‘’ Hapo unadhibiti tu mvutano wa hewa kwa kuwa na upanga yaani kata upepo katikati na nyuma. Huu upanga wa katikati ni kwa ajili ya kudhibiti kani mvutano na ule wa nyuma ni kwa ajili ya kuzuia ndege isiyumbe. Vitu hivyo ni muhimu na vikikosena vyote au kimoja kati ya hivyo, ndege itadondoka chini.”
Huyu ni kijana mtundu aitwaye Deogratius Charles, mkazi wa kijiji cha Bunga kilichopo mkoani Pwani, ambaye ana ndoto kuu ya kutengeneza mfano wa ndege na kuirusha.
Tangu akiwa mtoto, fikra zake hazikuwahi kutoka nje ya anachosema kutengeneza ndege na hatimaye kuirusha.
Sasa akiwa na miaka 26 amefanikiwa kutengeneza kifaa mithili ya helikopta anayosema amebakiza vifaa vichache iruke angani. Tena vifaa hivyo anasema havihitaji kiwango kikubwa cha fedha, akipata sh 1.2 milioni Charles ataanza kuirusha angani.
Anasema ndege hiyo inayotumia mafuta ya petroli na injini ya pikipiki kubwa za Kijapan, itakuwa na uwezo wa kukaa angani kwa saa tatu.
Ndege hiyo ameitengeneza kwa vifaa mbalimbali vikiwemo vyuma vya aluminiamu. Anasema ili iweze kuruka inahitaji mashine, mota pamoja na taa ambavyo kwa pamoja gharama zake zinafikia Sh 1.2milioni.
Alivyoanza ubunifu wake
Akiwa na umri wa miaka mitano, Charles anasema alipenda kuchora michoro mbalimbali wakati akicheza na wenzake hasa michoro ya ndege.
“Nilipenda kujifunza vitu mbalimbali kwa kuangalia, mathalani nikiona picha hata ya mnyama nachora kama ilivyo na wenzangu waliniita bwana chorachora,”anasema na kuongeza kuwa:
“Nilikuwa na rafiki yangu ana kitabu cha picha, nilipendelea kuangalia picha za helikopta nilivutiwa na picha zile kuanzia siku hiyo nikaweka ahadi ya kuwa mtengenezaji wa ndege,”anaeleza.
Kutokana na umri wake kuwa mdogo kwa kipindi hicho alitengeneza ndege ndogo kwa ajili ya kuchezea ambazo alitengeneza kwa kuangalia picha hizo za kwenye kitabu.
“Nilianza kutengeneza kwa kutumia maboksi, naangalia mchoro halafu naunda ya kwangu. Hapo ndipo nilipoanzia hadi kufikia hii kubwa ambayo naamnini ipo siku itapaa angani,” anasema.
Kwa kuwa ni kitu ambacho alipenda kutengeneza tangu akiwa mdogo, hakutaka kupoteza ubunifu wake kwani anasema utengenezaji wa chombo hicho utampa fursa ya kupata ajira katika kampuni za usafirishaji wa anga
“Lakini pia nilijaribu kuangalia kitu ambacho kitakuwa cha tofauti na wengine. Unajua hivi sasa ukiangalia wabunifu wengi wanatengeneza vitu vya kufanana, mimi chaguo langu limeangukia hapa,”anasema
Matarajio yake
Charles ana matarajio ya kurusha ndege yake siku moja ili hatimaye ajivunie ubunifu wake na kujitangaza kimataifa.
Mbali na hilo anatarajia kuwa mhandisi atakayeungana na wengine waliopo kutatua changamoto za usafiri wa anga nchini.
“Sipendi kuishia hapa nilipo, ndoto yangu siku moja niwe fundi bora kwa kutengeneza ndege mbalimbali zitakazosafiri ndani na nje ya nchi yetu,”anaeleza.
Anasema endapo atawezeshwa, atatengeneza ndege nyingi. Amefanikiwa kutengeneza ndege hiyo moja kutokana na kuwa na kipato kidogo.
Lengo la Charles ni kusaidia vijana wenzake kutoka katika wimbi la kuwa tegemezi, kwani anasema mradi wake ukiwa mkubwa kipaumbele cha kwanza kitakuwa ku fundisha vijana wenzake.
Changamoto
Haikuwa kazi ndogo kwake kufika alipo, kwa kuwa amepitia vikwazo kadhaa anavyosema alifanikiwa kuvivuka kwa sababu ya kuwa mvumilivu.
Anasema mara nyingi ndugu na jamaa walimkatisha tamaa, kwani wanafikiri kuwa anachokifanya ni sawa na kupoteza muda na fedha.
‘’ Niwe tu mkweli, kwa kipindi cha mwanzo, ndugu walinikatisha tamaa kwa kutoonyesha ushirikiano na kutaka fedha ninazotumia kununua vifaa bora, nizifanyie vitu vingine ikiwamo kujenga,”anaeleza.
Anasema kwa sasa ndugu hao wakiwamo wazazi wake wameanza kuelewa anachokifanya.
“Mwanzoni wakati naanza kuunda, waliona kama utani sasa hivi wakiona hatua niliyofikia wanafurahi na mimi napata faraja,”
Changamoto nyingine ni kutokuwa na fedha ya kutosha kwa ajili ya kununulia vifaa…. “Isingekuwa tatizo la fedha, nina imani hii ndege ingeshakamilika.’’
Anasema changamoto hizo zote na nyingine ndizo zinazosababisha ndege hiyo kuchelewa kuruka. Hata hivyo, anaamini kuchelewa huko sio sababu yeye kurudi nyuma kwa kuwa imani yake ni kuwa; ‘ipo siku itaruka’.
Wito wake kwa Serikali
Anatoa rai kwa Serikali kuunga mkono ubunifu wake kwa kumtembelea na ikiwezekana kukutanishwa na wabunifu wengine.
“Mimi naomba viongozi serikalini waje waone hiki chombo, pengine wanaweza kunishauri mengi ambayo yatanijenga zaidi katika safari yangu hii ya ubunifu wa ndege,”anaeleza.
Kwa kuwa changamoto yake kubwa ni fedha kwa ajili ya kununua vifaa, anasema kwa sasa kilio chake ni kupata Sh 1.2 milioni kwa ajili ya vifaa ili aweze kukamilisha matengenezo yaliyosimama kwa muda.
“Kipato changu ni kidogo, pea ninayopata katika kazi yangu ya ufundi magari na pikipiki inatosha kwa ajili ya kujikimu, lakini wakati mwingine najitahidi hivyo hivyo kujibana kuweka fedha kidogo kwa ajili ya vifaa,” anaongeza kusema.
Kwa kuwa aliishia elimu ya msingi, Charles anahitaji kupatiwa elimu ili kukuza ujuzi na maarifa aliyonayo.
“Nikipata nafasi ya kwenda chuo cha ufundi nitafurahi, nikiwa na elimu itajenga uaminifu katika kampuni mbalimbali za usafiri wa anga zitakapotaka kunichukua,” anasema.
Anasema Serikali itoe kipaumbele kwa wabunifu kwani kulingana na ukuaji wa sayansi na teknolojia, utakuwa na fursa nyingi za ajira na kupunguza wimbi la vijana wasiokuwa na kazi.
“Mimi naamini kama tutapatikana vijana 20 kama wabunifu tuna uwezo wa kutengeneza ndege zetu wenyewe zikafanya safari za ndani kuliko kununua kutoka nje,”.
Anasema wapo vijana wanaobuni vitu vingi lakini Serikali inashindwa kuwatambua kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kuwatembelea hasa wale waliopo maeneo ya vijijini.
Kwa sasa Charles, anaendesha maisha yake kwa kutengeneza pikipiki na magari, hata hivyo anasema ndoto yake haipo huko. Anahitaji msaada wa ujuzi zaidi ili atimize ndoto yake ya kuwa mhandisi wa ndege.
Kauli ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga
Charles anafanya haya yote akiwa kwa hajui lolote kuhusu taratibu za urushaji wa ndege, kama zinavyoainishwa na mamlaka husika.
“Sijui kama kuna taratibu zozote za kurusha ndege na nitakapokamilisha hivyo vifaa, natamani nionane nao ili wanipe mwongozo,” anasema.
Ofisa habari Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bestina Magutu anasema utaratibu uliopo ni kwamba ndege kabla haijaruka angani, mhusika anatakuwa kuwasiliana na mamlaka hiyo.
“Ni jambo zuri ila cha msingi kama anataka kuendelea mbele na ubunifu wake awasiliane na TCAA ili kujua ni jinsi gani anaweza kusaidiwa, lakini pia anavyoweza kupewa ushirikiano zaidi,”anaeleza.
Costech yamkaribisha
Hata Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), haitambui ubunifu wa Charles, licha ya ukweli kuwa tume hy imekuwa ikiwasaidia wabunifu na wagunduzi wanaojitokeza nchini
Huyo kijana hatumtambui lakini anaweza akaja katika ofisi zetu tukamshauri mambo mbalimbali. Inavyoonekana huyu kijana ni mtundu kwa kuwa ameweza kutengeneza bodi ya helikopta,’’ anasema mtafiti mwandamizi wa Costech Dk Georges Shemdoe.
Anasema tayari Tume imeanzisha kambi za ubunifu katika mikoa mbalimbali, kwa lengo la kuwasaidia wabunifu.
No comments:
Post a Comment