Wednesday, April 4

Radi zinavyozitikisa shule Kagera



Tangu tukio la mwaka 2005 lililosababisha vifo vya wanafunzi wawili na majeruhi, radi imetikisa tena shule ya msingi Kyakailabwa iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Katika tukio hilo la miaka 12 iliyopita lililoshuhudiwa na walimu na wanafunzi, pia mwanamke mmoja alifariki na maajabu makubwa zaidi siku hiyo ni jinsi mtoto wake mchanga alivyonusurika.
Aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati huo Jacob Kaijage, anasema alishuhudia matukio hayo na jinsi mamia ya wananchi walivyokusanyika kushuhudia janga hilo.
Radi iliyojirudia Machi 22,haikuleta madhara makubwa japo wanafunzi 61 pamoja na walimu wao wawili walipata mshtuko mkubwa na kulazimika kulazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Katibu wa hospitali hiyo Kilwanila Kiiza alisema pamoja na baadhi yao kupata michubuko na mshituko, hawakuwa kwenye hatari kubwa na waliruhusiwa kwa awamu kurudi nyumbani.
Radi shule za Kagera
Pamoja na kuwa radi haizoeleki, lakini limekuwa jambo linalojirudia mara kwa mara katika shule tofauti za Mkoa wa Kagera na mara kadhaa huacha madhara.
Kwa mfano, moto wa radi ndio uliochukua uhai wa Angelika Frolian mwaka 2014 aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari Iluhya iliyopo Wilaya ya Bukoba aliyekuwa amejikinga mvua kwenye ukuta wa darasa.
Tukio la shule ya msingi Kyakailabwa pia linarejesha kumbukumbu ya vifo vya wanafunzi wawili wa shule ya sekondari Kamuli Wilayani Kyerwa waliopigwa na radi na kupoteza maisha mwaka 2014.
Ushuhuda walimu na wazazi
Mwalimu Kaijage ambaye sasa anafundisha Shule ya Msingi Bilele Manispaa ya Bukoba, wakati wa tukio lililoua wanafunzi wawili wa shule ya Kyakailabwa ndiye aliyekuwa mwalimu mkuu.
Pamoja na kuwa shule anayosimamia sasa haina historia ya matukio hayo, anasema hofu yao sio kubwa kwa kuwa ni majirani na uwanja wa ndege wa Bukoba wenye mitambo kwa majanga kama hayo.
‘’Radi inaogopesha na kujenga hofu nilishuhudia nikiwa Kyakailabwa walimu na wanafunzi walivyotaharuki baada ya kuua wanafunzi wawili na mama aliyekuwa na mtoto mchanga’’anasema.
Majanga mengine shuleni
Shule za Mkoa wa Kagera zimeandamwa na majanga kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na tukio la wanafunzi wanne wa shule ya msingi Tumaini ya mjini Bukoba kuuawa kwa bomu August,31 mwaka 1994.
Shule hiyo ambayo imehamishiwa eneo jingine baada ya kiwanja cha ndege kurefushwa, alama pekee iliyobaki ni mnara wenye majina ya wanafunzi wanne waliofariki siku ya tukio.
Pia tukio la karibuni zaidi ni wanafunzi watano wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Kihinga Wilayani Ngara, kufariki baada ya kulipukiwa na bomu walilokuwa wanamiliki baada ya kuliokota.
Hali sio nzuri Kagera na Kigoma
Matukio ya radi yanakuwa mengi mkoani Kagera hasa mjini Bukoba baada ya kupakana na Ziwa Victoria, kama ulivyo Mkoa wa Kigoma unaopakana na Ziwa Tanganyika.
Tafiti za hali ya hewa zilizofanyika kwenye Ziwa Victoria zinathibitisha kuwa mawingu yenye chaji hatari zinazotengeneza radi yako upande wa Magharibi na Mashariki.
Malundo anasema kuwa matukio hayo hayakwepeki kwenye miji ya Bukoba,Tarime na Kisumu nchini Kenya.
‘’Zile chaji haziwezi kukaa angani lazima ziingie ardhini; matukio haya yanatokea wakati wa asubuhi na jioni upande wa Kaskazini na Kusini. Tatizo sio kubwa kama pande nyingine za Ziwa Victoria,’’anabainisha Malundo.
Chukua tahadhari
Kitu kilichounguzwa na radi inashauriwa kisiguswe haraka au hatua hiyo ifanyike kwa tahadhari, kwa kuwa huwa bado kimezungukwa na chaji ambazo bado zinaelekea ardhini.
Inashauriwa kutumia kipande kikavu cha mti ambacho hakina maji maji yanayoweza kutumika, kama mkondo wa kusafirisha maji na kukufikia kwa urahisi.
Ni hatari zaidi kuwa chini ya mti wakati wa mvua kwa kuwa maeneo yenye vitu virefu ikiwemo miti hutumika kusafirisha chaji za radi kwenda ardhini.
Pia hakuna usalama ukitembea kwenye eneo la wazi wakati wa mvua, kwa kuwa linaweza kutumika kama kifaa cha kusafirisha chaji kwenda ardhini na kupoteza maisha.

No comments:

Post a Comment