Habari za Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (VVU), kodi na manunuzi ya umma, habari za uchambuzi na matukio na kundi la Afya ya Uzazi kwa Vijana, zimeondolewa katika makundi yatakayowania Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari(EJAT) kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo rasilimali fedha.
Tuzo hizo zimezinduliwa rasmi leo ambapo makundi makundi matano kati ya 19, yamepunguzwa kutokana na sababu hizo.
Mwenyekiti wa maandalizi ya tuzo hizo zinazosimamiwa na Baraza la Habari nchini (MCT), Kajubi Mukajanga amesema mwaka huu kutakuwa na ushindani wa umahiri wa habari katika makundi 14 kati ya 19 yaliyokuwa yakishindaniwa mwaka jana.
Amevitaja vipengele vilivyobaki katika tuzo hizo ni habari za afya, habari za michezo na utamaduni, habari za uchumi, biashara na fedha, na uandishi wa habari za biashara, kilimo, elimu, utalii na uhifadhi, uchunguzi, data, haki za binadamu na utawala bora, mpiga picha bora wa magazeti na runinga, mchoraji katuni bora, habari za jinsia, wazee na watoto na kundi la wazi.
“Kazi zitakazoshindanishwa ni zile zilizochapishwa na kutangazwa kati ya Januari Mosi hadi Desemba 31 mwaka huu, na mwisho wa kuwasilisha kazi zao ni Februari 16, mwakani na tuzo hizi zitatolewa Aprili 27, mwakani,” amesema.
No comments:
Post a Comment