingine wa eneo hilo, Mafunda Abdalla.
Hali ilikuwa tofauti zaidi katika vituo vya kupigia kura vilivyopo Wilaya ya Wet, Kaskazini Pemba ambako pia kunatajwa kuwa ngome ya CUF kutokana na kujitokeza kwa watu wachache zaidi.
Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya wasimamizi wa vituo hivyo wakiwa wamelala katika madawati wakisubiri wapigakura ambao walikuwa wakifika mmojammoja.
“Kama unavyoona shughuli ya kupigakura inaendelea vyema kabisa na kuna usalama wa kutosha. Watu wanakuja ila si wengi kama ilivyokuwa Oktoba 25. Kituo hiki kina wapigakura 1,950,” alisema Maalim Haji, msimamizi wa uchaguzi Kituo cha Shule ya Msingi Kizimbani.
Mkazi wa Kizimbani, Sada Hamad Shamata aliyekutwa akipiga kura katika kituo hicho alisema: “Uchaguzi umekwenda vyema na hakuna usumbufu wala kusukumana maana watu ni wachache tofauti na uchaguzi uliopita.”
Mkazi mwingine wa Kizimbani, Ali Juma Fakih alisema: “Hilo siyo swali sheikh ni jibu. CUF kususia uchaguzi huu ndiyo sababu ya wapigakura kuwa wachache.”
Mkuu wa wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid aliyekuwa akizunguka vituo vyote vya uchaguzi vilivyopo katika wilaya hiyo alisema ni kawaida uchaguzi wa marudio kujitokeza watu wachache.
“Pemba CUF wapo wengi hilo lipo wazi ila binafsi kama mkuu wa wilaya nina jukumu la kuhakikisha hali ya usalama inakuwa shwari,” alisema Rashid.
Katika Kituo cha Ukunjwi, Jimbo la Gando, Kaskazini Pemba mwandishi wetu alishuhudia wapigakura watatu waliojitokeza baada ya kukaa hapo kwa nusu saa.
Katika kituo hicho baadhi ya majina ya wapigakura yaliyobandikwa ukutani yalikuwa yamechanwa hivyo kuwapa wakati mgumu waliofika kupigakura.

No comments:

Post a Comment